Social Icons

Pages

Monday, March 30, 2015

NYALANDU: ELIMU, MAJI SAFI, AFYA, ULINZI NI VIGEZO KWA MGOMBEA

Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, amesema moja ya mambo yanayoangusha wagombea kwenye uchaguzi ni kushindwa kuwapatia wananchi huduma muhimu kama elimu, afya, maji safi na ulinzi.
Nyalandu alitoa kauli hiyo juzi jijini Dar es Salaam wakati Chama cha Wanafunzi waliosoma shule ya Sekondari Ilboru (IAF) iliyopo Arusha walipokutana kupanga mikakati ya kuchangisha fedha kwa ajili ya kuikarabati shule hiyo.
Wanafunzi hao akiwemo Nyalandu wameguswa na matatizo ya uchakavu wa majengo ya shule, mabweni, maktaba na nyumba za walimu hivyo wameamua kukusanya nguvu ya pamoja kuikarabati ili kuirudhisha kwenye hadhi yake. Hadi sasa wameshakarabati madarasa manne ambayo awali paa zake zilikuwa kwenye hatari ya kudondoka kutokana na uchakavu.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Nyalandu alisema duniani wanasiasa wamekuwa wakishindwa au kupoteza nafasi zao za uongozi kwa sababu ya mambo machache. “Tunashindwa au kupoteza nafasi kama uchumi unakuwa haupo sawa, afya, usalama wa watu na mali zao na elimu unakuta changamoto ni kubwa,” alisema.
Nyalandu alisema shule ya Ilboru ilivyo sasa inasikitisha kutokana na uchakavu wa vyumba vya madarasa na majengo mengine licha ya kufanya vizuri kitaaluma. “Nilimaliza kidato cha sita shuleni pale mwaka 1993, walimu walitujengewa utamaduni wa umoja na maadili mema, tunapaswa kuienzi shule hii ili vizazi vya sasa na baadaye viweze kunufaika na elimu itolewayo hapo,” alisema na kuongeza:
Alitoa rai kwa chama hicho kuhakikisha wanafanya mchakato wa kuwatambua wanafunzi wote waliosoma shuleni hapo ambao kwa sasa wapo ndani na nje ya nchi ili wachangie. Alipendekeza siku ya uzinduzi wa uchagiaji waifanye iwe ‘live’ kwenye vyombo vya habari ili wadau wengine watakaoguswa waweze kutoa michango yao.
Mwenyekiti wa IAF, Dk. Daniel Maro, alisema kuwa, mwaka jana baadhi ya wana Ilboru walichangia kiasi kidogo ambacho kiliwezesha kukarabati madarasa manne ambapo gharama kwa darasa moja ilikuwa ni kati ya Sh. milioni 4 hadi Sh. milioni 5 kulingana na uchakavu.
Alisema lengo walilonalo ni kurekebisha mabweni, maktaba ambayo hivi sasa inachangamoto kutokana na kuwa na vitabu vya zamani huku ikikosa meza na viti. Pia alisema michango ikijitosheleza watakarabati pia nyumba za walimu ambazo zipi kwenye hali mbaya.
Alisema baadhi ya wadau ambao wamedhamini shughuli hiyo IPP Media, mifuko ya kijamii kama GEPF, PPF wengine ni BG Tanzania na Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA).

CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments: