Wakati saa 48 zilizotolewa na mgombea urais kwa 
tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad kutaka 
Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kuendelea na mchakato wa majumuisho ya 
kura na kumtangaza mshindi wa urais wa Zanzibar zikiwa zimemalizika, 
Ikulu ya Jamhuri ya Muungano imesema haijapokea maombi ya Maalim Seif 
kutaka kuonana na Rais Jakaya Kikwete.
Ijumaa iliyopita, Maalim Seif aliwaambia waandishi wa habari 
visiwani Zanzibar kuwa baada ya ZEC kufuta uchaguzi Jumanne iliyopita, 
alifanya jitihada kadhaa za kuwasiliana na Rais Kikwete na pia Rais wa 
Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, ili kuzungumzia suala hilo kwa maslahi 
ya Zanzibar lakini wito wake huo umekuwa ukipuuzwa.
Maalim Seif alisema tangu kufutwa kwa uchaguzi, amefanya juhudi za 
kutafuta ufumbuzi kwa kukaribisha mazungumzo na viongozi wenzake wa 
kitaifa akiwamo Rais Kikwete na pia Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed 
Shein, lakini wote wamekuwa wakimkwepa, licha ya kuanza kuwatafuta kwa 
kutumia mawasiliano ya simu na ujumbe kupitia wasaidizi wao, akitaka 
wakutane.
Hata hivyo, taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu 
iliyotolewa kwa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam jana, ilieleza 
kuwa Ikulu imesikitishwa na madai ya Maalim Seif, ikieleza kuwa siyo 
kweli.
Badala yake, Ikulu imesema haijapokea ombi lolote kutoka kwa Maalim
 Seif la kutaka kukutana na Rais Kikwete tangu siku ya kupiga kura na 
hata baada ya Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha, kufuta uchaguzi wa 
Zanzibar.
Taarifa hiyo ya Ikulu imesema kile ambacho Rais Kikwete amekipokea 
ni malalamiko ya CUF kuhusu baadhi ya vitendo kutoka kwa baadhi ya 
askari wa Jeshi la Polisi Zanzibar na ombi kwa ajili ya kuwezesha 
mazungumzo kati ya Maalim Seif na Mkuu wa Majeshi (CDF), Jenerali Davis 
Mwamunyange.
“Baada ya hapo, Rais Kikwete, ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu, 
amemuagiza Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Ernest Mangu, kuchunguza 
madai haya ya CUF na kumletea taarifa. Kadhalika, ametoa maelekezo 
ofisini kwake ya kuwezesha mazungumzo kati ya Jenerali Mwamunyange na 
maafisa wa CUF,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa Ikulu Rais Kikwete amekuwa akiguswa na 
hali ya kisiasa na usalama wa Zanzibar kama ilivyo kwa Watanzania 
wengine na amekuwa akifanya kazi bila kuchoka huku akipata ushauri wa 
kina juu ya kilichotokea Zanzibar siku chache zilizopita na kupata 
ufumbuzi.
Taarifa hiyo ilifafanua zaidi kuwa wakati jambo hilo likiwa bado 
katika mikono ya ZEC ambacho ni chombo huru cha uchaguzi, Rais Kikwete 
yuko tayari kufanya chochote kilicho ndani ya uwezo wake ili kupata 
suluhisho jema kuhusiana na hali ya Zanzibar.
KUFUTWA UCHAGUZI
Suala la kufutwa kwa uchaguzi Zanzibar linadaiwa kuviingiza visiwa hivyo katika mgogoro wa kikatiba na kisheria.
Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha, alitaja sababu tisa za 
kufikia uamuzi wa kufuta uchaguzi huo kuwa ni pamoja na kura kuongezeka 
katika baadhi ya majimbo kisiwani Pemba na pia baadhi ya makamishna wa 
Zec kutanguliza itikadi za vyama hadi kuvua mashati ili kupigana.
Kadhalika, alisema katika baadhi ya vituo, masanduku ya kupigia 
kura yaliporwa na kwenda kuhesabiwa nje ya vituo, kitendo ambacho ni 
kinyume cha sheria ya uchaguzi na pia, kuna taarifa ya kufukuzwa kwa 
baadhi ya mawakala wa wagombea na hivyo kushindwa kutekeleza wajibu wao.
Hata hivyo, waangalizi wa ndani na wa kimataifa, wakiwamo Umoja wa 
Ulaya (EU), Jumuiya ya Madola Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya 
Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Jumuiya ya Afrika 
Mashariki (EAC), waangalizi wa Marekani na Uingereza, katika ripoti zao 
wamesema uchaguzi wa Zanzibar mwaka huu ulikuwa huru na wa haki na 
kutaka Zec ikamilishe kazi ya kuhesabu kura na kumtangaza mshindi.
     CHANZO:
     NIPASHE
    

No comments:
Post a Comment