
Katibu wa Itikadi na Uenezi,Nape Nnauye.
Wabunge kadhaa kutoka CCM wakiwamo mawaziri Sospeter Muhongo wa Nishati na Madini na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, ni miongoni mwa vigogo waliotajwa kuhusika na kashfa hiyo na hivyo Bunge kuazimia kuwa waondoshwe.
Wabunge wengine wa CCM waliohusishwa na kashfa hiyo na kutakiwa kuondolewa kwenye nafasi zao za uenyekiti wa kamati za Bunge ni Mbunge wa Bariadi Mashariki anayeongoza Kamati ya Bajeti, Andrew Chenge , Mbunge wa Sengerema, Wiliam Ngeleja (Sheria, Katiba na Utawala) na Mbunge wa Lupa anayeongoza kamati ya Nishati na Madini, Victor Mwambalaswa.
Akizungumza na NIPASHE jijini Dar es Salaam jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema CCM haina mpango wa kuchukua hatua zozote dhidi ya wote waliotajwa kuhusika na kashfa hiyo kwa sababu hakijawahi kuwajadili kwa jambo hilo ambalo siyo la chama chao bali ni la Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Suala hili lipo chini ya Bunge na hivyo chama hakijaingilia kati na kuchukua hatua wabunge wake waliotajwa,” alisema Nape.
Aliongeza kuwa chama hakiwezi kuchukua hatua zozote dhidi ya wabunge wake waliobainika kula fedha hizo kwani suala hilo halijawahi kufikishwa kwenye vikao vyao.
“Hatujawachukulia hatua (waliotajwa), wala hatuna mpango wa kuwachukulia hatua kwa sababu suala hili haliko ndani ya CCM... liko ndani ya bunge, labda kama litaingia ndani ya chama ndiyo tutalitolea maamuzi,” alisema Nape.
Kauli ya Nape imekuja siku chache baada ya chama hicho kutoa msimamo wake dhidi ya wabunge wa chama hicho waliohusika katika sakata hilo kuwa bunge lichukue hatua stahiki.
Nape, akiwa na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, katika ziara ya kukagua, kuhimiza na kusukuma utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya mwaka 2010/15 mkoani Mtwara, walisema kila aliyehusika katika kashfa hiyo, abebe msalaba wake.
Nape alisema chama hakiwezi kulea maovu yanayofanywa kinyume na kanuni na taratibu za chama hicho, hivyo kama bunge limebaini waliokiuka maadili wachukuliwe hatua stahiki dhidi yao.
Kwa upande wake Kinana alisema muda wa kulindana na kubebana ndani ya chama umeisha na anayekiuka taratibu na kanuni za chama hicho awajibishwe na akishindikana achie ngazi.
Sambamba na kauli hizo pia waliupongeza uamuzi wa bunge kwa kutoa mapendekezo dhidi ya waliohusika na hatua za kuchukuliwa na kuishauri serikali ichukua hatua stahiki na kwa haraka dhidi ya wale wote waliobainika katika sakata hilo.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, wabunge walitoa maazimio manane kuhusu sakata la Escrow likiwamo la kutenguliwa kwa nyadhifa za Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Eliakim Maswi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Frederick Werema.
Wengine ni Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), viongozi wa umma na maofisa wa ngazi za juu serikalini waliohusishwa na vitendo vya kijinai katika sakata hilo linalohusisha kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania (IPTL).
Kadhalika, Takukuru, Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, kutakiwa kufanya uchunguzi dhidi ya wote waliotajwa kuhusika na sakata hilo na watakaobainika kuhusika kwenye vitendo vya jinai hatua za sheria zichukuliwe dhidi yao.
Maazimio mengine ni kumtaka Rais kuunda tume ya uchunguzi ya kijaji kuchunguza tuhuma za utovu wa maadili dhidi ya majaji kuhusishwa kwenye kashfa hiyo.
Majaji waliotakiwa kuchunguzwa ni Jaji Aloysius Mujulizi na Jaji Prof. Eudes Ruhangisa wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Aidha, Bunge lilitaka mamlaka husika za kifedha na za kiuchunguzi kuitaja Stanbic Bank Tanzania Ltd na benki nyingine yoyote itakayogundulika baada ya uchunguzi wa mamlaka za kiuchunguzi kujihusisha na utakatishaji wa fedha zilizotolewa katika akaunti ya Escrow, kuwa ni taasisi zenye shaka ya utakatishaji wa fedha haramu.
Pia, serikali iandae na kuwasilisha muswada wa marekebisho ya sheria iliyounda Takukuru kwa lengo la kuanzisha taasisi mahsusi itakayoshughulikia, kupambana na kudhibiti vitendo vya rushwa kubwa, ufisadi na hujuma za uchumi zinazotishia uhai wa taifa kiuchumi, kijamii na kisiasa kutokana na kushamiri kwa vitendo hivyo.
Serikali imetakiwa kutekeleza azimio la Bunge la kupitia mikataba mibovu ya kuzalisha umeme kati ya Tanesco na kampuni binafsi za kufua umeme na kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mapitio ya mikataba hiyo kabla ya kumalizika kwa Mkutano wa Bunge la Bajeti.
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment