
Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) wakiangalia moja la
bweni lililokuwa likiteketea leo katika hostel za Mabibo.
Jengo la ‘Block
B’ la Hostel za Mabibo, za wanafunzi wa kike wa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam (UDSM), jijini hapa limeungua kwa moto na kuteketeza vifaa na
mali kadhaa za wanafunzi waliokuwa wakiishi kwenye jengo hilo. Tukio hilo lililotokea leo majira ya 2:35 asubuhi linadaiwa kusababishwa na hitilafu ya umeme katika jingo hilo.
Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa Rwekaza Mukandala
aliyekuwa eneo la tukio akiahidi kubeba dhamana ya kushughulikia hasara
ya mali, nyaraka na fedha kwa wanafunzi walioathiriwa na tukio hilo. “Kwanza kuhusu vyeti vilivyoungua ,tutashughulikia
vipatikane vyote.Pili tutashughulikia hata bajeti za kujikimu kwa wale
walioathirika, lakini pia kuanzia leo wanafunzi wote ambao walikuwa
kwenye jengo hilo watahamishiwa jengo lingine wakati huo uchunguzi
ukifanyika kufahamu chanzo cha moto,” alisema Profesa Mukandala.
Kwa upande wake, Kamanda wa Mkoa wa Kinondoni,
Camilius Wambura alitoa tahadhari ya usalama kwa mali za wanafunzi
walioathiriwa na tukio hilo huku akisisiza utulivu wakati uchunguzi wa
chanzo hicho ukifanyika.
Taarifa kutoka miongoni mwa wanafunzi hao
zimebainisha kuwa, wakati wa tukio hilo wanafunzi wawili wa kike
waliruka kutoka gorofa ya pili mpaka chini na kujeruhiwa vibaya. Askari wa Zima Moto walifika eneo la tukio hilo
saa 3:45 asubuhi na kukuta moto ukiwa umeshapungua hatua iliyosababisha
wanafunzi hao kuwashambulia huku wakiwazomea na kuwataka waondoke.
Viongozi wawili wa zima Moto, Omary Katonga kutoka
Ilala na Mboke Msami wamesema changamoto kubwa iliyojitokeza ni
kutopata taarifa mapema. “Moto umetokea saa 2:35 asubuhi kwa nini
watujulishe tena kupitia Tanesco saa moja baadaye, tumefika hapa kwa
kutumia dakika 23, wanakosea kutulaumu ila kinachotakiwa ni taarifa
mapema,” amesema Katonga.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment