Social Icons

Pages

Thursday, December 04, 2014

MAABARA YA MKEMIA MKUU YAOMBA FEDHA ZAIDI

Waziri wa Afya Seif Rashid
Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali umeiomba serikali kuwaongeza bajeti ili kutekeleza mipango ya uchunguzi wa kimaabara kwenye nyanja za vyakula, uchafuzi wa mazingira, usalama mahali pa kazi na vielelezo vinavyohusiana na makosa ya jinai nchini.
Aidha, wameiomba serikali kuwasilisha fedha hizo  moja kwa moja kwa Ofisi ya Mkemia Mkuu kwani bila kufanya hivyo juhudi za serikali katika kutoa haki ndani ya vyombo vya sheria zitakwama.
Ombi hilo lilitolewa jana na Mkemia Mkuu wa Serikali, Profesa Samuel Manyele wakati wa uzinduzi wa jengo jipya la Maabara ya Sayansi jinai (Toksikolojia)  ambalo litatumika kwa ajili ya uchuunguzi wa kesi na vielelezo vya makosa ya jinai.
“Huduma ya uchunguzi wa vielelezo vya makosa ya jinai unakwama kwa sababu serikali haijapanga bajeti ya uchunguzi wa vielelzo vya makosa ya jinai pia ufinyu wa Jeshi la Polisi  kulipia gharama za uchunguzi hali inayokwamisha juhudi zetu za kuboresha huduma hii kulingana na hali ya uhalifu nchini,” alisema. 
Alisema wakala katika kutekeleza wajibu wake wamefanya ukarabati wa majengo, kuongeza vifaa na mitambo ya kufanyia kazi, kuongeza idadi ya watumishi na aina mbalimbali za ujuzi au utaalamu zaidi kulingana na teknolojia ya kisasa pamoja na kuanzisha ofisi na maabara za kanda ili kusogeza huduma karibu na jamii.
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii  Dk. Seif Rashid, alisema katika  ulimwengu wa sasa suala la uhalifu limeongezeka kwa kiwango cha juu huku likihusisha mbinu mbalimbali zikiwamo za kisasa, hivyo serikali inafanya jitihada mbalimbali ikiwamo matumizi ya vifaa vya teknolojia ili kukabiliana na hali hiyo.
Alisema kwa kutambua umuhimu wa wakala wa maabara ya makosa ya jinai serikali na jamii kwa ujumla itaendelea kufuatilia  na kushughulikia ombi lao la kununua mitambo mipya  na vifaa vya kisasa.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: