
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Ernest Mangu.
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)
kimemtaka Rais Jakaya Kikwete kutengua uteuzi wa mkuu wa wilaya ya
Chato, mkoani Geita, kwa madai ya kukiuka kwa makusudi Katiba ya nchi
aliyoapa kuilinda.
Aidha, kimemtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Ernest
Mangu, kumtimua kazi Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Chato (OCD), Alex
Mukama, kwa madai ya kujiingiza kwenye siasa za kukilinda chama tawala
badala ya kulinda raia na mali zao.
Akizungumza na waandishi wa habari juzi, Katibu wa Chadema Wilaya
ya Chato, Mange Ludomya, alisema Rais Kikwete anatakiwa kutengua uteuzi
wa mkuu wa wilaya hiyo, Rodrick Mpogolo, kwa sababu amekuwa kikwazo cha
maendeleo ya wananchi kutokana na kuamuru Jeshi la Polisi kuwapiga na
kuwakamata viongozi wa chama hicho na kuwafungulia mashitaka.
Alisema hatua hizo zimekuwa zikichukuliwa kwa kivuli cha agizo la
Rais Kikwete la ujenzi wa maabara na kudai viongozi wa Chadema 55
wakiwamo wenyeviti wa vijiji na vitongoji 26 wamekamatwa na polisi na
kufunguliwa kesi za kuwazuia wananchi kuchangia ujenzi huo.
Ludomya alisema mkuu huyo wa wilaya amekiuka Katiba, Ibara ya 146
(1), inayoeleza madhumuni ya kuwapo kwa serikali za mitaa ni kupeleka
madaraka kwa wananchi. Mkuu wa Wilaya ya Chato, Rodrick Mpogolo, alipotafutwa kuzungumzia
malalamiko hayo, alisema anatekeleza agizo la Rais Kikwete la ujenzi wa
maabara nchini na kwamba ameagiza kukamatwa viongozi hao kwa kuwa
wanawazuia wananchi kuchangia kiwango kilichoamriwa na kamati za
maendeleo ya kata (WDC).
Mkuu wa Polisi Wilaya ya Chato, alipotakiwa kuzungumzia malalamiko
dhidi yake, alisema hizo ni changamoto katika utendaji wa kazi zake na
kutaka malalamiko hayo yaelekezwe kwa jeshi la polisi siyo kwake.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment