Wakati Taifa likisubiri kauli ya
Rais Jakaya Kikwete kuhusu utekelezaji wa maazimio ya Bunge ya
kuwawajibisha mawaziri na watendaji wa Serikali waliohusishwa na kashfa
ya Akaunti ya Escrow, Kampuni za IPTL na Pan Africa Power Solutions
(PAP) zimekimbilia mahakamani kuzuia utekelezaji wa maazimio hayo.
Kampuni hizo kwa kushirikiana na Harbinder Singh
Seth zimefungua kesi ya kikatiba Katika Mahakama Kuu ya Tanzania dhidi
ya Waziri Mkuu wa Tanzania, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kuzuia na
Kupamba na Rushwa (Takukuru), Spika wa Bunge na Mwanasheria Mkuu wa
Serikali kupinga utekelezaji wa maazimio hayo.
Kesi hiyo imefunguliwa siku mbili baada ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema kujiuzulu wadhifa
huo akisema ushauri wake wa kisheria kuhusu Akaunti ya Tegeta Escrow
haukueleweka na hivyo kuchafua hali ya hewa. Pia ni katika kipindi ambacho kuna taarifa
zilizothibitishwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue kuwa Rais
Kikwete atazungumzia suala hilo wakati wowote kabla ya kesho.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo zimesambaa katika
mitandao ya kijamii Rais Kikwete atazungumza kupitia wazee wa Mkoa wa
Dar es Salaam leo, lakini Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu,
Salva Rweyemamu alipoulizwa jana hakukanusha wala kukubali akisema
ikitokea Rais anataka kuzungumza vyombo vya habari vitataarifiwa.
Tayari Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliyekuwa ziarani
Uarabuni amerejea nchini jana mchana baada ya ziara yake kukatishwa na
Rais Kikwete kwa shughuli maalumu na anatarajiwa kurudi tena Falme za
Kiarabu kesho kuendelea na ziara yake hadi Desemba 23, mwaka huu.
Kesi yenyewe
Katika kesi hiyo namba 59 ya mwaka 2014,
iliyofunguliwa chini ya hati ya dharura jana, kampuni hizo
zinawakilishwa na mawakili kutoka kampuni za uwakili za Bulwark
Associates Advocates, Asyla Attorneys na Marando, Mnyele & Co.
Advocates za Dar es Salaam.
Katika kesi hiyo, kampuni hizo zinadai kuwa kile
kilichofanyika ndani ya Bunge, kujadili na kupitisha maazimio dhidi ya
watuhumiwa hao, ni kinyume cha Katiba na kwamba kina lengo la
kugombanisha mihimili mitatu ya dola. Kampuni hiyo zinadai kuwa kulikuwa na kesi ambazo
zinaendelea mahakamani zinazohusu suala ambalo Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG), Takukuru walifanyia uchunguzi na hatimaye taarifa ya
CAG kujadiliwa bungeni na kutolewa maazimio hayo.
Maazimio ya Bunge ni pamoja na kutaka waliohusika
wawajibike kwa mujibu wa sheria, Serikali iangalie uwezekano wa
kutaifisha na kuifanya mitambo ya IPTL imilikiwe na Serikali, ipitie
upya mikataba yote na kuangalia kama ina masilahi na Taifa na iboreshwe. IPTL na PAP zimesema kitendo hicho cha kujadili na
kutoa maazimio kilipuuza amri ya Mahakama Kuu kwa kufuata tafsiri
potofu iliyotolewa na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Asha - Rose Migiro
kuhusu amri ya Mahakama hiyo, ambayo ilizua mjadala wa escrow kujadiliwa
bungeni.
Maombi
Mawakili hao wamewasilisha maombi likiwamo la
Mahakama Kuu kutangaza kwamba maazimio hayo ya Bunge ya Novemba 29/2014
na uamuzi wa Spika wa kuyakubali maazimio hayo ni kinyume na Katiba kwa
kuwa yanakiuka Ibara ya 13(1), 13(3), 13 (6)(a) (b)(e) na 24 na 26. Ibara hizo zinataka haki za kila mtu au jumuiya,
kulindwa na kuamriwa na Mahakama ya kisheria au chombo chochote ambacho
kimeanzishwa kisheria, hivyo maazimio hayo ni batili.
Wanadai kuwa maazimio yaliyotolewa na Bunge
yaliegemea upande mmoja kwa vile baadhi ya wahusika walioshiriki
kuyapitisha wana kesi zinazohusiana na suala hilo na walishindwa
kutangaza masilahi yao. Pia wamewasilisha maombi ya amri ya zuio la muda
la utekelezaji wa maazimio hayo, wakidai kufanya hivyo kutaathiri kesi
ya msingi na nyingine zinazoendelea ambazo wadaiwa ni sehemu ya kesi
hizo na kufanya hivyo ni kuifanya Mahakama kuegemea upande wa wadaiwa.
Katika maombi hayo ya zuio, kampuni hizo zinadai
kuwa wadaiwa wanatarajia kutekeleza maazimio yaliyopitishwa na Bunge
ambayo yapo kinyume na iwapo maombi hayo ya zuio hayatasikilizwa kama
suala la dharura, itaathiri haki katika kesi zinazowahusisha wadai na
kuonekana siyo wa muhimu.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment