Social Icons

Pages

Tuesday, December 08, 2015

DK. SHEIN SASA AWASHUKIA WATAALAM WA AFYA Z'BAR


Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein.
Wahitimu wa Chuo cha Taaluma za Sayansi za Afya Zanzibar, wametakiwa kuacha tabia ya kupiga chenga wanapopangiwa kufanya kazi kisiwani Pemba jambo linalosababisha upungufu wa wataalam katika sekta ya afya kisiwani hapa.
Wito huo umetolewa na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, kwenye Mahafali ya 22 ya Chuo hicho yaliyofanyika Mbweni Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja jana.
Akisoma hotuba kwa niamba ya rais, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, alisema kuna wahitimu wa fani ya afya Zanzibar wamekuwa wakipiga chenga kufanya kazi kisiwani Pemba.
Alisema kwa mujibu wa sheria, watumishi wa umma wanatakiwa kuwa tayari kufanya kazi sehemu yoyote watakayopangiwa na kuwataka kubadilika na kuwa tayari kuwatumikia wananchi kokote ili kufanikisha mpango wa kuimarisha huduma za afya kwa wananchi wa Zanzibar.
“Nimefurahi kusikia kuwa katika orodha ya wahitimu wetu wa fani za afya chuoni hapa wapo waliotoka Tumbatu, Kojani, Fundo, Mtende na maeneo mengine ambayo watu wengi huwa wanaona tabu kwenda kufanya kazi kutokana na mazingira ya kijiografia yaliyopo,“ alisema Balozi Seif.
Katika hotuba yake, Dk. Shein pia aliitaka Wizara ya Afya kufanya tathmini ya mahitaji ya wataalam wa afya ili kufahamu changamoto zake na hatua za kuchukua.
Aidha, alisema uwekezaji katika sekta ya afya Zanzibar umeanza kuleta mafanikio makubwa baada ya wawekezaji wa ndani na nje kujitokeza na kuanzisha hospitali kubwa visiwani hapa.
Alisema juhudi zinazochukuliwa na serikali katika kuimarisha huduma za afya kwa kushirikiana na wawekezaji na washirika wa maendeleo, zimekuwa na mchango mkubwa katika kukuza pia soko la ajira hasa kwa wahitimu wa chuo hicho.
“Machi mwaka huu nilialikwa kuifungua Hospitali ya Tasakhtaa inayoendeshwa na Global Hospital ya India katika Mtaa wa Vuga. Hii ni hospitali ya kisasa yenye uwezo mkubwa wa kutibu maradhi mbalimbali,“ alisema DK. Shein katika hotuba yake.
Hata hivyo, aliwataka wahitimu wa Chuo cha Taaluma za Sayansi za Afya Zanzibar, kuchangamkia ajira zinazotolewa na serikali na sekta binafsi wakitambua kuwa hospitali zote zina lengo la kuimarisha huduma za afya kwa wananchi wa Zanzibar.
Wahitimu 440 walihitimu na kufanikiwa kupata stashahada, hiyo ikiwa ni karibu mara mbili ikilinganishwa na wahitimu 280 wa mwaka 2014.
Muhitimu Faika Karim Zam, aliuomba uongozi wa chuo hicho kuanzisha mafunzo ya ngazi ya Shahada na Diploma ili kuwapunguzia gharama za kusoma ngazi hiyo nje ya Zanzibar.
Mapema Mkuu wa chuo hicho, DK. Haji Mwita Haji, alisema uongozi wa chuo chao kupitia baraza lake umeamua kuongeza majengo zaidi ili kuwahudumia vema wanafunzi wanaoamua kujiunga na chuo hicho.
Awali Naibu Waziri wa Afya Zanzibar, Mahmoud Thabit Kombo, aliwataka wahitimu kufuata maadili  ya kazi zao ili kupunguza au kuondosha malalamiko ya huduma mbovu kutoka kwa wananchi.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: