
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashid.
Wagonjwa wa figo nchini wameiomba serikali
kuanzisha mfuko maalum wa kusaidia kifedha matibabu ya ugonjwa huo ambao
matibabu yake yana gharama kubwa ndani na nje ya nchi.
Wagonjwa hao walitoa rai hiyo wakati wa sherehe fupi iliyoandaliwa
na Hospitali ya TMJ, jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya kuadhimisha
Siku ya Figo Duniani juzi. “Tunaiomba serikali kuanzisha mfuko maalum ambao utasaidia matibabu
ya figo na magonjwa mengine ambayo matibabu yake wagonjwa wengi
hawawezi kuyamudu kutokana na gharama kubwa,” walisema.
Mmoja wa wagonjwa hao, Robson Mashamba, alisema mgonjwa mmoja wa
figo anatumia Sh. milioni moja kwa wiki kwa ajili ya kusafisha damu,
wakati wagonjwa wengi wanaohitaji huduma hiyo ni maskini wasio na uwezo
wa kumudu gharama hizo kubwa. “Serikali lazima isaidie wagonjwa wa figo ambao wanaongezeka kwa kasi nchini,” alisema.
Mgonjwa mwingine, Kabuchi Enock, aliitaka serikali itoe kupaumbele
kwa wagonjwa wa figo, kwa kuweka utaratibu maalum wa kusaidia matibabu
yao na kushauri kuwa wagonjwa wote wa ugonjwa huo waingizwe katika
utaratibu wa Mfuko wa Bima ya Afya.
Pia alitoa pendekezo kwa mamlaka husika kujenga vituo vya kutolea
huduma kwa wagonjwa wa figo nchi nzima katika ngazi za kanda ili
kuwapunguzia adha wagonjwa hao, pamoja gharama kubwa za matibabu na
umbali mrefu kutoka vijijini kwenda Dar es Salaam kufuata tiba. Charles
Mdoe, mgonjwa mwingine alishauri serikali na wadau wa sekta ya afya
kuweka mikakati ili kuhakikisha wagonjwa wa figo wanatibiwa ndani ya
nchi badala ya kuwapeleka nje.
Akizungumza na wagonjwa, Mganga Mkuu mstafu, Dk. Gabriel Upunda,
alisema kuna dalili njema kwamba matatizo mengi ya figo yataanza
kutibitiwa ndani ya nchi. “Kwa jinsi ninavyoona mwelekeo, ndani ya miaka miwili au mitatu,
tiba ya magonjwa ya figo itapatikana hapa nchini na kutoa mfano wa Kituo
cha Kubadilisha Figo (Kidney Transplant) kinachojengwa na Hospital ya
TMJ.
Akizungumza kuhusu mradi huo, Mkurugenzi Mkuu wa hospitali ya TMJ,
Dk. Tayabali Jafferji, alisema maabara ya kubadilisha figo itakamilika
ndani ya mwaka mmoja na nusu na kuongeza kuwa hospitali hiyo itatoa
matibabu yote yanayohusu figo.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment