Jaji Gadi Mjemas anayesikiliza kesi inayomkabili
wakili maarufu jijini Arusha, Medium Mwale na wenzake watatu, ametupilia
mbali pingamizi lililowekwa na upande wa utetezi kupinga kupokelewa
maelezo ya mshitakiwa, Elias Ndejembi, kwa madai wakati akiyatoa
hayakurekodiwa na pia muda alioitwa polisi na aliomaliza kutoa maelezo
hayo haukutajwa.
Pia upande huo wa utetezi unadai wakati mshtakiwa huyo akitoa maelezo hayo, mke wake ambaye alikuwa shahidi wake alitolewa nje. Akitoa uamuzi wa pingamizi hilo, Jaji Mjemas alihoji endapo mke wa
mshitakiwa Ndejembi alitolewa nje, alikubalije kuandika maelezo yake
wakati akijua ndiye shahidi wake.
Jaji huyo pia alisema hakuna kifungu chochote cha sheria kinamtaka
ofisa wa polisi kurekodi muda wa mtuhumiwa kuanza kutoa maelezo ya onyo
na anapomaliza na kwamba hana mashaka kuwa haki za mshitakiwa
zilizingatiwa kwani sheria inataka ahojiwe si zaidi ya saa nne na
inaonyesha ilizingatiwa.
“Natupilia mbali hoja ya kwanini mtuhumiwa wakati anarekodiwa
maelezo yake mkewe alitoka nje wakati katika maelezo ya Mdemu inaonyesha
kabla ya kumhoji alimkumbusha kosa analoshtakiwa nalo pamoja na jina
lake na mahali anapokaa, kwa hiyo hakuna ukiukwaji uliofanywa wakati
wakuchukuliwa maelezo yake," alisema.
Awali, Mrakibu wa Msaidizi wa Polisi, Fadhili Mdemu, wakati akitoa
ushahidi wake, kuliibuka malumbano ya kisheria baada ya Mdemu kudai
aliandika maelezo ya mshtakiwa wa nne, Ndejembi na mshtakiwa wa pili Don
Bosco Gichana ambaye ni raia wa Kenya.
Baada ya shahidi huyo kueleza hayo, wakili wa utetezi, Albert
Msando, alikataa kupokelewa kwa maelezo ya Ndejembi kwa kile alichodai
yanaonyesha alihojiwa saa 9:18 alasiri, lakini hayaonyeshi alikamatwa
na kushikiliwa na polisi kuanzia muda gani.
Msando alidai maelezo hayo yana mapungufu kisheria kwani
hayajaambatanishwa na fomu ya uthibitisho kuonyesha mshtakiwa aliyasoma
na kuridhia kuwa ni yake.
“Inaonyesha mshtakiwa alipigiwa simu saa 2:00 asubuhi lakini
haielezi alikuwa chini ya ulinzi wa polisi kuanzia saa ngapi na muda
gani ulipita kabla hajahojiwa. Sheria iko wazi mtuhumiwa anapaswa
kuhojiwa ndani ya saa nne baada ya kuwa chini ya ulinzi wa polisi,”
aliendelea kudai Msando.
KESI NDANI YA KESI
Baada ya malumbano hayo ya kama maelezo ya mshtakiwa yakubaliwe
kama kielelezo au la, Jaji Mjemas aliamua suala hilo kusikilizwa kwenye
kesi ndani ya kesi, ambapo upande wa serikali uliahidi kupeleka
mashahidi watatu, huku upande wa utetezi ukiahidi kupeleka wawili.
Mawakili wa utetezi kwa pamoja walipinga kupokelewa kwa maelezo hayo, huku wakitoa hoja mbalimbali za kisheria.
Wakili wa utetezi, Moses Mahuna, alipinga kupokelewa kwa maelezo
hayo, akidai yaliandikwa bila kuonyesha kifungu cha sheria kilichokiukwa
na mshtakiwa.
Alidai kutoandikwa kwa kifungu cha sheria kilichokiukwa kunamfanya
mtuhumiwa ashindwe kuelewa mtiririko mzima wa maelezo ya onyo.
Hata hivyo, kesi hiyo ilishindwa kuelendelea kusikilizwa, kutokana na wazee wa baraza kutokuwapo na imepangwa kuendelea leo. Washtakiwa hao wanne wanakabiliwa na mashtaka 44, ikiwamo ya kula njama kutenda kosa, utakasaji fedha haramu na kughushi.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment