Social Icons

Pages

Monday, March 30, 2015

KAULI YA JK KUHUSU RIPOTI YA CAG IUNGWE MKONO


Juzi Rais Jakaya Kikwete wakati akipokea Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka unaoishia Juni 2014, alitoa maagizo makali baada ya kubaini ndani ya ripoti hiyo kuna madudu mengi ya matumizi mabaya ya fedha za umma.
Kwa jinsi ripoti hiyo ilivyotoa taswira mbaya kwa Serikali kuhusiana na matumizi ya fedha za umma, Rais Kikwete aliamua kuviagiza vyombo vya Serikali kubaini maofisa wote wa Serikali wanaohusishwa na matumizi mabaya ya fedha za Serikali, ikiwa ni pamoja na kutoa malipo bila nyaraka zozote, kutumia fedha nje ya Bajeti na kutoa malipo bila idhini ya ofisa masuhuli, ili wachukuliwe hatua kali za kisheria.
Pia, Rais Kikwete ameagiza kuchukuliwa kwa hatua kali za kisheria kwa maofisa wote wa serikali ambao wanahusika kulipa mishahara hewa kwa watumishi ambao wameacha kazi, wamefariki dunia, wamestaafu na wanaendelea kulipwa mishahara kupitia akaunti zao za benki.
Rais pia ameiomba Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi kuisaidia serikali kuboresha mfumo wa zabuni ambako serikali inapoteza fedha nyingi kwa kupitia mchakato mrefu mno wa kupatikana kwa wazabuni wa kutoa vifaa na huduma kwa Serikali.
CAG), Profesa Mussa Juma Assad, aligundua malipo yasiyokuwa na nyaraka, hati za malipo ambazo hazikuwasilishwa kwa ukaguzi, fedha iliyotumika nje ya bajeti, matumizi yasiyokuwa na manufaa (nugatory expenditure) na malipo ambayo hayakuidhinishwa na maofisa masuuli.
Profesa Assad alimweleza Rais Kikwete pia kuwa Ofisi yake inapendekeza kuwa taasisi zote za serikali zisiendelee kununua vifaa na huduma kutoka kwa wafanyabiashara wasiotumia mashine za stakabadhi za kielektroniki (EDF), stakabadhi ya kukiri kupokea fedha.
Mbali na udhaifu katika maeneo hayo, bado ugonjwa sugu wa watumishi hewa umeendelea ambapo kwenye ripoti ya CAG ya mwaka ulioishia Juni 2011, kiasi cha Sh1 bilioni kililipwa kama mishahara kwa watumishi wa halmashauri ambao hawapo; kutokuwasilishwa kwa vitabu vya stakabadhi za mapato kutoka halmashauri vyenye thamani ya Sh4,227,984,618.
Ni dhahiri mwaka baada ya mwaka CAG amekuwa akitoa ripoti nzuri na mara nyingi kumekuwa na maswali ya umma kwa ujumla wake, kwamba nini faida ya kuwa na ripoti hizi mwaka baada ya mwaka kama wahusika hawafanywi lolote kutokana na upungufu yanayojitokeza kwenye ripoti hiyo?
Tunaviomba vyombo husika kumsaidia Rais Kikwete kwa kuitekeleza kwa vitendo kauli yake ya kuwachukulia hatua za kisheria wale wote wanaotajwa ndani ya ripoti ya CAG kwamba wanahusika na matumizi mabaya ya fedha za umma.
Kuna wakati huko nyuma Rais Kikwete aliwahi kusema kuwa katika maeneo ambayo ripoti ya CAG inaonyesha dhahiri kulikuwa na wizi wa fedha za umma kwa watumishi, taarifa ipelekwe polisi na wahusika washtakiwe.
Sisi tunasema kauli ya Rais Kikwete ni ya kuungwa mkono kwa kuvitaka vyombo husika kuchukua hatua za kisheria bila kuchelewa na kwa kutenda haki. Ni muhimu kwa vyombo hivyo kufanyia kazi kwa haraka kauli hiyo ya Rais Kikwete.

CHANZO: MWANANCHI

No comments: