Social Icons

Pages

Wednesday, March 18, 2015

TAIFA NJIAPANDA

Wakati Taifa likijiandaa kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, yamebainika mambo matatu mazito ambayo yanaliweka njiapanda , hali inayosababisha viongozi na hata wananchi kubaki na maswali lukuki wakihoji hatma ya nchi yao.Mambo hayo ambayo hadi sasa hayajulikani hatma yake ni Katiba Inayopendekezwa, Mahakama ya Kadhi na uboreshaji wa Daftari la Wapigakura kwa vifaa vya kielektroniki vya Biometric Voter Registration (BVR).
Mambo hayo yamekuwa  mjadala wa kitaifa kwa muda sasa, hoja kubwa ikiwa ni endapo matukio makubwa ya kitaifa – upigaji wa kura ya maoni kupitisha Katiba Mpya na Uchaguzi Mkuu wa Oktoba yatafanyika kwa mafanikio au yanaweza kukwama na kusababisha sintofahamu.

Uandikishaji BVR
Hoja kubwa katika eneo hili imekuwa ni iwapo kura ya maoni ya kupitisha Katiba itafanyika Aprili 30, mwaka huu kama ilivyopangwa, lakini Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva mara kadhaa amesimamia msimamo wa Serikali kuwa uandikishaji unaendelea bila matatizo katika Mkoa wa Njombe kama ilivyopangwa.
Ukiacha upungufu unaosababisha shughuli hiyo kuchukua muda mrefu, Jaji Lubuva amekuwa akikwepa kuzungumzia madai kuwa Serikali haikutoa fedha za kutosha kufanikisha shughuli hiyo, lakini juzi alikiri kuwa Tume yake ilijaribu hata kuazima vifaa hivyo Kenya na Nigeria bila mafanikio.
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amekaririwa na gazeti hili jana akisema hata bajeti ya mchakato huo ya Sh297 bilioni  iliyopangwa haipo kwa kuwa katika kasma ya tume zilikutwa Sh7.01 bilioni na fedha za maendeleo na fedha za tume hazikuonekana.
Profesa Lipumba alisema pia hata Sh144 bilioni za kura ya maoni zilizoelezwa na Tume hazikuonekana kwenye vitabu vya bajeti na kuwa BVR 250 zilizopo badala ya 8,000 zilizokusudiwa haziwezi kufua dafu.
Kuhusu muda uliosalia wa siku 42 kabla ya kura ya maoni, umeelezwa na wachambuzi kuwa hautoishi, ukilinganishwa na Kenya iliyokuwa na BVR 15,000 na ikaandikisha wapiga kura milioni 14 kwa siku kati ya 45 hadi 60. Kutokana na hali hiyo, kinachosubiriwa na wananchi ni ama kuelezwa ni muujiza gani utafanyika hadi shughuli hiyo kukamilika na kura ya maoni kupigwa bila matatizo au kuahirisha kura hiyo hadi wakati au baada ya uchaguzi mkuu.

Mahakama ya Kadhi      
Saula jipya kabisa katika mjadala wa uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi inayotambuliwa na Serikali ni kesi iliyofunguliwa Mahakama Kuu na Mwenyekiti wa DP, Mchungaji Christopher Mtikila akitaka mahakama itamke kuwa Mahakama ya Kadhi na masuala ya Jumuiya ya Kiislamu (OIC) ni haramu na itamke kuwa ulinzi na uhai na utu wa binadamu nchini hauwezi kubaguliwa na Uislamu.
Kesi hiyo iliyofunguliwa siku moja kabla ya Bunge kuanza mkutano wake wa 19 jana ambao pamoja na mambo mengine umepanga kujadili muswada wa marekebisho ya sheria mbalimbali, unaokusudia Mahakama ya Kadhi itambuliwe katika mfumo wa mahakama nchini, hali ambayo inaweza kubadili upepo katika chombo hicho cha kutunga sheria.
Hata hivyo, Mkurugenzi  wa Shughuli za Bunge, John Joel alisema hadi jana chombo hicho hakikuwa na taarifa yoyote kutoka mahakama kuhusu kesi ya Mahakama ya Kadhi. Kwa siku za karibu suala la Mahakama ya Kadhi limeingia katika mjadala kutokana na ahadi ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliyoitoa bungeni kuwa Serikali ingeleta muswada huo ili kuitambua lakini isingewekwa katika Katiba Inayopendekezwa.

Katiba Inayopendekezwa
Katiba Inayopendekezwa ilipita katika misukosuko mingi na imeendelea kupingwa na baadhi ya makundi ya jamii, vyama vya siasa huku ikiungwa mkono na chama tawala na Serikali yake. Huku ikiendelea kupigiwa chapuo kupitia vyombo vya habari, mikutano ya kisiasa ya chama tawala na baadhi ya makundi, vile vile imeendelea kupingwa na makundi mengine, jambo ambalo ni dhahiri limeacha mgawanyiko kitaifa.
Vyama vya upinzani chini ya umoja wao wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wameweka msimamo wa kuendelea kuipinga na kujiweka kando katika mchakato wake, huku baadhi ya viongozi wa dini wakitoa matamko yanayoeleza msimamo wa kuipigia kura ya hapana Katiba hiyo.
Tamko la karibuni kabisa ni lile la Jukwaa la Wakristo lililotolewa na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) na Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPCT) lililoelekeza waumini kupiga kura ya Hapana kwa Katiba Inayopendekezwa.
Siku chache baada ya tamko hilo, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo aliibuka na kupingana na tamko hilo akisema waumini waachwe waamue wenyewe aina ya kura wanayoitaka, hivyo akaagiza tamko hilo lisambazwe na kusomwa makanisani ili waumini waamue wenyewe cha kufanya. Hata hivyo, Ushirika wa Wachungaji wa Kipentekoste Tanzania (PPFT), umetoa kauli yake ukionya taasisi za kidini zinazotumia mwavuli wa dini kwa maslahi binafsi kuacha kuwaburuza katika suala la Katiba mpya. Matamko hayo ya viongozi wa dini yameliweka Taifa kwenye kona na kuwaacha waumini wao na hata wananchi wengine wasijue washike lipi na waache lipi.

Kauli ya Serikali
Hata hivyo, akizungumzia matamko hayo, Kaimu Kiongozi wa Shughuli za Serikali bungeni jana, Samuel Sitta alisema mvutano uliopo kati ya Jukwaa la Wakristo Tanzania na Pengo kuhusu kuipigia kura ya “Hapana” Katiba Inayopendekezwa hauwezi kubadili msimamo wa Serikali kuhusu upigaji wa kura hiyo.
Sitta, ambaye pia ni Waziri wa Uchukuzi na aliyekuwa mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, alisema waumini waachwe wachague aina ya kura watakayopiga, kama viongozi hao wa dini wamegawanyika hamna namna ya kuwafanya wawe na kauli moja.

Maoni ya wadau
Kutokana na hoja hizo zinazolibana Taifa, waziri wa zamani wa mambo ya nje na mwanasiasa mkongwe nchini, Ibrahim Kaduma alisema: “Sikuwa natarajia kama ipo siku viongozi wetu watawadhihaki wananchi, kwani haiwezekani uwaambie kuwa kura ya maoni itafanyika Aprili 30, wakati uandikishaji unavyokwenda hauridhishi, hii ni kuwadhihaki tu.”
“Tumefanya makosa, turudi nyuma na tutumie uandikishaji kwa daftari letu, kisha tufanye uchaguzi na Kura ya Maoni, kwa kutumia BVR inahitaji mwaka mmoja au miwili zaidi kuhakikisha tunaandikisha watu wote.”
Alisema, “Tatizo Serikali haipo tayari kusikiliza ushauri kwani tulishasema huwezi kuandikisha watu wote kwa kipindi hiki kilichobaki, lakini haikusikia, hizo mashine zikimaliza kuandikisha zibaki hapo kwa ajili ya kuwaingiza watu wanaofikisha umri wa kuandikishwa na mchakato huu uwe endelevu, jambo ambalo sidhani kama litafanyika.”
Spika Mstaafu wa Bunge, Pius Msekwa alisema, “Kutojua ukweli ni adui mkubwa, wanazungumza Katiba hawajaisoma kuzungumzia jambo ambalo hujui ukweli wake ni tatizo, tusizungumze jambo kama hulijui undani wake.” Akizungumzia tamko la maaskofu alisema, “Kama Mkristo limenikwaza, sana lakini nilipata faraja na tamko la Kardinali Pengo. Kwanini  umnyime uhuru kupiga kura aipendayo, imenikwaza sana hii.”
“Usiwaelekeze jinsi ya kupiga kura kwani inajulikana na wanachotakiwa kukifanya ni kuwaelekeza kilichomo ndani ya Katiba hiyo na siyo kuwaeleza kwamba kapigeni kura ya hapana, hii siyo sahihi kwani ni watu wazima wanaweza kuamua wao wenyewe,” alisema Msekwa.
Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), Gration Mukoba alisema nchi inapoelekea inahitajika mtabiri wa hali ya juu atakayetabiri Tanzania ya mwaka 2016 itakuwaje. “BVR na vitambulisho vinavyotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) havina tofauti, lakini hawa Nida wana zaidi ya mwaka sasa na wakazi wa Dar es Salaam hawajapata wote, sasa kweli NEC watamaliza uandikishaji kabla ya Aprili 30, hii ni ndoto.”
Akizungumzia Mahakama ya Kadhi alisema, “Hivi leo tukiipitisha Mahakama ya Kadhi, kesho wanga nao watataka mahakama yao na makundi mengine yatajitokeza yakitaka mahakama yao nchi iko katika wingu zito sana,” alisema Mkoba ambaye pia ni rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT).
 Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk Ernest Mwasalwiba alisema, “Mahakama ya Kadhi ina mkanganyiko kwani elimu haijatolewa vya kutosha, mfano mtu asiyehusika nayo atafaidika nayo vipi, lakini kuna makundi yanapingana, nani atakayeiongoza, itatoa wapi fedha za kujiongoza haya yote yalitakiwa kutolewa ufafanuzi.”
Kuhusu BVR Dk Mwasalwiba alisema, “Muda uliobaki ndiyo unaolalamikiwa. Suala la kupiga kura ya maoni ni la wananchi, kwamba wapige au wasipige hilo lipo mikononi mwao.” Aliongeza, “Haya matamko nisingeungana sana nayo kuwa upige kura ya hivi, lakini walichopaswa au wanachopaswa kukifanya viongozi wa dini na Serikali ni kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi kuhusu mchakato huu.”
Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Billy Haonga alisema, “Uwezekano wa kura ya maoni kufanyika Aprili 30 ni mgumu kwani kama Njombe mpaka sasa hawajamaliza itakuwaje nchi nzima kumaliza kwa kipindi hicho.” “Kinachotakiwa kufanyika sasa ni mawazo ya busara kutumika kura ya maoni iahirishwe na uandikishaji uendelee kwa umakini na inawezekana kabisa ukafanyika pamoja na uchaguzi mkuu siku hiyo hivyo kwani inawezekana kabisa.”

CHANZO: MWANANCHI

No comments: