Social Icons

Pages

Friday, March 13, 2015

BENKI YA DUNIA KUIPANGILIA D'SALAAM

Jiji la Dar es Salaam  
Benki ya Dunia imetoa mikopo mitatu ya Sh710 bilioni (Dola 396 milioni za Marekani) kwa Serikali ili kusaidia kukuza miundombinu katika Jiji la Dar es Salaam na vitongoji vyake, kusaidia masuala ya uvuvi na ujenzi wa nyumba za gharama nafuu.
Akizungumza wakati wa kusaini mkataba wa makubaliano, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk Servacius Likwelile alitoa wito kwa taasisi zinazohusika kuhakikisha zinasimamia miradi hiyo kwa ukamilifu, kusiwe na upotevu wa fedha ili kupata manufaa.
Dk Likwelile alisema katika mgawanyo wa fedha hizo Dola 300 milioni sawa na Sh537.9 bilioni zinaelekezwa katika jiji la Dar es Salaam kuhakikisha miundombinu yake inakuwa ya kiwango bora pamoja na utawala. “Mkopo wa pili wa Dola 60 milioni za Marekani (Sh107 bilioni) utatumika katika ujenzi wa nyumba za gharama nafuu,” alisema Dk Likwelile.
Alisema mkopo huo ni ukombozi kwa watu jijini hapa kutokana na wengi wao kushindwa kujenga nyumba zao, hivyo fursa hiyo itawasaidia kupata vifaa vya gharama nafuu na kuweza kujenga. “Mkopo wa tatu ni wa Dola 36 milioni za Marekani, sasa huu ni wa mradi wa uvuvi wa kikanda ambao unashirikisha Tanzania, Comoro na Msumbiji, sisi tutapata Dola 36 milioni (Sh64.5 bilioni) na lengo lake ni kuendeleza uvuvi katika nchi hizi,” alisema Dk Likwelile.
Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia wa Uganda, Tanzania na Burundi, Philippe Dongier, alisema wameamua kutoa msaada huo ili kuliimarisha jiji la Dar es Salaam kwani ni kati ya majiji yanayokua kwa kasi duniani, tofauti na miundo mbinu iliyopo. “Zaidi ya watafutaji kazi 800,000 wanaingia katika jiji hili kila mwaka, katika uchunguzi wetu tumebaini pia makazi ni duni na miundombinu haikidhi.”
vigezo. Lakini pia tumetoa mkopo huu ili kusaidia jiji kukua na kupata maendeleo kwa haraka,” alisema Dongier. Hii ni mara ya kwanza kwa Benki ya Dunia kutoa mikopo serikalini, kabla ya kusimamishwa kwa misaada hiyo na nchi wahisani mwishoni mwa mwaka jana kufuatia sakata la Tegeta Escrow.

CHANZO: MWANANCHI

No comments: