Social Icons

Pages

Wednesday, March 18, 2015

CCM IRUHUSU WAGOMBEA WAJITANGAZE RASMI


Inashangaza kwamba kufikia leo hii, CCM bado inawazuia wanachama wake kutangaza kugombea urais. Chini chini, idadi ya wanaotaka kugombea nafasi hii inaongezeka. Wengine wanataka wenyewe, wengine wanasakiziwa.
Ukweli ni kwamba, ingawa nafasi ya urais ni moja tu, wanaoitamani ni wengi kupindukia. Vyama vingine vimebaki kimya, si kwamba vinazuia mtu kujitangaza labda ni mbinu za kutaka kusubiri kwanza kuona chaguo la CCM ili wajipange. Ila bado hatujasikia tamko la kuwazuia wanachama wa upinzani kujitokeza kugombea kama tunavyosikia kutoka CCM.
Unaweza kuiba, wakafumba macho, unaweza kukosa uzalendo, wakafumba macho, unaweza kushindwa kuwajibika wakafumba macho, unaweza kutoa roho ya mtu wakafumba macho, lakini ukitangaza kugombea urais kabla ya muda, unawekwa kifungoni. CCM wanashangaza! Ukali wanaouonyesha kwa watu wanaojitangaza mapema unatisha. Wangekuwa wakali kwa mambo mengine ya msingi, Taifa letu lingekuwa mbele zaidi. Mwaka jana, CCM iliwafungia wanachama wake sita waliojitokeza kujitangaza kugombea.
Wakapata adhabu ambayo hadi leo ni kama inaendelea maana, hakuna uwazi. Katika dunia ya leo ya sayansi ya teknolojia, bado mambo yanaendeshwa kama uchawi vile.
Tukihesabu siku, zinakwenda. Tungependa kuwafahamu wagombea, tungependa kuwahoji na kuyachunguza maisha yao, kuchunguza imani zao za mambo mbalimbali. Ni muhimu kufahamu mtu anayetaka kugombea uongozi wa juu katika Taifa anaamini nini? Ana itikadi gani? Anafuata sera gani? Ni mzalendo au ni kibaraka? Yote haya ni muhimu kufahamika mapema.

Ushawishi wa wananchi
Wagombea wa CCM, hawatoki mwezini. Ni watu wanaoishi kwenye jamii yetu. Tunawafahamu. Hivyo CCM, haiwezi kukwepa ushawishi wa wananchi. Hakuna ushahidi wa kutosha unaoonyesha kwamba Halmashauri Kuu inawafahamu vizuri wagombea kuwazidi Watanzania wengine.
Kama CCM inamtafuta mtu wa kuliongoza Taifa, haiwezi kukwepa mapenzi ya watu wote wanachama wa CCM na wale wasiokuwa wanachama. Kama mtu ni fisadi; anajulikana kwa kula rushwa, anajulikana kwa kufuja hovyo pesa za Serikali, anajulikana kwa kiburi chake na majigambo, anajulikana kwa kutotumikia bali kutumikiwa. Anajulikana kwa kutolipenda Taifa lake na kulithamini.
Anajulikana kwa kukaribisha miradi hewa na kushiriki kuiuza nchi, anatibiwa nje ya nchi, kila kitu chake kinanunuliwa nje ya nchi na watoto wake wanasomea nje ya nchi, halmashauri kuu haiwezi kuibadilisha hali yake. Mtu akishazidi miaka 55 ni vigumu kumbalidisha. Samaki hukunjwa angali mbichi!
Kama nilivyosema hapo juu, hawa wagombea hawatoki mbinguni. Tunaishi nao. Kama ni mwanamke, tunawafahamu wanawake wote wa CCM ambao wana sifa, mvuto na uwezo wa kuliongoza Taifa.
Kama ni vijana, tunawafahamu na kusema ukweli vijana wengi wamejitokeza na kuonyesha hamu ya kutaka kuliongoza Taifa lao. Ni wazi vijana wengine hawana historia hata ya kuandika chochote juu ya maisha yao, juu ya Tanzania au mwelekeo wa Taifa letu, wanajitokeza kufurahisha watu na kuonyesha kwamba kila Mtanzania anaweza kuwa Rais.
Hawa wanacheza na wala hatuna ulazima wa kuwasikiliza au kuwatilia maanani. Kuna vijana wachache, ambao wana uwezo mkubwa na kusema ukweli mtu ambaye ana miaka zaidi ya 40 siyo haki kumchanganya na vijana au watoto, huyu ni mtu mzima, baba wa familia na mtu mwenye wajibu mkubwa kwa familia yake na taifa lake. Hata hivyo, kuna baadhi ya wazee, wale ambao hawataki kustaafu, wanaotamani kufa wamekikalia kiti cha urais wamejitokeza pia. Ni wazi wazee hawa wanaongozwa na tamaa ya madaraka.
Nchi yetu imeweka miaka ya kustaafu kwenye umri wa miaka 60, sasa wazee wanaotaka kugombea urais na wako juu ya miaka 60, wana matatizo ya aina fulani. Tukishindwa kuwashawishi kustaafu kwa amani, basi tuwatafutie dawa ya ugonjwa wao.

CCM inamtaka nani?
Tunabaki kujiuliza, CCM, wao wanamtaka nani, huyo ambaye havutii hisia za watu? Maana kama anavutia ni lazima ataonekana kwa kila mtu. Kama anavutia ni lazima atapata kura za maoni. Atatoka wapi kama siyo miongoni mwa wale wale tunaowajua na kuishi nao? Atatoka wapi kama si wale wanaopitapita huku na kule wakisambaza bahasha miongoni mwa wajumbe wa mkutano mkuu?
Dunia nzima inajua jinsi Tanzania, tunavyoishi kishirikina. Mauaji ya watu wenye ualbino yamelipaka Taifa letu matope. Watu wanaamini tunaishi kishirikina. Na mwenendo wa CCM wa kuwanyamazisha wanachama wanaotaka kugombea umekaa kishirikina. Kwani kuna ubaya gani mtu kujitangaza kutaka kugombea urais?
Akitumia njia mbovu, ikifika kura za maoni, anatupwa nje. Lakini kufanya mambo kwa mfumo wa kishirikina ni kuongeza shaka katika mwenendo wa Taifa. Si lengo la makala haya kumpigia debe yeyote yule anayetaka kugombea kupitia CCM. Ingawa kumpigia mtu debe si dhambi, maana hii ni nchi yetu sote. Mimi kama Mtanzania na mzalendo wa kweli, nina lengo la kuwakumbusha vigogo wa CCM kwamba sauti ya watu ni sauti ya Mungu. Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, alisema kwamba Rais wa Tanzania, atachaguliwa na Mungu. Na Mheshmiwa Magufuli, akarudia kauli hiyo mara kwa mara. Ni Mungu gani anayeongelewa asiyepitia kwa watu wake? Kwa upande wa CCM, Mungu amesema kupitia kwa watu kwamba mtu mwenye sifa zisizotiliwa shaka ndiye atasimama upande wa CCM . Hiyo ndiyo sauti ya Mungu. Si maoni yangu, bali ni maoni ya watu tunaowauliza maoni yao juu ya uchaguzi ndani ya Chama cha CCM. CCM inaweza kuamua kuziba masikio lakini ukweli utabaki palepale.
Hivyo ni muhimu tukamfahamu mgombea wa CCM mapema. Tumpime na kumhoji na yeye ajieleze na kujipima na wagombea wa vyama vingine. Hivi ndivyo nchi zilizoendelea zinafanya.
Hivyo ndivyo nchi zote zinazofuata demokrasia zinafanya. Wagombea wanafahamika kwa watu zaidi ya mwaka mzima. Huu mfumo wa kuviziana kama wachawi, inaelekea ni Watanzania tu!
Ni lazima kubadilika ili tuweze kuishi kwenye dunia hii ya Utandawazi ambayo tuna imani kwamba, sasa imekuwa ni kijiji kimoja. Hivyo ni wito wetu kwa CCM, kuwaachia wagombea kujitangaza, tuwajue na kuwatathmini kama tunavyofanya kwa wagombea wa vyama vingine.

CHANZO: MWANANCHI

No comments: