Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Ummy Mwalimu.
Wakati Tanzania ikitajwa kuwa kichochoro cha 
kupitishia dawa za kulevya, wabunge wamehoji dawa hizo zinazokamatwa 
kama ushahidi zimekuwa zikipelekwa wapi kwa kuwa haionyeshi kama 
zimekuwa zikichomwa moto au la hali inayotia shaka udhibiti wa biashara 
hiyo.
Mbunge wa Viti Maalum, Rukia Ahmed, akiuliza swali la nyongeza jana 
bungeni, alisema kumekuwa na ucheleweshaji wa kesi za dawa za kulevya 
licha ya mtuhumiwa kukutwa na dawa hizo tumboni na pia zilizokamatwa 
haionyeshi zinapelekwa wapi.
Alisema kesi nyingi za mauaji na dawa za kulevya zinachukua muda 
mrefu kumalizika mahakamani na kusababisha watuhumiwa kukaa zaidi ya 
miaka saba rumande na kuhoji kwa nini muda wanaokaa rumande usijumuishwe
 kama sehemu ya hukumu wanapotiwa hatiani. Mbunge wa Karagwe (CCM), Gosbert Blandess, alihoji lini serikali 
itaanzisha mahakama maalum kwa ajili ya kushughulikia kesi za dawa za 
kulevya na rushwa kama njia ya kudhibiti tatizo hilo.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Ummy Mwalimu , alisema 
mahakama inaendeshwa kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za nchi, 
hivyo suala la hukumu pamoja na kipindi cha mshtakiwa kutumikia kifungo 
chake hufanyika kulingana na sheria inavyotamka kuhusu adhabu ya kosa 
husika.
Kuhusu zinapopelekwa dawa za kulevya zinazokamatwa, alisema 
kiutaratibu vidhibiti havirudishwi na hukumu ikishatolewa vinateketezwa.
     CHANZO:
     NIPASHE
    

No comments:
Post a Comment