
Mhasibu mzoefu
nchini, Leonard Mususa ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi
wa Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL), akichukua nafasi ya
Zuhura Muro.
Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Francis Nanai
alimpongeza Mususa kwa uteuzi huo akisema ujuzi wake unahitajika zaidi
katika kipindi hiki ili kuikuza na kuiendeleza kampuni. “Mususa amekuja Mwananchi wakati mzuri ambao
kampuni inahitaji ujuzi wake, akiwa Mwenyekiti wa Bodi, atasaidia
kuikuza na kuiendeleza,” alisema Nanai. Kampuni ya MCL inachapisha
magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti.
Alisema katika siku za karibuni, MCL imepitia
changamoto nyingi hasa baada ya Serikali kupunguza bajeti katika
matangazo, wafanyabiashara kutangaza zaidi katika runinga na redio na
mabadiliko ya namna wasomaji wanavyopata habari (kukua kwa mawasiliano
kwa njia ya teknohama). “Haya yote yana athari kubwa katika sekta ya
habari, changamoto hizi zinaathiri idadi ya usambazaji wa magazeti na
mapato. Hata hivyo, MCL imejitahidi kupambana na changamoto hizo na
kuendelea kushika usukani katika sekta zote, usambazaji, mapato na
matangazo,” alisema Nanai.
Mwenyekiti wa Kampuni ya Nation Media Group (NMG),
kampuni mama ya MCL, Wilfred Kiboro alimkaribisha Mususa kwenye Bodi ya
MCL na NMG na kusema kampuni imebahatika kumpata mtu mwenye ujuzi na
weledi. “Mususa ameungana nasi katika kipindi chenye
changamoto nyingi lakini pia ni kipindi chenye fursa, tunautegemea zaidi
mchango wake ili kuwa na gazeti lenye weledi katika ukanda wa Afrika
Mashariki,” alisema Kiboro.
Akizungumzia uteuzi wake, Mususa aliipongeza MCL akisema imekuwa ikifanya kazi nzuri na kujenga soko imara kwa miaka mingi. “Ninapongeza timu ya MCL, wakurugenzi, wafanyakazi
na bodi kwa kile walichokipata katika kipindi hiki chote kigumu hapa
nchini,” alisema.
Mususa aliyewahi kuwa Mwakilishi mwenza wa Kampuni
ya Ukaguzi ya Price Housewater Coopers Ltd nchini kwa miaka 14, alisema
akiwa ndani ya MCL atahakikisha wasomaji wanapata kilicho bora.
Akizungumzia mikakati kazi ndani ya MCL, mwenyekiti huyo alisema:
“Tutatathmini dhamira ya magazeti yetu, tutaangalia nyanja za usambazaji
na kuhakikisha idadi kubwa ya wasomaji wanapata habari zetu na habari
zetu zinapatikana katika majukwaa mengine ya kihabari.”
Alisema MCL itaendelea kuandaa timu ya waandishi
bora wenye ujuzi wa juu wa mawasiliano ambao wanaelewa mahitaji ya
kihabari ya wasomaji wao. “Nataka MCL iendane na mabadiliko yaliyopo katika
sekta ya habari. Haina budi kutoa habari za uhakika na sahihi kwa
wasomaji,” alisema.
Wajumbe wengine wa Bodi ya MCL ni Profesa wa
Kitivo cha Sheria Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Palamagamba Kabudi,
aliyekuwa mkurugenzi mtendaji wa Foundation for Civil Society, John
Ulanga; mhasibu, Hanif Jaffer na mfanyabiashara na mhandisi, Mohamed
Rweyemamu.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment