Hatimaye aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi 
(CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, amejitokeza kwa mara ya kwanza kwenye 
ofisi za makao makuu ya chama hicho zilizopo Buguruni jijini Dar es 
Salaam na kumtaka Rais Jakaya Kikwete amalize haraka mgogoro wa uchaguzi
 uliopo Zanzibar kabla ya kumpisha mrithi wake, Dk. John 
Magufuli.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi kuu za CUF jana, 
Lipumba alisema jaribio lolote la kutaka Rais Kikwete aondoke na 
kumuachia Magufuli suala hilo ni sawa na kumtwisha rais ajaye (Magufuli)
 mzigo mkubwa ambao hatauweza na mwishowe ni kusababisha madhara makubwa
 visiwani humo ikiwamo vurugu na uvunjifu wa amani.
Profesa Lipumba aliyasema hayo ikiwa imepita takriban miezi mitatu 
tu tangu atangaze kujiuzulu uenyekiti wa CUF Agosti 6, 2015 ili awe 
mwanachama wa kawaida wa chama hicho.
Lipumba alitangaza kuchukua uamuzi huo wa utata kutokana na kile 
alichodai kuwa ni kupinga uamuzi wa chama chake na vingine vinavyounda 
umoja wa katiba ya wananchi (Ukawa) vya NLD, NCCR-Mageuzi na Chama cha 
Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuwapokea waliokuwa makada wa CCM na 
kuwapa nafasi ya kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi mkuu 
uliofanyika Oktoba 25, 2015.   
Akieleza zaidi jana, Lipumba alisema Kikwete ana uelewa mpana wa 
masuala ya kisiasa na kwamba akiamua kwa dhati, anao uwezo mkubwa wa 
kumaliza mgogoro uliopo sasa Zanzibar kabla ya kumkabidhi madaraka 
Magufuli ifikapo Ahamisi ya Novemba 5 mwaka huu.
Alisema Rais Kikwete amewahi kuishi Zanzibar alipokuwa wakati 
katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na anaijua hali ya kisiasa visiwani 
humo kuliko ilivyo kwa mrithi wake, Dk. Magufuli.
“Suala hili Rais Kikwete ulimalize kabla ya Dk. Magufuli 
kuapishwa… usimwachie kwa kuwa (ni wazi) utampa mzigo mkubwa ambao 
hatauweza na (hakika) nchi itavurugika,” alisema Lipumba.
Hivi sasa, Zanzibar imeingia katika mgogoro mkubwa wa kisiasa baada
 ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha,
  kutangaza kufutwa kwa uchaguzi uliofanyika Oktoba 25 kutokana na kile 
alichodai kuwa ‘haukuwa huru na wa haki’, ingawa ndiyo uliotumika kupata
 kura zilizompa ushindi Magufuli kuwa Rais mteule wa Jamhuri ya Muungano
 wa Tanzania.  Umuazi huo wa Jecha umepingwa na CUF ambayo mgombea wake,
 Maalim Seif Sharif Hamad, aliitisha mkutano na waandishi wa habari hapo
 kabla na kuwaonyesha karatasi za matokeo halisi ya kura kutoka katika 
vituo vyote visiwani humo zkionyesha kuwa ameshinda kwa asilimia 52.87.
MAALIM SEF MSHINDI URAIS 
Akielezea zaidi kuhusiana na hali ya Zanzibar baada ya uchaguzi 
mkuu, Lipumba alisema njia pekee ya Rais Kikwete kumaliza mgogoro huo ni
 kuitaka ZEC iendelee na mchakato wa majumuisho ya kura na kumtangaza 
mshindi ambaye ni wazi anajulikana kuwa ni Maalim Seif, hiyo ikiwa ni 
kwa mujibu wa karatasi za matokeo ya kura zilizokusanywa kutoka kwenye 
vituo vyote visiwani humo.
Alisisitiza kuwa endapo Rais Kikwete atamkabidhi madaraka Magufuli 
kabla ya kumaliza mgogoro uliopo Zanzibar, ni dhahiri atakuwa amemuweka 
kwenye wakati mgumu na upo uwezekano kuwa mrithi wake huyo atatumia 
nguvu kubwa kutatua mgogoro huo, jambo ambalo ni la hatari zaidi kwa 
hatma ya Zanzibar na taifa. Aliongeza kuwa Dk. Magufuli hataweza 
kuiongoza nchi kwa amani ikiwa Zanzibar kutakuwa na machafuko,  hivyo 
Rais Kikwete anapaswa kulimaliza jambo hilo kabla hajamaliza muda wake 
wa uongozi.
“Kama watu wanavyomuita Magufuli kuwa ni tingatinga au bulldozer, 
basi ni dhahiri atatumia nguvu katika kutatua mgogoro huo… na jambo hilo
 litakuwa ni la hatari kubwa kwa Zanzibar na taifa,” alisema Lipumba.
MARUDIO UCHAGUZI, DK. SHEIN
Lipumba aliongeza kuwa wananchi wa Zanzibar hawawezi kurudia 
kufanya uchaguzi kwa mara ya pili kwa kuwa walishapiga kura na 
zikahesabiwa, na mgombea wao waliyemtaka alishaibuka mshindi.
Aidha, Lipumba alimtaka rais wa sasa, Dk. Ali Mohamed Shein, 
kukumbuka uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 pale ZEC ilipomtangaza yeye (Dk. 
Shein) kuwa mshindi kwa kupata asilimia 50.2 dhidi ya Maalim Seif 
asilimia 49.8, lakini Maalim Seif alikubali na Dk. Shein akawa Rais. 
Alisema Dk. Shein akumbuke pia matukio yaliyotokea mara baada ya 
uchaguzi wa mwaka 2000 ambao majimbo 16 ya mkoa wa Mjini Magharibi 
uchaguzi wake ulifutwa na ukarudiwa kwa nguvu na CUF waliitisha 
maandamano Januari 27, 2001 na makumi ya watu kuuawa huku watu wengine 
zaidi ya 2,000 kuwa wakimbizi Shimoni, Mombasa Kenya; jambo ambalo nchi 
haipaswi kulishuhudia tena.
Lipumba alisema sasa ni wakati muafaka kwa Dk. Shein kuonyesha 
ukomavu wa kisiasa kwa kukubali maamuzi ya Wazanzibari bila kuruhusu 
visiwa hivyo kuingia katika machafuko.
AJADILI KATIBA YA ZANZIBAR
Lipumba alisema katika katiba ya Zanzibar , Sura ya 9, inazungumzia
 ZEC na kadri alivyoisoma, hakuna kifungu chochote kinachoipa mamlaka 
 ZEC wala Mwenyekiti wa ZEC uwezo wa kufuta Uchaguzi Mkuu.
Alisema katiba hiyo na sheria yake haijawapa mamlaka  ZEC wala 
Mwenyekiti kufuta uchaguzi, bali Sura ya 9, kifungu cha 119, fasiri ya 
10, inaeleza kuwa maamuzi ya ZEC yatafanyika ikiwa kuna akidi imetimia 
na akidi hiyo lazima pawapo na Mwenyekiti au Makamu Mwenyekiti wa ZEC na
 wajumbe wengine wanne ndipo kikao cha maamuzi kinaweza kufanyika.
Aliongeza kuwa kwa mujibu wa katiba hiyo, maamuzi yoyote ya ZEC 
yatakayotolewa lazima yatokane na uwingi wa wajumbe wa ZEC waliokuwapo 
katika kikao rasmi ambacho akidi yake imetimia asilimia mia moja.
Alisema Mwenyekiti wa ZEC, Jecha, alitoa maamuzi ambayo hayakutokana na kikao rasmi cha tume hiyo.
Alisema hata kikao hicho kikifanyika, Katiba ya Zanzibar na Sheria 
za Uchaguzi za Zanzibar hazijawapa mamlaka ZEC ya kufuta uchaguzi bali 
ZEC imepewa mamlaka ya kuahirisha uchaguzi kama kumetokea tatizo.
AMKUMBUSHA MAGUFULI KUHUSU ESCROW
Katika hatua nyingine, Lipumba alisema kama Dk. Magufuli ana nia ya
 dhati ya kuleta maendeleo na kutokomeza ufisadi nchini kama alivyoahidi
 wakati wa kampeni zake, basi aanze kuwashughulikia watuhumiwa wa kashfa
 ya akaunti yaTegeta Escrow.
Alisema Dk. Magufuli anapaswa kuwakamata watuhumiwa wote 
waliohusika katika kashfa hiyo na kuwafikisha mahakamani ili sheria 
ichukue mkondo wake.
     CHANZO:
     NIPASHE
    

No comments:
Post a Comment