Social Icons

Pages

Friday, December 05, 2014

CAG MPYA AONYA WANASIASA

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Juma Assad amewahadharisha wanasiasia na wafanyabishara kwa kuwataka wasichanganye fani hizo kwani kinyume chake watavuruga utendaji na kusababisha athari kubwa kwa jamii.
Profesa Assad ambaye aliapishwa kushika wadhifa huo wiki hii, alitoa tahadhari hiyo jana wakati akihutubia kwenye mkutano mkuu wa mwaka wa wahasibu na wakaguzi (NBAA) unaofanyika jijini hapa.
Akieleza zaidi, CAG Assad alisema ni makosa kuchanganya siasa, biashara na matatizo binafsi katika utendaji wa kazi.
Alisema kuwa ofisi yake na watendaji wengine watafanya kazi kwa kufuata maadili na kila mmoja kuheshimu taaluma yake ili kuleta ufanisi.
Alisema iwapo kila mmoja atawajibika katika nafasi yake na kuaminiana katika shughuli za kila siku ziwe na kitendaji na biashara hakutakuwa matatizo yoyote.
“Matatizo ya watu binafsi yasichanganywe na shughuli za kila siku za ofisi ya CAG na wale wenye kufanya siasa na biashara pia wawajibike katika nafasi zao na ofisi yangu itafanya mambo kwa kufuata katiba ya nchi… wala siyo vinginevyo, ’’ alisema.
Assad alisema kila mtaalamu wa fani husika anapaswa kujifunza mambo mapya, kwani kila uchao teknolojia hupanuka, hivyo nao wanapaswa kwenda na wakati.
Awali akifungua mkutano huo, Naibu Waziri wa Fedha, Adamu Malima, aliwataka wataalamu wa uhasibu na ukaguzi kuwa wazalendo wa kweli kwa kulinda rasilimali za nchi ikiwa ni pamoja na kufuata maadili ya kazi yao bila kuyumbishwa.
Alisema iwapo hilo litazingatiwa, uchumi wa nchi utakuwa hasa ikizingatiwa kuwa taaluma hiyo ndiyo tegemeo katika kukabili matatizo yote ya ulaji fedha na hivyo mara zote wanapaswa kuwajibika kikamilifu.
Alisema baadhi wa wataalamu wa fani hiyo wanafanya kazi nzuri lakini wengine wanafanya vibaya na kwamba imefika wakati kila mmoja atambue kuwa fani hiyo ni muhimu kwa maendeleo ya taifa.
“Fahari ya kazi hii ni kufanya kazi kwa kufuata maadili na siyo vinginevyo. Na nyie ni lazima mtambue kuwa ni watu muhimu sana kwa maslahi ya nchi,” alisema Mwenyekiti wa Bodi ya NBAA, Isaya Jairo, alisema bodi hiyo itawaleta wataalamu kutoka nje ya kwa ajili ya kutoa mafunzo ya kazi katika sekta ya gesi na madini ili kuongeza ufanisi zaidi na kufanya shughuli hiyo kwa uweledi mkubwa.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: