Chiraka Muhura
Tumekuwa tukisoma na hata kusikia mazungumzo ya
kawaida na kwenye vyombo vya habari juu ya ndoto za wajasiriamali
mbalimbali wakisema wanataka kuwa kama mfanyabiashara fulani maarufu
kutokana na biashara wanazozifanya.
Haya ni mambo ya kawaida katika maisha kwani
maisha ni mwigo, lakini mwigo wenye uhalisia wa kweli kulingana na
mazingira, wakati, uwezo na uthubutu wa mtu katika jambo analolifanya.
Katika kufanikisha yale ambayo unayafanya na hata
unayotaka kuyafanya kwa mafanikio, huna budi kufanya mambo kadha wa
kadha kama tabia zako za kila siku za utendaji wako wa kazi.
Jaribu kufikiria juu ya uwezo ulionao katika
utendaji kazi wako kwani wajasiriamali waliofanikiwa wanajua udhaifu wao
na hawathubutu kuona kama vitu vya kuwakwamisha katika shughuli zao,
bali wanachukulia kama moja ya fursa za kufikia malengo yao.
Wajasiriamali waliofanikiwa hujaribu kutumia njia
mpya kwa lengo la kuimarisha mbinu za biashara zao kwa kuhakikisha kuwa
hawafanyi upotevu wowote wa rasilimali katika mchakato mzima wa
uendelezaji/uendeshaji biashara zao.
Jaribu kufikiria juu ya wateja wako kwani hao
ndiyo roho ya biashara yako na bila wao hakuna biashara kwani hakuna
familia yoyote hapa duniani ambayo imewahi kuendesha biashara kwa
kujitegemea kama wateja wanaojitosheleza.
Jambo la msingi hapa ni kujua au kupata taarifa za
jumla za idadi ya watu, hususani wateja ambao watakuwa watumiaji wa
bidhaa au huduma unazozitoa kwani ni muhimu kukumbuka kuwa mchakato wa
kutafuta soko au kujaribu kuuza bidhaa kwa watu ambao hawahitaji
bidhaa/huduma husika ni jambo la kupoteza muda na kujitafutia matatizo
yasiyo ya msingi kama vile msongo wa mawazo na kukata tamaa ya maisha.
Wajasiriamali waliofanikiwa hujikita zaidi
kutafuta masoko kwa watu wanaohitajika au wanaohitaji bidhaa husika na
hivyo kutumia muda vizuri na rasilimali zilizopo.
Pindi wajasiriamali wa aina hii wanapogundua kuwa
wanakidhi mahitaji ya wateja wao hutafuta njia au mbinu za kuhakikisha
kuwa wanawakamata na kuwakumbatia wasiwaponyoke.
Wajasiriamali hawa hufanya kila juhudi ya
kuanzisha uhusiano mzuri wa muda mrefu kwani tunaambiwa kuwa
mjasiriamali mzuri ni yule anayeona bidhaa yake kupitia mahitaji au
dhima ya mteja wake.
Kufikiria juu ya biashara yako ikiwa ni pamoja na
kufikiria kile kinachoendela nje ya biashara yako hasa kile kinachohusu
au kinachoshabihana na biashara yako ili kuwa na uelewa mpana wa mambo
mbalimbali yanayohusu shughuli unazozifanya.
Kufanya uchambuzi wa kina juu ya washindani wako
wa biashara si tu kunakusaidia kujua unayeshindana naye bali pia
kunakusadia kujua matatizo au makosa yanajitokeza katika biashara yako
ikiwa ni pamoja na tafsiri ya kina juu ya biashara yako kwa lengo la
kuleta ufanisi katika utendaji kazi wako.
Ingawa si vizuri kufikiria makosa au kuanguka kwako kulikotokea
siku za nyuma ni vizuri pia ukatumia udhaifu au anguko la kipindi cha
nyuma kama funzo la kuendesha mambo yako kwa mafanikio kwani wahenga
wanasema binadamu hujifunza kutokana na makosa.
Mjasiriamali wa kweli haogopi kushindwa bali
anafikiria zaidi namna ya kupata njia mbadala ya kurekebisha makosa
yaliyotokana au yanayotokana na mchakato mzima wa shughuli za
kijasiriamali kwa lengo la kupata mafanikio zaidi.
CHANZO: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment