Maadhimisho hayo yalifanyika chini ya kauli mbiu ya ‘Miaka 53 ya Uhuru ingia katika historia ya nchi yetu jitokeze kupigia kura Katiba inayopendekezwa.’
Waimbaji hao ambao waliutuliza uwanja uliofurika viongozi mbalimbali, waliimba kwa hisia huku baadhi ya maneno katika wimbo wao yakiwa na ujumbe kwa viongozi wa kisiasa na waandishi wa habari kulinda na kutunza amani ya nchi.
Waimbaji hao walisema ni vyema keki ya Taifa ikatolewa macho na kila Mtanzania, hivyo ni vyema ikagawanywa kwa usawa.
Rais Jakaya Kikwete aliingia uwanjani saa 4:07 asubuhi na kuanza kuzunguka uwanja akiwa kwenye gari ya wazi na baadaye kupigiwa wimbo wa Taifa, akapigiwa mizinga 21 na kukagua gwaride hadi saa 4:23. Baadaye gwaride lilianza kutoa heshima kwa kupita mbele ya jukwaa kuu kwa mwendo wa pole na kasi. Baada ya gwaride linaloundwa na askari wa vikosi vya ulinzi na usalama vya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Jeshi la Wananchi (JWZ), Jeshi la Magereza na Jeshi la Polisi, na wanafunzi kutoka shule mbalimbali za msingi Dar es Salaam na Zanzibar, walionyesha halaiki.
Halaiki hiyo iliambatana na ngoma ya asili ya mkoa wa Pwani ya mdundiko na ngoma ya bugobugo ya asili ya mkoa wa Mwanza, na baadaye walitengeneza ramani ya Tanzania, kuandika neno Miaka 53 ya Uhuru, neno Kiswahili, Mlima Kilimanjaro na kuonyesha bendere ya Taifa ikipepea kileleni, maua mbalimbali na kuimba nyimbo mbalimbali.
Katika halaiki hiyo mwanafunzi mmoja alizimia na kupatiwa huduma ya kwanza na watoa huduma waliokuwapo uwanjani.
Burudani nyingine ni ngoma ya asili kutoka maeneo mbalimbali nchini ikiwamo Kasulu, mkoani Kigoma, Zanzibar na Pemba.
Aidha, vikosi vya ulinzi na usalama viliburudisha kwa wimbo wa kuhamasisha amani, kufanya kazi kwa bidii kwa kuwa kazi ndiyo uhuru kwa sababu nchi tegemezi ni yenye Uhuru wa bendera na wananchi kujitokeza kupiga kura Katiba.
Viongozi wastaafu ambao hawakuhudhuria ni Rais wa awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa; Rais Mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume na Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal.
Waliohudhuria ni Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein; Waziri Mkuu, Mizengo Pinda; Rais Mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi; Makamu wa Kwanza wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad; Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi; Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Anne Makinda; Naibu Spika, Job Ndugai; Jaji Kiongozi, Shaban Lira na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema.
CHANZO:
NIPASHE


No comments:
Post a Comment