Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa
Sasa ni dhahiri kwamba ushawishi wa kumtaka Edward
Lowassa, awanie urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) umezidi kiasi
cha makundi ya wanachama wa chama hicho kupigana vikumbo nyumbani kwake
wilayani Monduli wakimtaka ajitokeze wakati ukifika.
Jana makundi hayo yalifika Monduli kwenye makazi ya Lowassa ambaye
pia ni mbunge wa jimbo hilo, yakiwa na fedha walizosema ni kwa ajili ya
kumpa ili akachukue fomu ya kuwania urais kupitia CCM wakati ukifika. Kundi la kwanza lililopiga hodi nyumbani kwa Waziri Mkuu huyo wa
zamani mjini Monduli jana kumshawishi na kumkabidhi fedha za kuchukulia
fomu, ni wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Arumeru.
Kundi hilo mbali ya kumshawishi Lowassa ajitose kwenye mbio za
urais kwa sababu anatosha kwenye kiti cha urais, walimkabidhi mchango wa
Sh. milioni moja za kuchukulia fomu ya urais kupitia CCM. Akizungumza katika ghafla hiyo fupi nyumbani kwa Lowassa, John Ole
Saitabau, ambaye ni mwenyekiti mstaafu wa halmashauri ya Meru, alisema
wamefikia hatua hiyo baada ya kuona Lowassa anatosha.
“Sisi tumekuja hapa kukushawishi uchukue fomu ya kuwania urais
kupitia chama chetu, uwezo huo unao Tanzania inakuhitaji,” alisema. Naye Mjumbe wa NEC, Mathias Manga, alisema zaidi ya asilimia 75 ya wajumbe wa NEC wanamshawishi Lowassa awanie urais.
Kundi la pili lililofika nyumbani kwa Lowassa jana ni la marafiki
wa Lowassa Kanda ya Kaskazini, lililojumuisha zaidi ya watu 500 kutoka
kada mbalimbali, wakiwamo walemavu wa macho, maalbino, ambao
walimkabidhi Lowassa Sh. 2,567,600 za kuchukua fomu ya urais.
Makundi hayo kutoka mikoani yaliwasili jana nyumbani kwake, kijiji
cha Ngarashi, wilaya ya Monduli, baada ya kufanya maandamano makubwa
yaliyoanzia njia panda ya Monduli, wakiimba nyimbo za matumaini kwamba
‘Wewe ni tumaini la walio wengi Tanzania, maamuzi na matumaini mapya,
Watanzania wako nyuma yako’.
Makundi hayo yaliyoongozwa na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa wa
Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kilimanjaro, Paul Matemu, Mratibu wa
Marafiki wa Lowasa Kanda ya Kaskazini, Noel Nnko, Mjumbe wa Mkutano Mkuu
wa Taifa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana (UVCCM), Mkoa wa
Arusha, Robnson Meitinyiku, Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa, Fred Mushi,
Askofu wa Kanisa la Calvary Assemblies of God, Christoher Madilu ambaye
pia ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa na Abdalah Sadick kutoka mkoa wa
Manyara.
Katika risala iliyosomwa na Protas Soka, kundi hilo linalojumuisha
vijana kutoka mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara, walisema
Watanzania wanamuhitaji Lowassa. “Kwa lugha nyingine Mheshimiwa Lowassa sasa tunakuomba utangaze nia
ya kuingia kwenye kinyang'anyiro cha urais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania 2015, wewe ni tumaini la walio wengi Tanzania,” alisema.
Kundi hilo pia lilipaza sauti kwa kulaalani vitendo vya mauaji
dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) na kwamba watasimama
kidete kuhakikisha ukatili huo una tokomezwa. Mbali na pilikapilika za jana nyumbani kwa Lowassa, Jumamosi
iliyopita (juzi) uongozi wa Shirika la Umoja wa Machinga Tanzania
(Shiuma) ulimtembelea Lowassa nyumbani Monduli, nao walimkabidhi Sh.
milioni moja za kuchukulia fomu kuwania urais kupitia CCM.
Mwenyekiti wa Shiuma, Matondo Masanja, akisoma risala yao kwa
Lowassa, alisema kuwa wamefikia hatua hiyo baada ya kumuona ndiye mtu
sahihi kumrithi Rais Jakaya Kikwete. “Tumejiridhisha juu ya uongozi wako ndani ya chama chako na katika
serikali, utumishi wako uliyotukuka, uwajibikaji na uzalendo wako
hususan katika kuwakomboa Watanzania na kuondoa umasikini,” alisema.
Pamoja na fedha hizo, pia walimkabidhi kadi ya uanachama wa Shiuma, wakisema Lowassa ameonyesha kuwa ni mwenzao. Viongozi wa shirika hilo ambalo makao yake yako Mwanza waliongozana
na wenyeviti wa Jumuiya ya Vijana ya CCM (UVCCM) kata za wilaya za
Nyamagana, mkoani Mwanza.
Wenyeviti hao nao pia walimtaka Lowassa atangaze nia. Walisema
Lowassa ndiyo tegemeo la vijana wanaokabiliwa na tatizo kubwa la ajira. “Umekuwa huchoki kupigia kelele tatizo la ajira kwa vijana ...
tunakuomba kuyakubalia maombi yetu na tunakuahidi kuwa tuko nyuma yako
kwa hali na mali kuhakikisha kuwa unapata ushindi mkubwa,” alisema Ahmed
Misanga, Mjumbe wa Halmashauri Kuu Wilaya Nyagamana.
Akizungumza baada ya kupokea maombi hayo, Lowassa aliwashukuru kwa
imani kubwa waliyoionyesha kwake na kuwaambia wamuombe Mungu ili jambo
hilo liende salama. Alisema anaendelea kumuomba Mungu amjaalie atimize ndoto yake ya safari ya matumaini. Aidha, alisema anajivunia mafanikio aliyoyapata wakati akiwa
mdhamini wa Umoja wa Vijana wa CCM kwa kusimamia umoja huo kupata
kitega uchumi kikubwa, ambacho ni jengo lililoko katika makao makuu ya
umoja huo jijini Dar es Salaam.
WENGINE WALIOMWENDEA LOWASSA
Tayari viongozi wa serikali, chama na wafugaji wa wilaya Mkinga walimchangia Lowassa Sh. 200,000 za kuchua fomu ya urais.
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment