Social Icons

Pages

Wednesday, December 10, 2014

MWIGULU AONJA MOTO WA ESCROW

Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wakiwa na bango linalosomeka 'Hakuna uchunguzi juu ya uchunguzi Escrow' wakati wakimpokea Naibu Katibu Mkuu wa CCM ambaye pia ni Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, kwenye uzinduzi wa kampeni za uchaguzi wa serikali za mitaa mkoa wa Geita kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Nyankumbu. Picha/Renatus Masuguliko.
Sakata la wizi wa zaidi ya Sh. bilioni 300 kutoka akaunti ya Tegeta Escrow katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) limeanza kukitesa Chama Cha Mapinduzi (CCM), baada ya Naibu Katibu Mkuu wake Tanzania bara, Mwigulu Nchemba kuonja joto ya jiwe katika mkutano wa Chama hicho.
Nchemba  ambaye pia ni Naibu Waziri wa Fedha, alijikuta katika wakati mgumu katika viwanja vya Nyankumbu, wilayani Geita, baada ya kupokewa kwa mabango ya wafuasi wa chama chake walioonyesha kutofurahishwa na hatua ya serikali kutowachukulia hatua viongozi waliotajwa kuhusika katika kashfa hiyo ambayo imeitikisa nchi nzima na kuzua mjadala mkubwa.
Wanachama hao waliohudhuria uzinduzi wa kampeni  za uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Jumapili wiki hii walimnyanyulia Nchemba mabango yaliyokuwa yameandikwa kuwa ‘Escrow hakuna uchunguzi juu ya uchunguzi’.
Baada ya wanachama wa CCM kuonyesha hisia zao za kutofurahishwa na kasi ndogo ya kuwawajibisha viongozi wa serikali waliohusika, Nchemba aliwajibu kwa kusema kuwa licha ya kuwapo na matatizo mengi nchini yakiwamo ya wizi katika  akaunti ya Tegeta Escrow, lakini wananchi wanatakiwa kuendelea kuiamini CCM.
Alisema licha ya mambo mengi kutokea  na kuwahusisha baadhi ya viongozi wa CCM, lakini chama hicho kimefanikisha kuwapo na maendeleo ya mbalimbali kuanzia ya barabara, madaraja na miundombinu mingine.
Sakata hilo lilibuka bungeni na kuzua mjadala mkubwa nchini baada ya ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuwasilishwa bungeni baada ya kupitiwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).
PAC ilipowasilisha ripoti hiyo bungeni ilibainisha kwamba fedha hizo zilikuwa za umma tofauti na kauli zilizokuwa zikitolewa na viongozi wa serikali awakiwamo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda; Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo; Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Eliakim Maswi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema.
Pia PAC ambayo ilikutana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kabla ya ripoti hiyo kuwasilishwa bungeni, ilieleza jinsi fedha hizo zilivyoibwa na zilivyochukuliwa benki na watu kadhaa walionufaika na mgawo huo.

MAAZIMIO YA BUNGE
Novemba 29, mwaka huu, Bunge lilifikia maamuzi hayo baada ya PAC kuwasilisha ripoti yake Bungeni chini ya uenyekiti wa Zitto Kabwe, ikitaka kufukuzwa kazi kwa baadhi ya vigogo, kufilisiwa na kufikishwa mahakamani.
Waliopendekezwa kufutwa kazi ni Prof Muhongo, Maswi, Werema na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka, ambaye taarifa ya PAC ilieleza kuwa alinufaika kwa mgawo wa Sh. bilioni 1.6 kutoka kwa James Rugemalira, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya VIP Engneering&Marketing LTD.
Wengine waliopendekezwa  kuvuliwa yadhifa zao ni wenyeviti wa kamati za kudumu za Bunge hilo,  William Ngeleja (Sheria, Katiba na Utawala), Andrew Chenge (Bajeti) na Victor Mwambalaswa  (Nishati na Madini).
Pia Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) ivunjwe.Azimio hilo linawataka viongozi wa umma na maofisa wa ngazi za juu serikalini kuwajibika kwa sababu wamehusishwa na vitendo vya kijinai katika sakata hilo linalohusisha kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania (IPTL).
Bunge pia lilitaka Takukuru, Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi dhidi ya wote waliotajwa kuhusika na sakata hilo na  wale watakaobainika kuhusika  kwenye vitendo hivyo vya jinai wawajiubishwe.
Kwa mujibu wa taarifa ya CAG, Chenge na Ngeleja wametajwa kunufaika na fedha za mwanahisa Rugemalira kwa Chenge kupewa Sh. bilioni 1.6 na Ngeleja Sh. milioni 40.2.Maazimio mengine  ni kumtaka Rais kuunda Tume ya Uchunguzi ya Kijaji kuchunguza tuhuma za utovu wa maadili dhidi ya majaji kuhusishwa  kwenye kashfa hiyo.
Majaji waliotajwa na Bunge kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi ni Jaji Aloysius Mujulizi na Jaji Prof. Eudes Ruhangisa wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Bunge pia lilitaka mamlaka husika za kifedha na za kiuchunguzi kuitaja Stanbic Bank Tanzania Ltd na benki nyingine yoyote itakayogundulika baada ya uchunguzi wa mamlaka za kiuchunguzi kujihusisha na utakatishaji wa fedha zilizotolewa katika akaunti ya Escrow kuwa ni taasisi zenye shaka ya utakatishaji wa fedha haramu.
Hata hivyo, juzi  Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, alisema Rais Jakaya Kikwete atafanya maamuzi baada ya uchunguzi zaidi wa kina juu ya suala hilo kukamilika.
Balozi Sefue alisema kwamba, Rais hawezi kufanya uamuzi bila uchunguzi wa kina wa vyombo vinavyohusika kukamilisha uchunguzi.
Alitoa kauli hiyo baada ya waandishi wa habari waliotaka kujua hatua zilizochukuliwa na Rais Kikwete baada ya Bunge kutoa maazimio manane yakiwamo ya kutenguliwa kwa nyadhifa za vigogo hao.
Alisema ni lazima haki itendeke na kwamba maamuzi ya Bunge yanaheshimika na kwamba ripoti zote za CAG na PAC zilikuwa nzuri, lakini vyombo vya uchunguzi vinapaswa kwenda kwa undani zaidi kwa ajili ya kuchunguza.
Balozi Sefue alisema baada ya uchunguzi huo, Rais atakuwa kwenye nafasi nzuri ya kufanya maamuzi na kwamba hakuna mahali maamuzi ya kamati yamemtaka kuchukua hatua moja kwa moja, bali vyombo husika kuchunguza zaidi.
Tangu kutolewa kwa kauli hiyo, makundi kadhaa katika jamii hususani wanasiasa wamekuwa wakihoji kuwa kwa kuwa Takukuru, TRA, CAG walishachunguza ni vyombo vipi vitatumika kuchunguza tena.

MBATIA ATEMA MOTO
Wakati huo huo,  Mbunge wa  Kuteuliwa, James Mbatia, amaesema atakuwa wa kwanza  kuwahamisisha wananchi wasilipe kodi kama watuhumiwa waliotajwa kwenye sakata la Escrow hawatakamatwa na kufilisiwa.
Akihutubia katika mkutano wa hadhara wa kampeni za uchaguzi wa serikali mitaa katika eneo la Njia Panda, Vunjo, mkoani Kilimanjaro, alisema  maazimio ya Bunge yanapaswa kufanyiwa kazi na siyo watu wachache kuwatetea watuhumiwa wa sakata hilo.
Mbatia alisema yeye hakuteuliwa na Rais Jakaya Kikwete ili akakae bungeni na kufumbia macho  masuala yenye utata na yanayolifedhehesha taifa kwa sababu tu ameteuliwa na Rais na badala yake  ataongeza kasi ya  kuisimamia serikali kama sehemu ya Wabunge.
“Niliwahi kuzungumza bungeni wakati wa sakata la Escrow kwamba itafika mahali Watanzania watachoka masuala ya ufisadi, watasusia  ama kufanya migomo baridi ya kutolipa kodi na kwa maana hiyo, mimi ntakuwa wa kwanza kuungana na wananchi. Niko tayari kuwatetea  wananchi,” alisema Mbatia.  
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: