Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe
Takribani miezi mitatu na ushei tangu sakata la
uchotwaji wa fedha zaidi ya Sh. bilioni 200 katika akaunti ya Tegeta
Escrow kutikisa nchi huku mawaziri wawili na mwanasheria mkuu wa
serikali wakiondoka madarakani na katibu mkuu mmoja akichunguzwa,
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe,
amefichua kuwa wajumbe wote wa kamati hiyo wataadhibiwa vibaya kwenye
majimbo yao kama njia ya kulipiza kisasi kutokana na kuwaumbua wote
walionufaika na fedha hizo.
Katika mahojiano na kituo cha ITV kwenye kipindi cha Dakika 45,
kilichorushwa jana usiku, Zitto amesema kuwa wakati PAC wakiendelea
kuchambua ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)
juu ya Escrow, mjumbe mmoja wa kamati hiyo aliitwa na ‘wakubwa’na
kuelezwa kwamba akifika bungeni awageuke wenzake na aseme kuwa mgogoro
wa ripoti ya Escrow iliandikwa kwa shinikizo la mfanyabiashara mmoja.
“Mmoja wa wajumbe wangu aliitwa kuombwa aingie bungeni aseme kwamba
kuna mfanyabiashara mmoja mkubwa amewapa wajumbe wa PAC fedha ili
watengeneze hiyo ripoti ya PAC,” alisema. Aliongeza kuwa mjumbe huyo alipokataa aliambiwa: “ Umekataa
kutekeleza hili? Sasa tumetenga Sh. milioni 500 kwa kila jimbo kwa kila
mjumbe wa PAC ili kuhakikisha hawarudi bungeni.”
Hata hivyo, Zitto hakutaka kumtaja mfanyabiashara huyo. Zitto alifafanua kwamba maana ya fedha hizo ni kwamba watu hao
watatafuta wagombea wa kupambana na waliokuwa wajumbe wa PAC kwa nguvu
ya fedha ili wahakikishe wanakwama kutetea majimbo yao katika uchaguzi
mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Aliongeza kuwa kitendo cha kutaja wanufaika wa Escrow wazi wazi,
kama vile majaji, mawaziri na wengine wote alijua kuwa hawawezi kukubali
jambo hilo lipite hivi hivi tu. “Kuna watu wana fedha nyingi bwana. Kwa mfano IPTL kwa mwezi wanalipwa capacity charge Sh. bilioni nne,” alisema.
Kwa hiyo, kitakachoendelea kwenye uchaguzi mkuu wajumbe wa PAC
watawekewa watu wa kupambana nao kuanzia kwenye kura za maoni, hata
wakishinda watawekewa wapinzani katika majimbo yao na fedha nyingi
zitatumika kuhakikisha wanaangushwa. Wajumbe walioshirikia uchambuzi wa
ripoti ya Escrow ndani ya PAC walikuwa 17.
Wajumbe hao ni Zitto, Deo Filikunjombe, Desderius Mipata, Asha
Jecha, Lucy Owenya, Ester Matiko, John Cheyo, Zaynabu Vulu, Ally Keissy,
Zainab Kawawa, Kheri Ali Khamis, Faida Mohammed Bakar, Ismail Aden Rage
na Modestus Kilufi.
Walioongezwa ni Kangi Lugola, Luhaga Mpina na Dk. Hamisi Kigwangalla. Hata hivyo, Zitto alisema hadi sasa hana ushahidi kwamba kesi yake
dhidi ya Chadema imetupwa mahakamani kwa sababu za Escrow, ingawa
anasisitiza kwamba mkakati wa kutengeneza majungu na mambo ya ovyo ovyo
dhidi ya wajumbe wa PAC ulianza wakati wa kujadili ripoti yao bungeni
mwaka jana.
JE, AMENUFAIKA NA MGAWO WA ESCROW?
Zitto anasema kuwa tuhuma kwamba naye alinufaika na fedha za Escrow
hazina msingi wowote na alikwisha kusema kuwa suala hilo lichunguzwe
baada ya kuibuliwa maneno ya kuokoteza na kuwasilishwa bungeni. Alitoboa siri nyingine kwamba usiku wa kuamkia siku ya PAC
kuwasilisha ripoti yake kuhusu Escrow bungeni, kila mbunge anakoishi
chini ya mlango wake lilipenyezwa kabrasha lililokuwa limejaa habari za
kupika, nia ikiwa ni kubadili upepo ili kuonyesha kuwa naye (Zitto)
alikuwa amenufaika na fedha hizo.
“Wanadai kwamba eti nami nilimtumia dada mmoja alikwenda kuomba
fedha kwa niaba yangu ili nimuuguze mama yangu,” alisema Zitto na
kuongeza kuwa: “Huu ni uongo tu mama yangu alikuwa mjumbe wa Bunge Maalum la
Katiba, matibabu yake na gharama zote za matibabu yake zilikuwa
zinalipwa na Bunge hilo. Sasa mimi niombe hela ya kumtibu wakati gharama
zilikuwa zinalipwa zote?”
ESCROW NA BARAZA LA MAADILI
Hata hivyo, Zitto anasema kuwa sakata la Escrow kwa mara nyingine
tena limeibua hoja nzuri kwamba bado taifa hili lina vyombo vya
kuthibiti uwajibikaji kwani wote waliotajwa kwenye mgawo wameitwa na
Baraza la Maadili kwa njia ya wazi kabisa na mashauri yamesikilizwa.
Anakumbusha kwamba miongoni mambo yaliozungumzwa na Tume ya Rushwa
ya Jaji Warioba ni tatizo kubwa la ufisadi na rushwa na kwamba hali hiyo
imezidi kustawi nchini kwa kuwa hakuna mfumo madhubuti wa uwajibikaji.
Alieleza kwamba kuibuka kwa Baraza la Maadili na kuwahoji wanufaika
wa mgawo wa Escrow ni kielelezo kingine kwamba mifumo ya uwajibikaji
nchini inaweza kufanya kazi.
MAGUMU KATIKA SIASA
Katika mahojiano hayo, Zitto alisisitiza kwamba bado ni mbunge wa
Kigoma Kaskazini kwa sababu anaamini mchakato wa kumvua uanachama ndani
ya Chadema kwa mujibu wa katiba na kanuni za chama chake haujafuatwa.
Anaamini kwamba baada ya kesi yake kutupwa na mahakama atapata
fursa ya kuitwa, ajitetee na ikibidi akate rufani kama taratibu za chama
zinavyosema. Hata hivyo, anasema ni makosa kwa chama cha siasa kinachotafuta
madaraka ya dola kuzuia wanachama wake kwenda mahakamani kwani kufanya
hivyo ni sawa na kuikataa katiba ya nchi ambayo imesema wazi kwamba
chombo cha juu kabisa ndani ya nchi cha kugawa haki ni mahakama.
Anatamani aibuke mwanachama wa Chadema aende mahakamani kupinga
kanuni hiyo kwani ni kinyume cha katiba ya nchi na kwa kweli inakinzana
na haki za msingi za binadamu. Katika mahojiano hayo, Zitto anataja miaka ya 2007 na 2014 kama
miaka migumu kwake kisiasa akiwa amepita katika mabonde na milima mingi.
Anautaja mwaka 2007 kwamba ndipo aliposimamishwa ubunge na Bunge
kwa madai ya kusema uongo baada ya kusema kwamba aliyekuwa Waziri wa
Nishati na Madini, Nazir Karamagi, alikuwa amesema uongo bungeni kuhusu
mkataba wa Buzwagi.
Anasema pamoja na ukweli huo, kufukuzwa kwake kulikipa chama chake
fursa ya kutembea nchi nzima na kueleza wananchi juu ya matatizo ya
mikataba ya madini, hatimaye mwaka 2008 Rais Jakaya Kikwete aliunda
kamati ya Jaji Bomani kuchunguza sheria na sera ya madini ambavyo
vilipatikana vipya.
Mwaka wa 2014 anautaja kuwa wa changamoto nyingi zaidi kwake kwani
ndiyo aliopoteza mama yake mzazi, Bibi Shida Salum. Alifariki dunia
Jualai mwaka jana baada ya kuugua kwa muda. Zitto anasema mwaka jana unakuwa wa kumbukumbu kwake kwa sababu
katika hali ambayo hakutarajia alijikuta anakipeleka chama chake
mahakamani ili kupata haki yake baada ya kuvuliwa nyadhifa ndani ya
chama hicho, lakini bila kwanza kusikilizwa.
Anaamini kwamba alichaguliwa na wananchi wa Kigoma Kaskazini siyo
kwa sababu tu ya kuwa mwanachama wa Chadema kwani idadi ya wanachama hao
haizidi 3,000 wakati kura zake zilikuwa ni zaidi ya 27,000. Katika
mazingira hayo ni lazima atafute haki yake na kuheshimu uamuzi wa
wananchi wa Kigoma Kaskazini.
Magumu mengine ni jinsi alivyoshughulikia suala la Escrow, ingawa
lilikuwa ni jambo zito, anafarijika kwamba amefanikiwa kusaidia taifa
kujenga uwajibikaji kwani wapo watu wameachia ngazi kwa sababu ya ripoti
ya PAC.
NINI MAJALIWA YAKE
Zitto anaamini kwamba yote yanayotokea ni majaribio ya kisiasa, na yana maana kubwa kwake kwani anaandaliwa kwa mkubwa zaidi. Anataja wanasiasa wakubwa duniani ambao walipitia changamoto kubwa
na nzito kuliko zake kuwa ni pamoja na aliyekuwa Waziri Mkuu wa India,
Indira Gandhi. Aligombana na chama chake akiwa waziri mkuu akaenda
kuanzisha chama kipya na kureja tena kuongoza India.
Alimtaja pia Mahathir Mohamed wa Malaysia kuwa alifukuzwa akiwa
mbunge, lakini baadaye akaja kuwa waziri mkuu wa nchi hiyo kwa miaka
zaidi na 20 na ndiye alileta mapinduzi makubwa ya uchumi kwa kufuta
umasikini kutoka asilimia 56 ya wananchi wote hadi asilimia tatu.
Zitto pia anamtaja aliyekuwa katibu mkuu wa chama cha Kikomunisti
cha China miaka ya sitini, Deng Xiaoping, kwamba alitofautiana na
wakubwa nchini kwake na kuwekwa kizuizini mara tatu, lakini baadaye
alikuja kuwa kiongozi wa taifa hilo na anatajwa kuwa ndiye chimbuko wa
maendeleo ya China ya sasa.
Wanasiasa wengine aliowataja kuwa wamepitia tanuri la kukataliwa na
kuadhibiwa ni pamoja na Aziz Bouteflika wa Algeria, ambaye alikuwa
mbunge na kukimbizwa nchini kwake na kwenda kuishi uhamishoni Ufaransa,
lakini baadaye alifuatwa na kuomba kuja kugombea urais na kuongoza nchi
hiyo.
Kwa Tanzania alimtaja Maalim Seif Sharif Hamad kwamba alifukuzwa
CCM akiwa Waziri Kiongozi, akawekwa kizuizini, akaja kuibuka na CUF na
sasa ni Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar. Zitto aliwataka wale wote walioanza kuandika tanzia yake ya kisiasa
kuwa na subira kidogo kwa kuzingatia historia ya viongozi wengine wa
kisiasa duniani.
DEMOKRASIA NDANI YA VYAMA
Anasema demokrasia ndani ya vyama ipo na inatofautiana kati ya chama na chama. Haiwezi kuwa sawa na fomula ya Coca Cola. Anaamini kwamba kila chama kina mfumo na uratatibu wake, ila la msingi ni vema kila chama kiheshimu haki za wanachama wake.
CCM ITAFUFUKA KWA KUWA UPINZANI
Zitto pamoja na changamoto zinazomkabili kwa sasa anasema kuwa bado
anamini kwamba CCM imechoka na kama inataka iwe na mabadiliko ya kweli
ya kioungozi na kuleta mabadiliko ni lazima ikae kando kwenye madaraka
ya dola. “CCM hata ifanye nini kama haitakuwa upinzani haitabadilika. CCM imeleemewa sana uchovu,” anasema.
BVR NA KURA YA MAONI
Anaamini kuwa mchakato wa kuandikisha wapiga kura katika daftari la
wapigakura kwa mfumo wa BVR una changamoto nyingi. Hata hivyo anawataka
wananchi kujiandikisha kwa wingi zaidi kwa sababu bila kufanya hivyo
watapoteza haki yao ya kupiga kura.
Anazungumzia mchakato wa katiba mpya na maandalizi ya kura ya maoni
kuhusu katiba hiyo kwamba ni jambo linalopaswa kuwekwa pembeni kwa kuwa
kwa sasa limekaa katika mkao wa kuwagawa wananchi. Anasisitiza kuwa mchakato wa kuandikisha katiba mpya ulivurugwa.
WENYE NACHO Vs WASIOKUWA NACHO
Anakumbusha kuwa toafuti ya kipato nchini baina ya wenye nacho na
wasio na kitu ni kubwa sana. Anaeleza kuwa hali hiyo isiposhughulikiwa
taifa halitasimama. Alisema tofauti na Kenya kwa mfano watu wa kipato cha kati (middle
class) ni wengi, kwa maana hiyo hata pale machafuko yalipotokea Kenya
mwaka 2007 na 2008, wenyewe walikubaliana kukaa kuzungumza, tofauti na
Tanzania kundi la kati ni wachache sana na hakuna wa kuwasilikiza.
“Wasiokuwa nacho nchini ni wengi mno, wakinyanyuika hawa nchi
haitakuwako. Kwanza wana hasira na hao wachache wa kipato cha middle
class,” anaonya na kutaka mipango endelevu ipatikane kukabili tofauti ya
kipato na umasikini unaokabili jamii.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment