Jaji Mkuu Othman Chande.
Wafungwa 14 waliohukumiwa adhabu ya kifo katika
gereza la Isanga, mkoani Dodoma, wamelalamikia ucheleweshwaji wa nakala
za hukumu za kesi zao kwa zaidi ya miaka mitano, hali inayowakwamisha
kukata rufaa.Kwa mujibu wa taarifa ya wafungwa hao ambayo NIPASHE imeiona, ofisi
ya Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Mashariki imekuwa na ukiritimba
katika utoaji wa nakala za hukumu za kesi na hivyo kushindwa kukata
rufaa wakati ni haki yao ya msingi.
Wafungwa hao (majina tunayahifadhi), walisema Kanda ya Mashariki
imekuwa na tatizo katika kushughulikia suala hilo ukilinganisha na
Mahakama Kuu za kanda nyingine ambazo wafungwa wamekuwa wakipewa nakala
za hukumu za kesi kwa ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.
“Sisi wafungwa wa adhabu ya kifo wa gereza la Isanga Dodoma
tunailalamikia kanda ya Mashariki hususan Msajili wa Mahakama Kuu Kanda
ya Mashariki kwa kutucheweleshea milolongo na nakala za hukumu za kesi
zetu kwa zaidi ya miaka mitano tofauti na kanda zingine zote ambazo
hutoa nakala hizo ndani ya mwaka mmoja tu,” wameeleza katika taarifa
yao.
Waliongeza kuwaa ucheleweshaji huo wa nakala za hukumu hupelekea
kuchelewa kusikiliza rufani zao kwa zaidi ya miaka kumi tofauti na kanda
zingine rufaa husikilizwa ndani ya miaka miwili tu. “Baya zaidi maswahibu haya hutukumba sisi tusio na pesa, mnyonge
mnyongeni, haki yake mpeni, haki inayocheleweshwa ni haki inayonyimwa,
tunamuomba Mwanasheria Mkuu, Jaji Mkuu na Waziri wa Katiba na Sheria
watutatulie kero hiyo kwani siyo wote tulio gerezani tuna makosa,”
wameeleza.
Wafungwa wanaolalamikia suala hilo ni wale ambao walihukumiwa
adhabu ya kifo kati mwaka 1992 ambao idadi yao ni mmoja, 2003 (mmoja),
2004 (mmoja), 2007 (mmoja), 2009 (wawili), 2010 (watatu), 2011 (watatu)
na mwaka 2012 wapo wawili.
Msemaji wa Jeshi la Magereza, Deodatus Kazinja, alipoulizwa alisema
suala la ucheleweshaji wa nakala za hukumu za kesi kwa wafungwa siyo
jambo geni kwani limekuwa ni tatizo ambalo linazua malalamiko sana ya
wafungwa hapa nchini. “Suala hili ni tatizo la nchi nzima lakini sisi Jeshi la Magereza
halituhusu japo tunakuwa na hao wafungwa, wahusika ni mahakama na
mamlaka nyingine,” alisema.
Naye Mkuu wa Kituo cha Mawasiliano cha Mahakama, Nurdin Ndimbe,
alipoulizwa alisema yupo likizo, hivyo hawezi akazungumzia lolote kuhusu
suala hilo.
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment