Social Icons

Pages

Friday, December 19, 2014

KAMATI KUU CHADEMA YAJADILI UCHAGUZI WA MITAA

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe (Kulia), akizungumza kwenye kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho jijini Dar es Salaam jana. Wengine kulia kwake ni Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willibrod Slaa, Naibu Katibu Mkuu (Bara), John Mnyika na Naibu Katibu Mkuu (Zanzibar), Salum Mwalim.
Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), jana ilianza kikao chake cha kufanya maamuzi magumu kuhusu mambo mbalimbali yanayoendelea nchini ikiwamo kuvurugika kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Kikao hicho maalum cha siku moja,  kilifanyika chini ya Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe jijini Dar es Salaam. Kikao kilianza saa 5:00 asubuhi kwa wajumbe kupewa taarifa kuhusiana na kasoro na hujuma zilizotokea wakati wa uchaguzi huo uliofanyika Jumapili iliyopita nchini kote.
Taarifa kutoka ndani ya kikao hicho zinaeleza kuwa wajumbe pia walielezwa kamatakamata ya wagombea wa Chadema, wanachama na wafuasi wa chama hicho inayoendelea nchini kwa kuhusishwa na  matukio ya vurugu.
Aidha, wajumbe walielezwa kuwa katika baadhi ya maeneo ambako uchaguzi ulivurugika kutokana na sababu kadhaa zilizosababishwa na wasimamizi wa uchaguzi, uchaguzi umeanza kufanyika kwa kushtukiza bila kuwajulisha wananchi hususani wale ambao walionekana ni mashabiki wa vyama vya upinzani. Afisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene, alisema kikao kitakapomalizika taarifa rasmi ya maamuzi itatolewa leo.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: