Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mhe. Aggrey Mwanri. Wabunge wanaotoka mikoa ya mipakani
wamelalamikia kuhusiana na watu wasio raia kupiga kura na kuchaguliwa
katika chaguzi kinyume cha sheria.
Wabunge hao ni Mbunge wa Viti Maalum, Josephine Genzabuke na Ally Keisy wote wa CCM walihoji juu ya tatizo hilo bungeni leo. Katika swali lake la msingi Genzabuke aliihoji
serikali juu ya wakimbizi waliopiga kura katika baadhi ya maeneo mkoani
Kigoma ikizingatiwa ulikuwa uchaguzi wa serikali za mitaa haukuwa na
vitambulisho maalum kama vile kadi ya kupigia kura.
Swali lililoulizwa pia na Keissy ambaye alisema
katika jimbo lake kuna wenyeviti wa vijiji na vitongoji ambao
wamechaguliwa wakati si raia wa Tanzania? Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri ofisi ya Waziri
Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa, Aggrey Mwanri alisema
serikali itakuwa tayari kushirikiana na mbunge ili kuchunguza suala hilo
na kuchukua hatua ya kulipatia ufumbuzi.
Hata hivyo, alisema ni jukumu la viongozi wa
vijiji, vitongoji na mitaa pamoja na wananchi kuwabaini watu ambao siyo
raia au wakazi wa eneo husika na kutoa taarifa kwa mamlaka husika ili
hatua ziweze kuchukuliwa. Alisema kwa mujibu wa kanuni kabla ya siku ya
uchaguzi orodha ya wapiga kura walioandikishwa hubandikwa katika kituo
cha kupigia kura ili kuwawezesha wananchi wa eneo husika kubaini watu
wasiokuwa na sifa wakiwemo wakimbizi au wasio wakazi wa eneo hilo.
CHANZO: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment