
Kaimu Balozi wa China Li Xuhang
Miji hiyo inaungana kuifanya Butiama na Mara kuwa kivutio cha utalii, uwekezaji kibiashara na kitaaluma kwa kushirikiana Xiang Tan jiji lenye maendeleo makubwa.
Muungano huo wa miji huo ulifanyika wiki iliyopita mjini Musoma, wakati Kaimu Balozi wa China Li Xuhang na Meya wa Musoma Kisusura Malima, waliposaini mkataba wa makubaliano ya ushirikiano.
Balozi Xuhang alisema ushirikiano huo mpya unaenzi kazi za viongozi wakuu wa China na Tanzania Mwalimu Nyerere na Mao Zedong ambao walianzisha urafiki baina ya mataifa yao uliodumu hadi sasa.
Akiwa mkoani Mara kuadhimisha miaka 50 ya Urafiki wa Tanzania na China, Balozi Xuhang alisema kuunganisha miji hiyo kutakwenda pamoja na kukarabati, makumbusho ya Mwalimu Nyerere yaliyoko Mwitongo na kuyaunganisha na Makumbusho ya Mao.
Balozi huyo wa China aliahidi kuifanya Musoma kuwa kitovu cha kipekee cha utalii na eneo lenye heshima maalum ambao ni mkakati wa kudumisha ushirikiano huo ambao mwaka huu ulisherehekea Jubilee ya Miaka 50 tangu kuundwa kwake.
Alisema China itaboresha makumbusho hiyo kwa kuipanua zaidi kama itakavyowezekana na kujenga nyumba ya Mwalimu aliyoishi kabla ya kujiunga na siasa ili iwe sehemu za kumbukumbu na historia ya maisha yake.
Balozi huyo alitembeleaShule ya Msingi Mwisenge aliposoma Mwalimu Nyerere na kutoa Sh. milioni 20 kwa ajili ya ujenzi wa maabara ya kisasa, itakayojengwa na kampuni ya Chicco ya China.
Balozi huyo alitangaza ufadhili wa masomo kupitia ‘Skolaship’ ya Balozi wa China iliyowazawadia wanafunzi 10 bora zaidi ya 200.
Wanafunzi 10 bora wa darasa la kwanza hadi la sita walipata Sh 100,000 kwa mshindi wa kwanza, wa pili hadi wanne Sh. 80, 000 na waliobakia Sh 60,000. Pia aliwazawadia watoto wenye ulemavu wa kuona na albino Sh. 50,000.
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment