Social Icons

Pages

Monday, December 29, 2014

TUNATARAJIA USHINDANI ZAIDI MZUNGUKO WA PILI LIGI BARA

Katuni
Mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara ulianza mwishoni mwa wiki hii na tayari klabu takriban zote zimeshacheza mechi zao raundi ya nane.

Klabu kama za Simba na Kagera Sugar zilifungua mzunguko huu juzi wakati nyingine kama Yanga na Azam zikicheza jana ikiwa ni muendelezo wa ufunguzi huo kuelekea kilele cha kutafuta bingwa na mwishowe klabu mbili zitakazoliwakilisha taifa katika michuano ya kimataifa mwakani. Sisi, kama ilivyo kwa wapenzi na wafuatiliaji wa soka nchini, tunazitakia kheri klabu zote, tukiamini kwamba zitaendelea kuonyesha mchezo mzuri, wenye ushindani mkali na mwishowe kupata mabingwa sahihi wa watakaoliwakilisha vyema taifa.
Ni imani yetu kuwa kama ilivyo ada, kamwe hakutakuwa na kingine kitakachotawala kwenye vyombo vya habari zaidi ya kuwapo kwa ushindani zaidi na soka la kiungwana katika kila mechi. Kwamba, badala ya kuwapo na taarifa zilizozoeleka katika siku za nyuma na hivi karibuni kuhusiana na ligi hiyo, sasa tutakuwa tukisikia zaidi namna washambuliaji wanavyofunga magoli ya kusisimua zaidi, mabeki wakionyesha ungangari katika kuzilinda timu zaidi na pia makipa wakionyesha umahiri wa kudaka kwa namna ya kuwalinganisha na nyani.
Tunasisitiza hili kutokana na ukweli kwamba soka ni biashara, soka ni ajira, soka ni burudani. Ikitokea kwamba taarifa mbaya kama za kuwapo kwa tuhuma zisizokuwa na ushahidi zikaendelea kutawala ripoti za mechi za ligi kuu, ni wazi kwamba msingi wa mchezo wenyewe utatetereka. Ni kwa sababu mashabiki watajihisi kukosa kile wanachokitarajia kutoka kwenye mchezo huo na mwishowe athari zake zitakuwa mbaya na kutishia hatma ya mchezo huu unaopendwa na maelfu ya watu nchini na kwingineko duniani.
Kwa mfano, katika mzunguko wa kwanza, licha ya kuwapo na ushindani mkali uliozishuhudia timu kubwa kama za Simba, Yanga na Azam zikibanwa kwa namna isiyotarajiwa na kukamata nafasi zisizokuwa za kileleni, tayari kulishaanza uvumi wa hapa na pale kuhusiana na uchezeshaji mbaya wa baadhi ya marefa. Makocha, mashabiki na wadau wote wa mchezo wa soka wanapaswa kuhakikisha kwamba tuhuma zozote hasi zinapaswa kufanyiwa kazi kwanza, tena kupitia njia zinazotambulika kwa mujibu sheria, kanuni na taratibu zilizopo na wala siyo kujisemea tu hovyo kwenye vyombo vya habari.
Tunalisema hili siyo kwa sababu tunataka marefa waendelee kuchezesha kadri watakavyo. La hasha. Bali, tunadhani kwamba ni muhimu wadau wenyewe wa mchezo huu wakahakikisha kwamba hawaharibu taswira nzuri ya mchezo wao kwa minajili tu ya kujitetea pindi timu zao zinapofanya vibaya. Kwamba, ni vyema wakajitahidi kadri wawezavyo kutoa maelezo ya kiufundi kuhusiana na sababu za kufanya vibaya pindi timu zao zinapopoteza mechi na wala si vinginevyo.
Pamoja na hilo, ni imani yetu kwamba wadau wa soka wataepuka tabia ya hovyo ya kuwatuhumu wachezaji wao kwa ubaya pindi timu zao zinapofanya vibaya. Wakumbuke kuwa daima mchezo wa soka hutegemea makosa ili mmoja apate goli. Beki akipigwa chenga ndipo goli hupatikana na hapo huwa ni furaha kwa wanaoshinda na kilio kwa wanaofungwa. Kadhalika, kipa anapokosea kudaka mpira kwa usahihi ndipo goli hupatikana.
Kinyume chake, katika hali ya kutokuwa na makosa, basi matokeo huwa ni 0-0 na mashabiki hukosa ladha ya magoli. Kwa kutambua hilo, kamwe isiwe nongwa kuona kuwa makosa fulani yawe ni kwa sababu ya mchezaji kununuliwa na wapinzani. Bali, ndivyo mchezo wenyewe ulivyo.
Hakika, yapo mengi ya kuwakumbusha wadau wa soka kuhusiana na mzunguko huu wa Ligi Kuu ya Bara. Hata hivyo, yatosha kuzingatia machache tuliyogusia kwa mustakabali mwema wa soka letu.
Shime, uungwana utawale katika mzunguko huu wa ligi kuu ya Bara. Klabu zionyeshe soka safi na lenye ushindani wa hali ya juu kama ilivyoonekana katika mechi za juzi na jana ambazo hata vigogo Simba na Yanga zilijikuta zikidondosha pointi licha ya usajili makini zilizodai kuufanya.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: