
Aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe.
Mapya yanazidi kuibuliwa juu ya sakata
linaloiandama Kampuni ya Reli Limited (TRL) ya uingizaji mabehewa feki
nchini, sasa ikifahamika kuwa hata Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya
Umma (PPRA), haikushirikishwa kwenye manunuzi hayo.
Kufichuka kwa ukweli huo, ndiko sasa kunaongeza hali ya wasiwasi
ndani ya TRL na kuna uwezekano mkubwa sakata hilo litaibua mjadala
katika mkutano wa 19 wa Bunge unaotarajiwa kuanza kesho mjini Dodoma. Ukweli huo uliwekwa wazi mwishoni mwa wiki na Mwenyekiti wa Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Uchumi, Viwanda na Biashara, Luaga Mpina, wakati
wa kikao cha kamati yake na PPRA.
Mpina alitoboa siri hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kikao baina ya kamati yake na PPRA. Alisema kamati yake iliwahoji PPRA kuhusu ushiriki wao kwenye
ununuzi wa mabehewa hayo na kubaini kuwa mamlaka hiyo haikushirikishwa. “Tunashangaa kwamba hata PPRA hawakushirikishwa kwenye mchakato wa
ununuzi wa mabehewa hayo. Hadi sasa ninapozungumza hawajawahi kuitwa
kushuhudia mabehewa 150 yaliyobainika kuwa ni feki,” alisema Mpina.
Mpina ambaye pia ni Mbunge wa Kisesa, alisema hali hiyo inaonyesha
mambo kufanywa kinyume cha taratibu katika mchakato mzima wa ununuzi wa
mabehewa hayo, hali aliyosema imechangia kuingiza hasara serikali kwa
kununua mabehewa feki. Ili kulishughulikia suala hilo sawa sawa, mbunge huyo alisema
kamati yake inatarajia kukutana na uongozi wa PPRA chini ya mkurugenzi
wake, Laurent Shirima Ijumaa wiki hii mjini Dodoma, kwa ajili ya kupata
taarifa zaidi kuhusu ununuzi wa mabehewa hayo feki.
Wakati huo huo, kamati iliyoudwa na aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi,
Dk. Harrison Mwakyembe, imewasilisha taarifa ya uchunguzi wake kwa Bodi
ya Wakurugenzi wa TRL kama walivyoagizwa na Waziri wa sasa wa Uchukuzi,
Samuel Sitta, ambaye anatarajiwa kukabidhiwa ripoti hiyo leo.
Mabehewa hayo yaliingizwa nchini kupitia kandarasi ya Kampuni ya
M/S Hindustan Engineering and Industrial Limited ya India ikishirikiana
na kampuni moja nchini inayomilikiwa na mfanyabiashara mmoja jina kwa
sasa linasitiriwa. Mfanyabiashara huyo amekuwa akijihusisha na biashara
nyingi za kulaghai mashirika ya umma na kujipatia ukwasi wa kupindukia.
Waziri Sitta ambaye alichukua hatua ya kusimamisha uingizaji wa
mabehewa mengine 124 yaliyosalia hadi hapo atakapopata taarifa ya
uchunguzi ya mabehewa ya awali ambayo yamebainika kuwa feki, amekwisha
kuweka wazi kwamba hatakuwa na simile kwa yeyote atakayehusika na kadhia
hiyo hata kama ana madaraka makubwa kiasi gani.
Mabehewa hayo yaligundulika kuwa mabovu baada ya kufanyiwa majaribio baadhi yalianguka kwa kukosa ‘stability’ yakiwa relini. Habari za ndani ya TRL zinasema kuwa, mabehewa hayo yaliyopokelewa
na Dk. Mwakyembe Julai 24, mwaka jana, hayakupitiwa na jopo la mafundi
wa TRL ili kuthibitisha ubora wake.
Ingawa Dk. Mwakyembe amekuwa akijiweka mbali na sakata hilo na
kueleza kuwa alijua tatizo mapema ndiyo maana akaagiza kamati ichunguze,
hataweka wazi ilikuwaje kwenda kuyapokea kwa mbwembwe wakati hakuwa na
ripoti kamili ya ubora wake na ufuataji wa sheria ya manunuzi katika
kutoa kandarasi hiyo kwa kampuni ya India kwa kushirikiana na
mfanyabiashara huyo.
Dk. Mwakyembe aliyapokea mabehewa hayo kwa bashasha, huku akieleza
kuwa ununuzi wake ni utekelezaji wa mpango wa serikali wa ‘Matokeo
Makubwa Sasa (BRN)”, ambao umelenga kuhakikisha reli inahimili
usafirishaji wa abiria na mizigo nchini. Menejimenti ya TRL imetajwa kwa nyakati mbalimbali na vyanzo vyetu ndani ya TRL kuwa na mikono katika kashfa hiyo.
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment