Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju.
Wakati Mkutano wa 19 wa Bunge la 10 ukitarajiwa
kuanza kesho mjini Dodoma, hadi sasa Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria
na Utawala, haijauona Muswada wa Mahakama ya Kadhi.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Jasson Rweikiza, akizungumza na NIPASHE
kwa njia ya simu jana, alisema kamati yake haijauona muswada huo bali
Katibu wa kamati alipigiwa simu na kuelezwa kuwa kuna muswada
utapelekwa.
“Kama ujuavyo tunafanya kazi kwa maandishi na siyo kwa simu, kama
kungekuwa na muswada huo Spika angeniandikia Mwenyekiti wa Kamati. Hadi
ninavyoongea sasa sijauona na sitegemei kama kwa sasa utaletwa na
kuufanyia kazi,” alisema.
Kauli ya Mwenyekiti huyo inakuja huku kukiwa na ahadi ya serikali
kwa muswada huo kuwasilishwa bungeni, huku Jukwaa la Wakristo Tanzania,
likipinga kwa kuwa hauhusiani na masuala ya kiserikali.
Makundi ya dini za Kiislamu na Kikristo kwa nyakati tofauti yametoa
kauli za kudai kuhamasisha waumini wao kutoipigia kura Katiba
pendekezwa iwapo suala hilo halitakwenda kwa jinsi pande zinavyotaka.
KAULI YA MWANASHERIA MKUU
Mwezi uliopita Mwanasheria Mkuu wa serikali, George Masaju,
alivieleza vyombo vya habari kuwa Mahakama ya Kadhi haitakuwa na athari
yoyote hasi nchini. Alisema tatizo lililopo ni kwamba serikali haijachukua hatua
madhubuti kuwaelimisha wananchi namna ambavyo mahakama hiyo itakuwa
inaendesha kazi zake.
“Suala la Mahakama ya Kadhi limekuwapo tangu zamani na ilikuwa
ahadi za Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005,
serikali hatuoni kwa nini suala hili lisifanikiwe,” alisema.
Masaju alisema Watanzania lazima watambue kuwa Mahakama ya Kadhi
itahusu mambo ya Waislamu wenyewe ambayo ni mirathi, ndoa na talaka na
haihusiani kabisa na mambo mengine au watu wa dini jingine ikiwamo
makosa ya jinai.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment