Naibu Waziri wa Fedha, Adam Malima.
Wabunge wameilaumu serikali wakisema ndio inayofuga
mgogoro kati ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na wafanyabiashara
kuhusu matumizi ya mashine za kodi zinazotumia mfumo wa kisasa wa
kielektroniki (EFD).
Lawama hizo zilitolewa kutokana na kushindwa kuitisha kikao cha
kamati ya majadiliano ya kushughulikia kero zote za kodi wanazotozwa
wafanyabiashara kupitia EDF kwa zaidi ya miezi sita tangu iundwe na
Waziri wa Fedha Saada Salum Mkuya.
Pia wamelalamika namna mapato ya serikali yanavyopotea kwa kuhoji
kampuni ya Home Shopping Center (HSP) inakopata nguvu za kulazimisha
wafanyabiashara kutumia wakala zake pekee kuingiza kontena, ambazo
hutozwa kodi ndogo tofauti na thamani halisi ya mzigo na bila kupewa
stakabadhi.
Walitoa malalamiko hayo katika kikao kati ya Kamati ya Bunge ya
Uchumi, Viwanda na Biashara, uongozi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara
Tanzania, watendaji wa TRA na wa wizara hiyo, walioongozwa na Naibu
Waziri wa Fedha, Adam Malima (uchumi na fedha).
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Luhaga Mpina, alimweleza Kamishna Mkuu
wa TRA, Rished Bade, kwamba hakuna mtu mwingine anayepaswa kulalamikiwa
kuhusu kuendelea kwa mgogoro huo kutokana na kuchelewesha kuitishwa kwa
kikao cha kamati hiyo tangu iundwe Oktoba, mwaka jana, isipokuwa TRA.
Akijibu hoja hiyo, Bade alikiri kasoro hiyo na Malima akaahidi kuwa kikao hicho sasa kitafanyika ndani ya siku 14 kuanzia sasa. Kamishna wa Mapato wa Wizara hiyo, Shogholo Msangi, alisema
Februari 18, mwaka huu, walikutana na wasambazaji wa mashine hizo, ambao
walitumia fursa hiyo kueleza matatizo yaliyopo, ikiwamo ubovu wa
mitandao na karatasi zinazotumika.
Mbali na Mpina, ambaye ni Mbunge wa Kisesa, wabunge wengine
walioilalamikia serikali kuhusiana na kuendelea kwa mgogoro huo na mfumo
mbovu wa ukusanyaji wa kodi, ni Khatib Haji (Konde), Josephine
Genzabuke (Viti Maalumu) na Juma Ngwali (Ziwani).
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment