Askofu Josephat Gwajima.
Familia ya Kiongozi wa Kanisa la Ufunuo na Uzima,
Askofu Josephat Gwajima, imeeleza hofu yake kwamba imeshangwazwa na
hali ya afya ya kiongozi huyo kubadilika ghafla akiwa mikononi mwa Jeshi
la Polisi akihojiwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, katika Hospitali ya TMJ
jijini Dar es Salaam, mke wa Askofu Gwajima, Grace Gwajima, alisema
familia bado haielewi ni kwa namna gani Askofu huyo alizimia ghafla
wakati aliondoka nyumbani akiwa mzima wa afya.
Alisema kama familia kuna vitu vinavyowachanganya na hawapati
majibu haraka ikiwamo la Askofu Gwajima kuondoka nyumbani akiwa mzima wa
afya huku akitembea, lakini muda mfupi baadaye anapelekwa hospitali
akiwa amezimia akihojiwa na polisi. “Tunahisi kuna kitu amefanyiwa, kwa maana haiwezekani mtu aondoke
nyumbani akiwa wa afya, lakini baadaye kidogo tunapewa taarifa amezimia
yupo TMJ, hapa kutakuwa na kitu,” alisema Grace akiwa na mmoja walinzi
wa Askofu Gwajima.
HALI YA ASKOFU GWAJIMA
Akizungumzia hali ya Askofu Gwajima, aliyelazwa hospitalini hapo
kwa siku tatu, Grace alisema mumewe anaendelea vizuri na madaktari
walikuwa wanajiandaa kumtoa chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi
maalum (ICU) jana na kumpeleka wodi ya wagonjwa wa kawaida. Alisema kwa sasa Askofu Gwajima anaweza kuongea, kula chakula na
hata kuzungumza na watu mbalimbali wanaofika kumjulia hali. “Kuna
improvement zimeaza kujitokeza, ki ukweli kuna hali ya uzima na
anaendelea vizuri,” alisema Grace.
Hata hivyo, waandishi wa habari walizuiwa na uongozi wa Hospitali
ya TMJ kwenda kumwona Askofu Gwajima na badala yake walimwita Grace
azungumze na waandishi.
KUKAMATWA KWA WACHUNGAJI
Mke wa Askofu Gwajima (Grace), alidai kuwa juzi usiku Polisi
walifika hospitalini hapo na kuwakamata wachungaji 30 waliofika kumjulia
hali Askofu Gwajima.Alidai kuwa Polisi waliwakamata wachungaji hao pamoja na magari yao na kuwapeleka kusikojulikana.
“Jana usiku kulizuka tafrani hapa hospitalini, Polisi walifika na
kuwakamata wachungaji wapatao 30 wa Kanisa la Ufufuo na Uzima na
kuondoka nao,” alidai Grace hata hivyo, NIPASHE lilimtafuta Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya
Dar es Salaam, Suleiman Kova, kuthibitisha taarifa hizo, lakini alisema
angetuma taarifa hiyo kwa vyombo vya habari. Hata hivyo, hadi
tunakwenda mitamboni Kova hakutuma taarifa hiyo.
ULINZI WAIMARISHWA HOSPITALINI
Hali ya ulinzi katika Hospitali ya TMJ iliimarishwa ndani na nje ya eneo hilo, kwa kuwapo kwa askari waliovalia nguo za kiraia. Askari hao walionekana wakiimarisha doria nje ya wodi aliyolazwa Askofu huyo na kuzuia watu kusogelea wodi hiyo.
Nje ya hospitali hiyo kulikuwapo na gari la Polisi lililokuwa
limeegeshwa likiwa na askari waliovalia nguo za kiraia, huku wengine
wakiingia ndani na kutoka kila mara. Mbali na askari hao, pia walinzi wa Askofu Gwajima nao walionekana wakiwa karibu na wodi hiyo.
Ijumaa iliyopita, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam
lilimhoji Askofu Gwajima kwa tuhuma za kumkashifu na kumtukana hadharani
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Policarp
Kardinali Pengo.
Muda mfupi wakati wa mahojiano hayo yakiendelea, Askofu Gwajima
alizimia ghafla akiwa kwenye chumba cha mahojiano katika Kituo cha
Polisi Kati. Kufuatia hali hiyo, Askofu huyo alipelekwa katika hospitali tofauti
ikiwamo ikiwamo Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na mwishowe
kupelekwa TMJ.
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment