Social Icons

Pages

Thursday, December 04, 2014

MWANAMKE ANA HAKI YA KUMILIKI MALI KISHERIA


 

Ukimuelimisha mwanamke umeielimisha jamii. Ni wakati wa kuondokana na mfumo dume. Mwanamke akiwezeshwa anaweza. Mwanamke ndiye mlezi wa familia.
Ni wakati wa haki sawa kwa wote. Ni wakati wa kuondokana na mila potofu na kulinda haki za mwanamke.
Hizi ndizo kauli zilizotawala majukwaa mengi ya siasa, jinsia, elimu, biashara na hata uchumi pia. Lakini ni muhimu kufahamu je, sheria zinasemaje kuhusu mustakabali wa mwanamke kumiliki mali?
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetamka wazi katika ibara ya 24 kuwa kila mtu ana haki ya kumiliki mali.
Mtu huyo anayetajwa hapo anaweza kuwa mwanamume au mwanamke. Hii haijalishi hadhi yake ya kindoa. Kwa mujibu wa Kifungu cha 56 na 58 cha Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971, mwanamke ana haki ya kununua, kuuza, kumiliki, kutoa au kumilikisha mali binafsi au ya pamoja na mume wake.
Sheria ya Ardhi pamoja na Sheria ya Ardhi ya Vijiji ya mwaka 1999, zimeeleza kinagaubaga pia kwamba mwanamke ana haki ya kumiliki ardhi pasipo kubaguliwa wala kunyanyaswa kwa jinsi yoyote ile.
Kama sheria zote hizi zinamtambua mwanamke, litakuwa ni jambo la kushangaza endapo mwanamke mwenyewe atakuwa hatambui kuwa sheria zinamtambua. Pia litakuwa ni jambo la kutisha na kusikitisha endapo jamii itatumia mfumo dume, ubaguzi, unyanyasaji, ukatili na usanii kumnyima mwanamke haki yake ya kumiliki mali.
Umefika wakati ambao mwanamke hahitaji kusubiri kuolewa ndipo amiliki gari, nyumba, viwanja, mashamba na hata kufanya biashara. Atakuwa amechelewa endapo atasubiri mumewe afe ndipo aanze kumiliki mali.
Hatazifurahia. Anapaswa ajitambue na atambue haki zake kisha achukue hatua za kujikwamua kiuchumi. Uzuri na ubora wa mwanamke wa sasa haupimwi kwenye sura, shepu au umbile alilo nalo, bali ufahamu na maarifa aliyonayo na namna anavyoweza kuyatumia katika kujikwamua kibiashara na kiuchumi. Akiwa vizuri kiuchumi, sura na umbile vinajitengeneza vyenyewe.
Mfumo dume, mila na desturi na sheria kandamizi zimeshapitwa na wakati. Ni ukweli usiopingika kuwa mwanamke akijikwamua kiuchumi jamii yote itakwamuka kiuchumi. Ni kosa kisheria kumnyima mwanamke haki ya kumiliki mali kwa sababu tu yeye ni mwanamke.
Asingelikuwapo mwanamke hata huyo mtoto wa kiume asingelizaliwa. Wote wana haki sawa katika umiliki wa mali. Hakuna aliye bora zaidi kuliko mwenzake. Ni makosa kwa mwanamke kufanya biashara kisirisiri kwa kuogopa kwamba akimshirikisha mume wake atamkataza. Ndoa isiwe gereza la kumfunga mtu kiuchumi au kibiashara.
Mwanamke anapaswa kujitambua, kujithamini, kujitathimini na kujiongeza.
Hakuna biashara ya jinsia fulani peke yake. Ukombozi wa mtoto wa kike wa kesho unaanza kwa kujikomboa kwa mwanamke wa leo.
Anaweza kuwa mjasiriamali wa kiwango cha juu au tajiri mkubwa. Biashara nyingi zilizoanzishwa na wanawake zimedumu kwa muda mrefu. Ulimwengu bado unasubiri ubunifu wa biashara ya mwanamke na hakuna shaka kwamba anaweza kufanya mambo makubwa ya kuushangaza ulimwengu wa biashara.

CHANZO: MWANANCHI

No comments: