WAZIRI wa Maliasili na Utalii na Mbunge wa Jimbo la SingidaK askazini (CCM), Lazaro Samwel Nyalandu, ambaye ametangaza rasmi kugombea
nafasi ya urais katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwakani.
Mambo yamezidi kunoga katika
kinyang’anyiro cha urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) baada ya
Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu kutangaza nia ya kuwania
nafasi hiyo katika Uchaguzi Mkuu mwakani. Nyalandu ambaye ni Mbunge wa Singida Kaskazini
alitangaza nia hiyo jana kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika
Kijiji cha Ilongero, ndani ya jimbo lake la uchaguzi.
Akihitimisha fununu zilizokuwa zikimtaja miongoni
mwa wanaCCM wanaotaka kukalia kiti hicho kinachoachwa na Rais Jakaya
Kikwete, Nyalandu alisema baada ya kutafakari kwa muda mrefu na
kujikagua kwa kina, ameona anao uwezo wa kutosha wa kupokea kijiti
kutoka kwa Rais anayemaliza muda wake mwakani kwa mujibu wa Katiba.
“Kujikagua huko ni pamoja na kutafakari jinsi
nilivyoweza kutekeleza ilani ya uchaguzi ya CCM katika vipindi vitatu
(miaka 15) nikiwa mbunge wa Singida Kaskazini. Katika kipindi hicho cha
ubunge, nimetumia zaidi ya Sh2 bilioni kuchangia miradi ya maendeleo
katika sekta mbalimbali zikiwamo za afya, maji na barabara,” alisema
Nyalandu.
Alisema wakati ukifika, Watanzania kutoka sehemu
mbalimbali za nchi wakiongozwa na wakazi wengi wa Jimbo la Singida
Kaskazini watamsindikiza kwenda Dodoma kuchukua fomu za kuwania urais.
Katika mkutano huo uliohudhuriwa na mamia ya
wananchi wa jimbo hilo ambao ulipambwa na vikundi mbalimbali vya
burudani wakiwamo waimbaji mahiri wa nyimbo za injili nchini, Rose
Muhando na Christina Shusho, Waziri huyo alitoa changamoto kwa wanasiasa
wanaojitokeza kila kukicha kuwania urais kuonyesha walichowafanyia
Watanzania. “Watanzania waliokwishaonyesha nia ya kuwania
urais mwakani, nawaomba sote tuonyeshe kazi tulizozifanya katika
kuwahudumia wananchi ili waweze kutupima vizuri na kujijengea mazingira
mazuri ya kuchagua rais atakayewafaa kwa kuwaletea maendeleo,” alisema.
Alikishukuru Chama Cha Mapinduzi kwa maandalizi
yake mazuri ya kuhakikisha kinapata mwanachama safi, mwadilifu na
mchapakazi atakayepeperusha bendera yake katika kinyang’anyiro hicho
mwakani.
Wa nne kutangaza nia
Nyalandu anakuwa mwanaCCM wa nne kutangaza rasmi
nia ya kuwania urais baada ya Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia, January Makamba na Mbunge wa Nzega, Dk Hamis Kigwangalla na
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliyesema ametangaza nia kimyakimya.
Mbali na hao waliotangaza nia, wapo wanasiasa
ambao wamekuwa wakitajwa kuwa miongoni mwa wanaotaka nafasi hiyo ambao
ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, Naibu Waziri
wa Fedha, Mwigulu Nchemba na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi
Maalumu), Profesa Mark Mwandosya.
Wapo pia Mbunge wa Songea Mjini, Dk Emmanuel
Nchimbi, Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano, Dk Mohamed Gharib Bilal na Waziri wa Sheria na
Katiba, Dk Asha - Rose Migiro.
Ukawa
Wazazi wazungumza
Vilevile, lipo kundi la ambao hawajatangaza nia lakini walipewa
onyo na CCM kwa kuanza kampeni mapema wakiwamo mawaziri wakuu wa zamani,
Edward Lowassa na Frederick Sumaye, Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais
(Uhusiano na Uratibu), Stephen Wasira na aliyewahi kuwa Waziri wa
Nishati na Madini, William Ngeleja. Makamba pia alipewa onyo.
Ukawa
Kwa upande wa upinzani, mpango unaofahamika ni
Ukawa wa kusimamisha mgombea mmoja na wanaotajwa kuwa na uwezekano wa
kuwania nafasi hiyo ni Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa,
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi,
James Mbatia na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.
Wazazi wazungumza
Baada ya Nyalandu kutangaza nia hiyo, baba yake
mzazi, Samwel Nyalandu alisema amepokea kwa mikono miwili kusudio la
mtoto wake kuwania nafasi nyeti ya urais kwa kuwa anao uwezo wa kumudu
nafasi hiyo.
Alimtaka endapo atafanikiwa kupata nafasi hiyo na
kuwa mkazi wa kwanza wa Singida kuwa rais, ahakikishe anafuata nyayo za
watangulizi wake.
“Pia namwomba akifanikiwa aje kuwa karibu zaidi na
wananchi. Sikio lake liwe jepesi kusikiliza kero mbalimbali
zinazowakabili wananchi atakaokuwa akiwaongoza au kuwatumikia.
Mzee Nyalandu alisema mwanaye Lazaro alianza
kuonyesha dalili kuwa mbele ya safari ya maisha yake atakuwa kiongozi wa
watu kwani alipokuwa mdogo, alikuwa anapenda kukusanya wenzake na
kuanza kuwaongoza katika mambo mengi ikiwamo michezo.
Alisema pia alipokuwa anasoma Shule ya Msingi
Pohama, alikuwa akiongoza kuanzia darasa la kwanza hadi alipomaliza
darasa la saba na kuwa mwanafunzi pekee kufaulu mtihani wa Taifa wa
kumaliza elimu ya msingi na kujiunga na shule ya sekondari ya Kibaha ya
wanafunzi wenye vipaji maalumu na baadaye Ilboru kidato cha tano na
sita. Akimzungumzia waziri huyo, mkulima na mkazi wa
Kijiji cha Ilongero, Eliwanja Hango alisema Nyalandu ameonyesha uwezo
mkubwa katika kuwatumikia wakazi wa jimbo lake na wakati wote yupo
karibu nao. Alisema kutokana na uzoefu alioupata katika
kuwatumikia wakazi wa jimbo hilo na uzoefu wake wa kuzunguka dunia
nzima, kazi ya urais haitampa shida ataimudu.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment