Social Icons

Pages

Monday, November 09, 2015

MAALIM SEIF: NASUBIRI KUAPISHWA URAIS Z'BAR


Mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Wananchi (CUF) Maalim Seif Sharif Hamad, amesema kuwa hana wasiwasi kuhusu ushindi wake kutokana na idadi kubwa ya kura alizopata dhidi ya mpizani wake, Dk. Ali Mohammed Shein, katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Amesema kwa sasa anajihesabu kama Rais anayesubiri kuitwa na kuapishwa na sasa yupo katika matayarisho ya kuunda serikali ili akiapishwa asipoteze tena muda wa kufikiria kuunda serikali hiyo.
Maalim Seif aliyasema hayo wakati akizungumza na wajumbe wa mkutano mkuu ngazi za wilaya na majimbo katika ukumbi wa Majid Kiembesamaki, nje kidogo ya mji wa Zanzibar.
Alisema tayari dunia nzima wanamfahamu Rais aliyechaguliwa na wananchi wa Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu uliopita na kuwataka wanachama wa chama hicho kuacha kusikiliza kile alichokiita propaganda za Chama Cha Mapinduzi (CCM) zinazoeleza kurejewa kwa uchaguzi.
Alisisitiza msimamo wake kuwa hakuna sababu za kurejewa kwa uchaguzi huo kwani ulishakamilika katika ngazi zote na washindi wa uwakilishi na udiwani kutangazwa bila ya kuwapo malalamiko yoyote na kwamba kinachosubiriwa hivi sasa ni kukamilika kwa kazi ya uhakiki wa kura za urais kwa majimbo yaliyobakia na hatimaye mshindi wa uchaguzi huo atatangazwa.
“Niwaambie wafuasi na wapenzi wa CUF tembeeni kifua mbele kutokana na ushindi mkubwa nilioupata katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 25 mwezi uliopita,” alisema.
Maalim Seif alisema ushindi huo umeleta matumaini mapya kwa Wazanzibari ambao wameitumia vyema haki yao ya kupiga kura na kuwachagua viongozi wanaowataka.
Alisema hakuna namna yoyote ya kupindua maamuzi ya wananchi waliyoyafanya kupitia masanduku ya kura.
Alisema wanachokifanya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (Zec) hivi sasa ni kuchelewesha kukamilisha uhakiki wa kura kwa majimbo 14 yaliyobakia na kumtangaza mshindi wa urais na hivyo kuishauri Zec kukamilisha kiazi hiyo ili serikali mpya ianze kufanya kazi ya kuwatumikia wananchi.
Akizungumzia madai ya ongezeko la kura katika kisiwa cha Pemba, Maalim Seif alisema hayana ukweli kwani hakuna hata kituo  kimoja kilichozidishwa wapiga kura 350 kilichopangiwa na kwamba vituo vingi vilikuwa na wapigakura chini ya idadi hiyo. 
Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Mipango na Chaguzi wa CUF, Omar Ali Sheikh, alisema licha ya ushindi wa urais, chama hicho pia kimepata ushindi mkubwa kwa nafasi za uwakilishi na udiwani.
Sheikh alisema katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, CUF ilipata Wawakilishi wanne  na madiwani saba kwa upande wa Unguja ambapo uchaguzi wa 2015, imefanikiwa kupata Wawakilishi tisa na madiwani 15.
Aidha alisema CCM imepoteza wodi zote tatu za udiwani katika kisiwa cha Pemba na kuifanya ishindwe kupata mjumbe yeyote wa Baraza la Wawakilishi, Ubunge na Udiwani.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: