
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe,
akihutubia mamia ya wananchi kwenye mkutano wa hadhara alioufanya katika
mji mdogo wa Mwandiga, mkoani Kigoma mwishoni mwa wiki. Katika mkutano
huo, Zitto, aliwaaga wananchi wa Jimbo la Kigoma Kaskazini kuwa
hatagombea ubunge wa jimbo hilo uchaguzi mkuu ujao Oktoba mwaka huu.Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, ametangaza kijivua ubunge wa jimbo hilo. Zitto ambaye alivuliwa uanachama na Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema) wiki iliyopita baada ya kushindwa kesi aliyoifungua
Mahakama Kuu ya Tanzania, alitangaza uamuzi huo jana katika mkutano wa
hadhara kwenye uwanja wa soko la kijiji cha Mwandiga, mkoani Kigoma.
Zitto hakueleza ni sababu zipi zilizomlazimisha kujitoa Chadema
zaidi ya kudai kuwa ni kutokana na migogoro ndani ya chama hicho. “Ndugu zangu mabibi na mabwana nawaaga rasmi kuwa mimi si Mbunge wa
Jimbo la Kigoma Kaskazini, nawatakia kila la kheri na tuko pamoja
katika kuijenga Kigoma yetu na nchi yetu kwa ujumla,” alisema Zitto.
Katika mkutano huo uliofurika umati mkubwa wa watu uliompokea Zitto
kwa kumbeba juu juu huku wakiimba “shujaa wetu ameingia, rais wetu
mtarajiwa ameingia” na akina mama wengi wakiangua vilio baada ya Zitto
kutangaza hatua hiyo. Aidha, baadhi ya wananchi walimpongeza Zitto kwa uamuzi huo ili
kuondokana na walichodai kuwa ni migogoro ya kisiasa inayoendelea katika
Chadema na kuahidi kushirikiana naye popote atakapokwenda.
“Mimi nimeamua kufanya kile kisichozoeleka katika siasa za nchi
yetu, nimeamua kujitoa kwenye nafasi ya ubunge, kwa kunipa jukumu hili
nikiwa kijana mdogo niliamini kuwa ushujaa wangu mzuri wa kusimamia
misingi ya maendeleo kwa wananchi wangu kuhakikisha huduma muhimu
zinawafikia nimezipigania,” alisema Zitto wakati akitangaza uamuzi huo. Alisema katika safari hiyo amepata marafiki wengi sana na pengine hata maadui wachache.
“Safari hii ya miaka 10 kuna watu niliwafurahisha na kuna watu
niliwaudhi, kwa wale niliowaudhi, nawaomba radhi na kwa wale
niliowafurahisha nawaomba wasiache kuniongoza na kunishauri kila
wakati,” alisema. Alisema haikuwa safari rahisi na hakutegemea iwe rahisi.
“Kiuhalisia ilikuwa ni safari ngumu yenye mafunzo makubwa na ilikuwa
safari kama kiongozi na pia kama safari binafsi ya kupevuka kifikra na
kupata mafunzo kuhusu maisha” alisema.
Hata hivyo, Zitto alisema anajivunia safari hiyo kwani ilikuwa ni
njema, hivyo ni wakati sasa wa kutoa nafasi kwa nguvu mpya kuongoza
jimbo hilo kushika kijiti alipoishia ili kurekebisha pale alipokosea na
kuimarisha pale alipofanikiwa. Aliwataka wananchi wa jimbo hilo kuacha kusononeka, kuumiza mioyo yao na kulia kutokana na hatua aliyoichukua.
Vilevile, Zitto alirudia kauli yake kuwa hatagombea tena ubunge
katika jimbo hilo Oktoba, mwaka huu, kauli inayoelezwa na wachambuzi wa
mambo kuwa, atagombea katika Jimbo la Kigoma Mjini. “Mimi sitakuwa Mbunge wenu baada ya uchaguzi mkuu wa mwezi Oktoba,
lakini nitaendelea kutetea maslahi ya mkoa wa Kigoma na taifa letu kwa
njia nyingine” alisema.
Kumekuwapo na habari mjini hapa kuwa, Zitto anatarajia kutangaza
kujiunga na chama cha ACT-Tanzania na kwamba kesho atakwenda kuaga
bungeni na Jumatano kujiunga rasmi na chama hicho jijini Dar es Salaam,
lakini NIPASHE lilipomuuliza, alisema anasubiri kufanya maamuzi ya
kushangaza.
KUVULIWA UONGOZI
Zitto ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu
za Serikali (PAC), alivuliwa na Chadema nafasi ya unaibu Katibu Mkuu na
Naibu Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, Novemba 22, mwaka 2013. Wengine waliovuliwa ni aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa
Arusha, Samson Mwigamba na Mjumbe wa Kamati Kuu, Prof. Kitila Mkumbo,
kwa tuhuma za kukisaliti chama.
MAAMUZI YA CC
Januari 3 na 4, 2014, Kamati Kuu ya Chadema ilikutana na kuwajadili
wanachama hao na kutoa uamuzi baada ya kupitia mashtaka 11 yaliyokuwa
yanawakabili. Januari 5, mwaka jana, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa,
alitangaza maamuzi ya Kamati Kuu, ambayo ni kuwatimua Mwigamba na Prof.
Kitila na kuwataka wanachama kutoshiriki mikutano nje na ya ndani au
shughuli yoyote ya kisiasa itakayofanywa na Kabwe au mawakala wake kwa
jina la Chadema.
Kabla ya kamati hiyo kukutana, Zitto kupitia wakili wake, Albert
Msando, alifungua kesi Mahakama Kuu ya Tanzania, kuweka zuio la
mahakama asijadiliwe katika kikao cha CC cha Januari 3, mwaka 2014
kuhusu uanachama wake hadi hapo rufani yake itakapotolewa uamuzi na
Baraza Kuu.
MASHITAKA DHIDI YAO
Mashtaka yaliyokuwa yanawakabili ni 11 yanayohusu ukiukwaji wa
vifungu mbalimbali vya katiba ya chama, kanuni za uendeshaji kazi za
chama, kanuni za kusimamia shughuli, mwenendo na maadili ya wabunge wa
chana na mwongozo wa kutangaza kusudio la kuwania nafasi ya uongozi
kwenye chama, mabaraza na serikali.
Alisema mashtaka yote yalitokana na watuhumiwa kuandaa kile
kinachoitwa mkakati wa mabadiliko, 2013, uliojikita katika kukashfu
viongozi wakuu wa chama, kutokuwa wakweli na wawazi kwa kushirikiana na
vikundi vya majungu kwa kuanzisha na kuratibu mtandao wa siri ulioitwa
‘mtandao wa ushindi’ nje ya utaratibu wa chama ili kumwezesha Zitto
kutwaa nafasi ya Mwenyekiti wa chama Taifa.
Mengine ni kutoa tuhuma za uongo dhidi ya viongozi wa chama na bila
kupitia vikao halali vya chama, kujihusisha na vikundi nyenye misingi
ya ukabila, udini na ukanda vyenye makusudi ya kubaguana ndani ya chama
na miongoni mwa jamii, kujihusisha na vikundi na vitendo vya
kuchonganisha au kuzua migogoro ndani ya uongozi wa chama na wanachama
wake.
Kuandaa na kutekeleza mpango wa kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa
chama Taifa bila kutangaza kusudio la kufanya hivyo kwa mujibu wa
mwongozo wa chama, kutengeneza makundi na mitandao haramu ya kuwania
uongozi ndani ya chama kinyume cha mwongozo wa chama, kuwachafua
viongozi na wanachama wenye nia au kusudio la kugombea nafasi ya
Mwenyekiti wa chama kinyume cha mwongozi wa chama.
Kwamba ushiriki wa Zitto ukweli huu unathibitishwa na mawasiliano
ya barua pepe iliyotumwa na Zitto kwa mtu anayejiita Chadema Mpya 2014
wa Oktoba 27, mwaka 2013, ikiwa ni mwezi mmoja kabla ya kikao cha CC
kilichowavua madaraka. Dk. Slaa alisema mkakati huo haukuwa na lengo la kumwezesha Zitto
kutwaa nafasi ya Mwenyekiti wa Taifa wa chama pekee, bali ulikuwa na
malengo makubwa zaidi ya kukibomoa chama kwa kukichafua kwa wananchi na
kuwachafua viongozi wake wa juu kwa kutumia tuhuma za uongo za ufisadi.
Alisema CC imeridhika kwa ushahidi wa nyaraka mbalimbali
zilizoandaliwa na Zitto ama mawakala wake wakitumia vitambulisho bandia
katika mitandao ya mawasiliano ya kijamii kwamba mkakati wa kukibomoa
chama umeandaliwa na kutekelezwa kwa muda mrefu.
Alisema mkakati huo ulihusisha pia hujuma dhidi ya chama kwa
kuwaengua wagombea wake katika chaguzi mbalimbali kama ilivyotokea
katika majimbo ya Mpanda Mashariki, Musoma Vijijini na Singida Mjini
ambako alidai Zitto alishiriki moja kwa moja. Hata hivyo, tuhuma hizo zilikanushwa na viongozi hao.
UAMUZI WA MAHAKAMA
Machi 10, mwaka huu, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam,
ilitangaza kutupilia mbali na kuifuta kesi iliyofunguliwa na Zitto dhidi
ya Kamati Kuu ya Chadema, baada ya kukubali pingamizi zilizowasilishwa
na chama hicho na kutakiwa kulipa gharama zote za kesi.
CHADEMA YAMFUKUZA
Muda mfupi baada ya hukumu hiyo, Mwanasheria Mkuu wa Chadema,
Tundu Lissu, alitangaza kumvua uanachama kwa madai ya kukiuka katiba ya
chama hicho ibara ya 8(a)(X) ya kukipeleka mahakamani.
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment