Waziri wa Mambo ya Nje wa Libya amesema makundi ya itikadi kali za
kiislamu yameanza harakati mpya za kuviteka tena vyanzo vya mafuta,
baada ya shambulio katika matangi ya kuhifadhia mafuta mashariki mwa
taifa hilo.
Shambulio hilo katika eneo la kaskazini lilisababisha moshi mkubwa
mweusi kutanda katika anga ya eneo hilo. Akizungumza kutoka mjini Cairo,
Misri Waziri wa Mambo ya Nje Mohamed Dairi, alisema shambulio hilo
limefanywa na kundi la wanamgambo wa kiislamu lenye makao yake makuu
katika mji wa magharibi wa Misrata na ambalo ni tiifu kwa serikali
hasimu ya Tripoli.
Alisema makundi ya Kiislamu yamejiunga katika shambulio hilo, ambalo
limelazimisha kufungwa kwa bandari kubwa ya kusafrishia mafuta. Afisa
mmoja kutoka shirika la mafuta nchini humo Mohammed al-Hariri alisema
Jumamosi iliyopita kuwa mapipa 850,000 ya mafuta yaliangamia kutokana na
kuripuka kwa matangi matano ya kuhifadhia.
Mapigano yalizukaa katika maeneo ya karibu na eneo kubwa la
kuhifadhia mafuta la Sidra, ambalo kwa hivi sasa lipo katika udhibiti wa
kundi la wanamgambo lenye kupinga itikadi kali, lenye ushirika na
serikali yenye kutambulika kimataifa ambayo ina makaazi yake katika mji
wa mashariki wa Tabruk. Mapema mwezi huu serikali ya Tripoli ilijiapiza
kulikomboa eneo la Sidra.
Kwa mara ya kwanza makombola ya angani yaliripotiwa mjini Misrata, kwa
kile kilichoonekana kama majibu yaliyosababishwa na shambulio katika
vituo vya mafuta. Ahmed al-Musmari, msemaji wa jeshi linaloongozwa na
Tobruk, aliuambia mtandao wa habari wa al-Wasat kwamba shambulizi hilo
lilikuwa likilenga ngome zilizokuwa zikilenga kushambuliwa wanajeshi
wake.
Maafisa usalama mjini Misrata walisema mashambulizi ya anga
yalifanyika karibu na uwanja wa ndege, ambapo kombora moja lilishambulia
mita 300 kutoka katika mnara wa kuongozea ndege lakini halikufika
katika eneo la lami. Afisa ambae alizungumza kwa msaharti ya kutotaja
jina lake kwa kuwa hakuidhinishwa kuzungumza na waandishi, alisema
shambulizi hilo limesababisha kusimamishwa kwa safari za ndege za
shirika la ndege la Uturuki lakini hata hivyo hakuna maafa yoyote
yalioripotiwa.
Dairi, waziri wa mambo ya nje wa serikali ya Tobruk alisema makundi ya
wenye itikadi kali za kiislamu, baadhi yakiwa na makubaliano ya muungano
na kundi kubwa linalojiitwa Dola la Kiislamu, yameongeza wigo wao
nchini Libya, ukiwemo mji mkuu wa taifa hilo.
"Kwa bahati mbaya, tumekuwa na wasiwasi hapa Libya kutokana na
ongezeko la wapiganaji wa Dola la Kiislamu kutokana na ongezeko la
makundi ya wenye itikadi kali kama unavyojua kundi la Ansar Al Sharia
limejiunga kufanya mashambulizi tata dhidi ya maeneo yenye hifadhi ya
mafuta".Alisema waziri Dairi
Mazungumzo yanayodhaminiwa na Umoja wa Mataifa kati ya serikali hasimu
nchini humo yamepangwa kufanyika Januari 5. Na mpango maalum wa kuiunga
mkono Libya wa Umoja wa Mataifa umelaani vikali mashambulizi ya anga ya
Misrata.
CHANZO: DW KISWAHILI

No comments:
Post a Comment