Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa akiwakaribisha wananchi kutoka mikoa
ya Kilimanjaro, Arusha, Tanga na Manyara waliofika nyumbani kwake
wilayani Monduli jana kumwomba atangaze nia na kugombea urais mwaka
2015.
Staili aliyotumia Mjumbe wa Halmashauri
Kuu ya Taifa ya CCM, Dk Raphael Chegeni kumshawishi Waziri Mkuu
mstaafu, Edward Lowassa agombee urais imetumika tena jana baada ya
makundi mbalimbali ya jamii kwenda nyumbani kwake Monduli na kumtaka
achukue uamuzi huo haraka.
Wakiwa nyumbani kwa Lowassa, wananchi hao kutoka
Kanda ya Kaskazini walimkabidhi Sh2,567,600 walizosema zimechangwa na
marafiki wa Lowassa kwa ajili ya kuchukulia fomu.
Miongoni mwa watu hao walikuwamo vijana, wazee,
wanawake, viongozi wa dini na watu wenye ulemavu wanatoka mikoa ya kanda
ya kaskazini ya Kilimanjaro, Arusha,Tanga na Manyara pamoja na wajumbe
watatu wa Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM na wenyeviti wawili wa Umoja wa
Vijana wa CCM (UVCCM).
Wananchi hao walifika nyumbani kwa Lowassa
wakitembea kwa miguu kutoka umbali wa kilometa moja huku wakiimba wimbo
wa “Tuna imani na Lowassa”.
Akisoma risala kwa niaba ya wananchi hao, Protas
Soka alisema kwa sasa Watanzania wanamhitaji Lowassa aweze kuwaongoza
kama Rais wa awamu ya tano.
“Tunakuomba usimame mbele ya Watanzania na utoe japo neno roho zao zitulie,” alisema Soka ambaye ni mlemavu wa ngozi.
“Kwa lugha nyingine mheshimiwa Lowassa sasa
tunakuomba utangaze nia ya kuingia kwenye kinyang’anyiro cha urais wa
Tanzania 2015. Wewe ni tumaini la walio wengi Tanzania,” alisema.
Kwa upande wake, mratibu wa marafiki wa Lowassa
Kanda ya Kaskazini, Noel Nko alisema Sh2.5 milioni walizomkabidhi,
zimechangwa na wananchi wa kawaida kabisa kutoka moyoni mwao.
Akizungumza na wananchi hao, Lowassa alisema yuko
tayari kutangaza nia wakati wowote lakini anasubiri tamko kutoka CCM na
huenda akatangaza nia hiyo mwanzoni mwa Aprili.
Lowassa alisema iwapo CCM itatoa tamko hilo,
atatangaza nia hiyo katika uwanja wa mpira wa Sheikh Amri Abeid Jijini
Arusha, akisema anaamini kundi hilo pia litamuunga mkono siku hiyo.
“Nimebubujikwa na machozi ya furaha kwa ujio wenu
huu. Ninawashukuru kwa tendo hili. Tukishafanikiwa katika safari yetu ya
matumaini tukutane tena hapa hapa,” alisema.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment