NINGEPENDA kuwauliza wasomaji wangu kwa nini
waandishi hawazingatii maelekezo na maoni kuhusu uandishi bora
yanayotoilewa mara kwa mara kupitia gazeti hili?
Inawezekana kuwa waandishi wanaosoma makala
zangu ama hawaelewi au hawapendi kubadilika. Hata hivyo, hatutakata
tamaa kwani taaluma ya saikolojia inadai kuwa wako watu wenye vichwa
vigumu kuelewa jambo na wako wepesi kukubali mabadiliko. Makala ya leo ni mwendelezo wa azma yetu ya
kuendelea kurekebisha makosa yaliyo katika magazeti kwa faida ya
waandishi na wasomaji kwa jumla.
Kwa mfano imeandikwa:
“ Ukiachilia mbali sakata hilo, mechi ya maafande hao ilifana.” Katika maelezo hayo hapo juu, maneno ‘ukiachilia
mbali’ yanatumika katika mazungumzo na ni mara chache tunayatumia katika
uandishi . Katika Kiswahili fasaha, maneno ‘ukiachili mbali’ hayafai
kutumika na badala yake tunatumia “Mbali ya sakata hilo, mechi ya
maafande hao ilifana.”
“ Tulisaini kujiunga na mchakato huu mwaka 2004
wakati huo Benjamin Mkapa akiwa Rais na Jakaya Mrisho Rais wa sasa akiwa
Waziri wa Mambo ya Nje.” Kwa kawaida jina la mtu linatakiwa kuwa na maneno
matatu ili kumtofautisha na mtu mwingine. Jina la Rais wa Awamu ya Tatu
ni Benjamin William Mkapa na Rais wa sasa ni Jakaya Mrisho Kikwete.
Jambo la pili ni kuwa kwa kuwa Rais wa sasa anafahamika hatumtaji na
kuanza kumwelezea yeye ni nani. Kwa hiyo maneno ‘Rais wa sasa’
hayahitajiki. Ingetakiwa kuandikwa,
“Tulisaini kujiunga na mchakato huu mwaka 2004
wakati huo Benjamin William Mkapa akiwa rais na Jakaya Mrisho Kikwete
akiwa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje.” “Wanahukumiwa kwa jinai dhidi ya binadamukatika matukio yaliyojiri baada ya Uchaguzi Mkuu wa mawaka 2007”.
Dhana inayopatikana hapa ni kwamba mwandishi
alikuwa akifikiri kwa kutumia dhana za kigeni. Kwa msomaji wa kawaida
hataweza kuelewa mantiki ya sentensi hii. Katika kuandika Kiswahili
fasaha, tunatumia neno jinai likifuatiwa na neno makosa. Kwa hiyo iwe
’makosa ya jinai’ na hivyo sentensi isomeke: “wanatuhumiwa kwa makosa
ya jinai dhidi ya binadamu katika matukio yaliyojiri baada ya Uchaguzi
Mkuu wa mwaka 2007.” ‘Lakini nje ya hiyo ni kwamba timu bora imepoteza mchezo.”
Waandishi wengi wanadhani kuwa kuandika maneno mengi ni kuipamba
lugha. Hii siyo sahihi. Ukweli ni kuwa tunatakiwa kuandika kwa ufupi
na kwa ufasaha. Maneno yasiyo ya lazima yaachwe kuandikwa kwani
katika utaratibu wa uandishi bora tunazingatia matumizi ya maneno
machache inavyowezekana. Kwa hiyo kuandika, Maneno ’Lakini nje ya hiyo
ni kwamba’ hayahitajiki. Tukiandika ‘Timu bora imepoteza mchezo’ msomaji
ataelewa.
“Watu wawili walikufa mkoani katika matukio
mawili tofauti kufuatia kunywa pombe haramu ya gongo.” Kosa moja
linaloonekana wazi ni kutokuutaja mkoa husika. Msomaji atapata shida
kuufahamu mkoa husika na hivyo kupoteza lengo lako. Pamoja na hayo kosa
jingine ambalo linajitokeza sana na limeshaingia katika fikra za
waandishi wengi ni ‘kufuatia’. Nilipoandika mara ya kwanza
niliwafahamisha wasomaji wangu kuwa ‘kufuatia’ ni utohozi wa neno
kufuata. Maana ya kufuata ni kwenda nyuma, kuandamana, ambatana,
n.k. Tunasema kufuata nyayo, kuifuata sheria. Kwa hiyo kufuatia ni kwenda
nyuma ya mtu au kitu. Kwa hyo siyo sahihi kusema matukio yalifuatia
kunywa pombe. Badala yake tunasema ‘kutokana na kunywa pombe.’
“Sasa katika makundi yetu, baada ya muda mchache tulifanikiwa kupata usafiri wa kutupeleka bandarini.”
Katika suala la muda, ni bora mhusika akatumia
muda mfupi au muda mrefu badala ya muda mchache au muda mwingi. Kutumia
neno ‘chache’ ambalo ni kielezi tunamaanisha kidogo, adimu, pungufu,
kutokea mara moja moja. "Nimewiwa kuandika makala hii kueleza mambo ya kifamilia.”
Maana ya ‘wia’ ni kutaka kilicho chako kutoka kwa
mtu mwigine au kudai. Mwandishi anasema ‘amewiwa’ kwa maana ya kusema
kuwa anajihisi kama anadaiwa na wanafamilia kuandika makala. Huu ni
msemo mgumu kueleweka kwa wasomaji wa kawaida ambao wengi wao ni wenye
kisomo cha kawaida.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment