Social Icons

Pages

Wednesday, March 18, 2015

SERIKALI IACHE MAIGIZO, ITEKELEZE MAJUKUMU HAYA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Jakaya Mrisho Kikwete 
Mambo yanayoendelea kufanyika nchini hivi sasa wakati wananchi wakitakiwa kujielekeza katika masuala muhimu yanayohusu mustakabali wa Taifa letu yanaweza kufananishwa na maigizo kama siyo sarakasi.
Katika historia ya nchi yetu, hakuna wakati ambapo wananchi walijikuta wakitakiwa kutekeleza majukumu makubwa ya kitaifa kwa wakati mmoja kama ilivyo mwaka huu. Bahati nzuri wananchi wanatambua kwamba majukumu hayo ni mazito na muhimu, hivyo yanahitaji umakini mkubwa katika utekelezaji wake.
Tutakuwa hatujakosea tukisema kwamba majukumu hayo yanayowakabili wananchi mwaka huu ni ya kihistoria, kwani wanapaswa kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapigakura ili waweze kupiga Kura ya Maoni kuhusu Katiba Inayopendekezwa Aprili 30 na pia kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba, mwaka huu. Wananchi wanatakiwa kusoma Katiba Inayopendekezwa kwa umakini mkubwa ili waweze kufahamu maudhui yake kabla ya kuipitisha au kuikataa katika kura hiyo ya maoni.
Sheria ya Kura ya Maoni inataka elimu ya uraia kuhusu Katiba Inayopendekezwa itolewe kwa siku 60 na kampeni za kuunga mkono au kukataa Katiba hiyo zifanyike kwa siku 30 kabla ya kura hiyo ya maoni. Ni wazi kwamba muda uliobaki hautoshi kukidhi matakwa ya Sheria ya Kura ya Maoni, huku uandikishaji wa wapigakura kwa kutumia mashine za kielektroniki za BVR ukiwa unasuasua sana kutokana na matatizo mbalimbali. Mpaka sasa uandikishaji unaendelea katika mkoa mmoja tu wa Njombe, huku mikoa mingine 29 nchini ikiwa inasubiri kuanza kwa kazi hiyo. Serikali imesisitiza kwamba kazi hiyo itamalizika katika muda uliopangwa, ingawa wananchi wengi siyo tu wamepoteza matumaini ya kufanyika kwa Kura ya Maoni katika muda uliobaki, bali pia wanaona utakuwa muujiza wa kipekee kazi hiyo kumalizika kwa muda katika mazingira kama hayo.
Hofu ya wananchi wengi ni kwamba siasa imegubika masuala hayo kwa kiasi kikubwa na kusababisha viongozi kutoa kauli tatanishi zisizoendana na hali halisi, huku wananchi wakiwa hawaoni utekelezaji wa masuala hayo kama Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na Sheria ya Kura ya Maoni zinavyoelekeza. Kwa mfano, pamoja na mchakato wa kupata Katiba Mpya kuanza miaka minne hivi iliyopita, wananchi wameshuhudia porojo kuliko vitendo kwa upande wa viongozi na wanasiasa. Ndio maana inashangaza kuona kwamba Serikali imeipatia Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), mashine za BVR 250 tu badala ya mashine zaidi ya 8,000 zinazohitajika kuandikisha wapigakura nchi nzima.
Kama tulivyosema awali, kinachoendelea mpaka sasa ni kama maigizo au sarakasi. Masilahi ya Taifa yamewekwa kando na baadhi ya watu wamechukulia mchakato wa kupata Katiba Mpya na kuelekea Uchaguzi Mkuu kama fursa ya kutimiza ndoto zao. Wananchi wanajiuliza: Imekuwaje Serikali ishindwe kupata fedha za kununua mashine 8,000 za BRV, badala yake ifuje fedha ikizunguka katika nchi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Kenya na Nigeria kuazima mashine za BVR bila mafanikio? Nini hiyo kama sio aibu iliyopitiliza kwa Taifa letu kwa kufanya mzaha kwa mambo nyeti kwa mustakabali wa Taifa letu kama kupata Katiba Mpya na kufanya Uchaguzi Mkuu?
Imebaki miezi saba tu kufanya Uchaguzi Mkuu. Kwa mwendo huu wa uandikishaji wa wapigakura, nani anasema muda huo utatosha? Nani anasema muda uliobaki kabla ya kupiga Kura ya Maoni unatosha?

CHANZO: MWANANCHI

No comments: