Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova.
Polisi wanaodaiwa kuwa na silaha za moto wamevamia
na kuzingira ofisi ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC),
jijini Dar es Salaam na kisha kuchukua kompyuta 27, simu za mkononi 25
na kuwakamata watumishi 36 wa kituo hicho.Tukio hilo lilitokea jana mchana kwa kile kilichoelezwa kuwa ni
uwezekano wa kituo hicho kuwa na matokeo ya uchaguzi ambayo yapo kinyume
cha yale yaliyokuwa yakikusanywa na kutangazwa na Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (Nec) ambayo kisheria ndiyo yenye wajibu wa kuyatangaza.
Akizungumza na Nipashe jana, Mwanasheria na Mkurugenzi wa Utetezi
na Maboresho wa LHRC, Harold Sungusia, alisema polisi wakiwa na silaha
walivamia ofisi hizo na kuwaweka chini ya ulinzi kabla ya kukamata vifaa
vyao.
“Tumepewa kibali na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) kufuatilia
uchaguzi, lakini katika hali ya kushangaza polisi wametuvamia,
wamekusanya kompyuta zetu 27, wamechukua simu 25 na kuwaweka chini ya
ulinzi vijana wetu 36,” alisema.
Alisema vifaa na vijana waliokamatwa walikuwa wanapokea taarifa
kutoka kwa waangalizi wa uchaguzi walioko kwenye majimbo mbalimbali
nchini ili waandike taarifa ya mwenendo wa uchaguzi ambayo baadaye
ingetangazwa kwa umma.
Kaimu Mkurugenzi wa LHRC, Emelda Urio, alisema polisi walivamia
kituo hicho majira ya saa 8:30 mchana na kutaka kuwapekua kwa madai kuwa
wanakusanya taarifa za uchaguzi na kuzisambaza kwa umma.
Alisema baada ya kuonyeshwa kibali cha upekuzi, walikubali
kupekuliwa lakini waliwaambia polisi kuwa wao (LHRC) ni waangalizi wa
ndani ambao wana kibali cha kufuatilia mchakato wa uchaguzi.
Majira ya saa 1:30 usiku, Nipashe ilishuhudia polisi wenye silaha
wakiwa kwenye magari mawili aina ya Land Cruiser wakiondoka na vifaa
hivyo, huku vijana 36 wakipakiwa kwenye moja ya mabasi ya Uda kuelekea
kituo kikuu cha polisi.
Upekuzi katika kituo hicho uliongozwa na mpelelezi wa Kawe, aliyetajwa kwa jina moja la OCD Mgonja.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura, alipotafutwa
na Nipashe, dereva wake alipokea simu na kueleza kuwa yupo kwenye
kikao.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman
Kova, alipoulizwa kuhusiana na tukio hilo, alikataa kulizungumzia kwa
madai kuwa anayehusika nalo ni Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni.
Kabla ya tukio la jana, wengine waliowahi kukamatwa kutokana na
tuhuma zinazohusiana na majumuisho ya kura ni vijana zaidi ya 100 wa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wanaodaiwa walikuwa
wakikusanya na kulinganisha kura alizopata mgombea wao wa urais, Edward
Lowassa, kutoka katika majimbo mbalimbali nchini.
Chadema imekuwa ikipinga matokeo yaliyotangazwa na Nec na kumpa ushindi mgombea wa Chama Cha Mapinduzi, Dk. John Magufuli.
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment