Social Icons

Pages

Monday, November 09, 2015

SBL YAFADHILI 100% WANAFUNZI UDSM

Meneja Miradi Endelevu wa SBL, Hawa Ladha.
Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL), imetoa ufadhili kwa wanafunzi wahitaji katika masomo ya chuo kikuu.Wanafunzi hao waliofaulu daraja la kwanza wanaanza masomo yao mwaka huu wa masomo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). 
Wanafunzi waliopata ufadhili huo ni Michael Daniel na Consolatha Mushi, wanaokwenda kusomea uhandisi wa ujenzi na Lisa Kalokola, anayekwenda kusomea uhandisi wa madini. Ufadhili huo utahusisha gharama za karo, malazi na fedha ya kujikimu kwa mwezi kwa asilimia 100.
Meneja Miradi Endelevu wa SBL, Hawa Ladha, alisema mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam kuwa ufadhili huo unafanyika kupitia mfuko wa East African Breweries Limited (EABL) Foundation. “Hii ni moja ya mikakati ya kampuni hii kusaidia jamii,” alisema. Alisema mfuko huo hutenga fedha kila mwaka kusaidia miradi mbalimbali ya kijamii ikiwamo ya elimu.
Alifafanua kuwa wanafunzi waliopata ufadhili huo ni wale walioomba na kutimiza vigezo vilivyowekwa na kampuni. 
Aliwataka vijana hao kutumia vizuri ufadhili huo kwa kusoma kwa bidii ili baada ya kuhitimu watoe mchango kwa familia zao na taifa kwa ujumla. Mmoja wa wanafunzi hao, Laurent, alisema ufadhili huo utamsaidia mno katika masomo yake. 
“Nimefaulu vizuri kidato cha sita, lakini sikuwa na uwezo, ufadhili huu wa asilimia 100 ni ukombozi,” alisema.
Alisema atatumia fursa hiyo kusoma kwa bidii na kufaulu vizuri ili ndoto zake katika maisha zitimie.
Kwa upande wake, Kalokola aliipongeza kampuni hiyo kwa kutenga fedha kusaidia jamii na hasa katika sekta ya elimu. “Wanafunzi wasio na uwezo wachangamkie fursa kama hizi zinapotangazwa,” alisema.
EABL Foundation ilianza kutoa ufadhili huo wa elimu vyuo vikuu tangu mwaka 2005 na kufaidisha zaidi ya vijana 200 katika nchi za Afrika ya Mashariki.  Kwa Tanzania, programu hiyo imeshafadhili vijana zaidi ya 25 wanaofanya kazi katika kampuni mbalimbali. 
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: