Social Icons

Pages

Tuesday, March 31, 2015

MUSWADA WA BARAZA LA VIJANA WAKOSOLEWA

Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara.
Wabunge wameijia juu serikali kuhusu muswada wa sheria ya Baraza la Vijana wa mwaka 2015, wakipinga vifungu vilivyompa Waziri wa Vijana mamlaka ya kuteua Mwenyekiti wa Baraza hilo na wajumbe wa bodi.
Muswada huo ambao uliwasilishwa bungeni jana na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara, vifungu hivyo vimepingwa pia na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii na Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni.
Akiwasilisha maoni ya Kamati hiyo jana, Mwenyekiti wake, Said Mtanda, alisema kamati ilifanya marekebisho katika kifungu cha 4 (3), kinachozungumzia uanachama wa vijana kwenye baraza hilo utokane na wale waliojiunga na asasi za kiraia zilizosajiliwa na badala yake kijana yeyote mwenye umri wa miaka 15 hadi 35, wajiunge kwa hiyari yao.
Pia, Kamati hiyo imepinga kifungu cha 5 (7) (a) kinachompa waziri mwenye dhamana mamlaka ya kuteua Mwenyekiti wa Baraza la Vijana na badala yake vijana kupitia Mkutano wake mkuu wamchague mwenyekiti wao. Kadhalika, kamati imependekeza pia kuwa muundo wa baraza hilo uende hadi ngazi ya Kata badala ya kuishia wilayani.
Naye msemaji wa kambi ya upinzani katika wizara hiyo, Joseph Mbilinyi, alisema kwa mamlaka ya Waziri kutaka kuteua Mwenyekiti na wajumbe wa bodi, serikali itakuwa inaunda shirika la umma na siyo Baraza huru la vijana.
Mbilinyi alisema kambi hiyo baada ya kuuchambua kwa kina imebaini kuwa serikali imeuleta kuwahadaa vijana kwa kuwa ni kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu. “Kambi Rasmi ya Upinzani baada ya kuuchambua kwa kina muswada huu tumegundua kuwa umelenga kuanzisha shirika la umma badala ya kuunda chombo huru cha kuwaunganisha vijana nchi nzima bila ubaguzi wa kiitikadi, rangi, kabila na tamaduni zao. Muswada huu umempa mamlaka Waziri ya uteuzi wa viongozi na bodi ya usimamizi, huu ndio mtindo unaotumika katika uteuzi wa wakurugenzi wakuu na wenyeviti wa mashirika ya umma,” alisema.
Aliongeza kuwa: “Vijana wa Tanzania hawataki kuwa na shirika la umma, wanataka kuwa na baraza huru.”
Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, alisema muswada huo haujazingatia maoni ya wadau na kwamba utaunda baraza bovu akieleza kuwa ni afadhali lisiundwe kuliko mapendekezo ya muswada huo yapite.
Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Esther Bulaya, alipinga mamlaka ya Waziri kuteua Mwenyekiti na wajumbe wa bodi akieleza kuwa itaondoa uhuru wa baraza hilo. Vile vile, alitaka vijana wawe huru kujiunga badala ya kulazimishwa kujiunga kwa kupitia kwenye asasi zilizosajiliwa kwa mujibu wa sheria na kutaka baraza lifike hadi ngazi ya Kata.
Mbunge wa Kalenga (CCM), Godfrey Mgimwa, alitaka baraza liende hadi ngazi ya Kata na kwamba elimu iwe ni sifa mojawapo ya mtu kuteuliwa kuongoza baraza hilo.
Mbunge wa Nzega (CCM), Dk. Hamis Kigwangalah, naye alipinga madaraka ya Waziri kuteua viongozi wa baraza huku mbunge wa Viti Maalum (CUF), Kuluthumu Mchuchuli, alitaka vijana wajiunge kwa hiyari na kwa kadi maalum kwenye baraza hilo na kwamba idadi ya wajumbe kwenye baraza ngazi ya Mkoa na Wilaya izingatie idadi ya watu, kata na ukubwa wa eneo.
Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Margaret Sitta, alipendekeza kuwa serikali iandae utaratibu wa kutoa mafunzo ya ufundi mbalimbali na pia kila Halmashauri ihakikishe inatenga asilimia tano ya fedha za vijana kila mwaka.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: