Social Icons

Pages

Friday, October 30, 2015

NI MAGUFULI

Mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli.
Hatimaye, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imemtangaza rasmi mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, kuwa mshindi wa nafasi ya urais kwa kipindi cha miaka mitano ijayo hadi 2020.
Ushindi huo wa Magufuli umempa fursa ya kuwa Rais ajaye wa awamu ya tano, atakayemrithi Rais Jakaya Kikwete, anayemaliza muda wake. Akitangaza matokeo hayo jana, Mwenyekiti wa Nec, Jaji mstaafu Damian Lubuva, alisema walioandikishwa ni wapiga kura 23,161,440 na waliopiga kura ni 15,589,639, sawa na asilimia 67.31 ya waliojiandikisha.
Alisema kura halali ni 15,193,862, sawa na asilimia 97.46, huku kura zilizokataliwa zikiwa ni 402,248, sawa na asilimia 2.58.
Alisema Dk. Magufuli amekuwa mshindi wa kinyang’anyiro hicho baada ya kupata kura 8,882,935, sawa na asilimia 58.46, akiwaacha mbali wagombea wenzake akiwamo mshindani wake wa karibu, Edward Lowassa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) aliyepata kura 6,072,848, sawa na asilimia 39.97. 
Kwa mujibu wa matokeo hayo, Lowassa aliyekuwa pia akiwakilisha muungano wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ameachwa na Dk. Magufuli kwa tofauti ya kura 2,810,087.
Jaji Lubuva aliwataja wagombea wengine sita walioshiriki uchaguzi huo na kura walizopata kuwa ni Anna Mghwira wa ACT-Wazalendo aliyepata kura 98,763 (asilimia 0.65), Chifu Lutalosa Yemba wa ADC aliyepata kura 66,049 (asilimia 0.43),  Hashim Rungwe wa Chaumma aliyepata kura 49,256 (asilimia 0.32), Maximillian Elifatio Lymo wa TLP kura 8,198 (asilimia 0.05), Fahmy Dovutwa wa UPDP aliyepata kura 7,785 (asilimia 0.05) na Kanken Kasambala wa NRA aliyepata kura 8,028, sawa na asilimia 0.05.
Kabla ya kutangaza matokeo hayo, Jaji Lubuva alisema kati ya wagombea nane, sita wamekubali kusaini matokeo hayo kama ishara ya kukubaliana na matokeo huku Chaumma na Chadema wakiyagomea matokeo hayo.
Alisema kwa mujibu wa katiba na sheria ya uchaguzi, baadhi ya vyama kukataa kusaini matokeo hayo hakuizuii Nec kuendelea na shughuli ya kumtangaza na kumpa cheti cha ushindi mshindi wa nafasi husika.
Kadhalika, alisema kwa mujibu wa katiba na sheria, baada ya mgombea urais kushinda, na mgombea mwenza wake anakuwa mshindi wa nafasi hiyo.
 
UCHAGUZI ULIOPITA HALI ILIKUWAJE?
Matokeo ya uchaguzi wa mwaka huu yanaonekana kuwa na ushindani mkali zaidi kulinganisha na chaguzi zilizopita kutokana na tofauti ya asilimia ya kura kati ya mshindi na waliomfuatia.
Katika uchaguzi uliopita wa mwaka 2010, Rais Jakaya Kikwete aliipatia CCM ushindi wa asilimia 61.16 baada ya kupata kura 5,275,899, akifuatiwa na Dk. Willibrod Slaa wa Chadema aliyepata kura 2,271,885, sawa na asilimia 26.34; Prof. Ibrahim Lipumba wa Chama cha Wananchi (CUF) alipata kura 697,014 (asilimia 8.08), Peter Mziray wa APPT Maendeleo alipata kura 96,932, Hashimu Rungwe aligombea kupitia NCCR- Mageuzi na kupata kura 26,321 (asilimia 0.3); Mutawega Mgahywa wa TLP alipata kura 17,434 (asilimia 0.20) na Fahmi Dovutwa wa UPDP aliyepata kura 13,123, sawa na asilimia 0.15.
 
APONGEZWA
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, alisema anashukuru matokeo yametoka na Dk. Magufuli amekuwa rais mteule wa Tanzania. Mwakilishi wa NRA alisema katika kugombea nafasi za uongozi kuna kushinda na kushindwa na kwamba ni lazima apatikane mshindi ambaye kwa uchaguzi wa mwaka huu ni Dk. Magufuli. Wengine waliompongeza Magufuli baada ya kutangazwa mshindi jana ni wawakilishi kutoka TLP na pia Baraza la Kikristo Tanzania (CCT).
 
WAMIMINIKA OFISI ZA CCM 
Wafuasi wa CCM, jana walifurika nje ya ofisi za chama hicho mtaa wa Lumumba jijini Dar es Salaam kushangilia ushindi wa mgombea Urais, Dk. John Magufuli.
Wafuasi na makada wa chama hicho walianza kuwasili nje ya ofisi hizo saa 9:00 alasiri muda mfupi kabla ya kuanza kutangzwa kwa matokeo. Mara baada ya Dk.  Magufuli kutangazwa rasmi kuwa mshindi, wafuasi hao walilipuka kwa shangwe na kuanza kuimba nyimbo mbalimbali na kucheza.
Katika mtaa wa Lumumba, barabara ilifungwa wakati wananchi hao wakisherehekea ushindi huo. Aidha, askari walitanda katika uwanja huo wakiangalia usalama wa wafuasi hao.
Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM mkoa wa Dar es Salaam, Simba Gadafi,  alisema wataenzi yaliyo mema yaliyofanywa na serikali ya awamu ya nne na kwamba wamejipanga kufanya kazi kikamilifu katika serikali ya awamu ya tano.
 
MAJIMBO YA UCHAGUZI, WAPIGA KURA
Wakati Nec ikitoa matokeo hayo huku ikieleza ni ya majimbo 264 nchini, lakini kwa takwimu za kutangaza matokeo tangu Oktoba 26, mwaka huu, inaonyesha kuwa majimbo yaliyotangazwa ni 258 huku mawili ya Mbeya Mjini na Geita yalitangazwa mara mbili, kati yake CCM ikiongoza kwa kupata kura nyingi kwenye majimbo 209, huku Chadema ikiongoza kwenye majimbo 49. 
Kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu Jumapili iliyopita (Oktoba 25), mwaka huu, Nec ilitangaza idadi ya Watanzania wenye sifa ya kupiga kura kuwa ni 22,751,292. Hata hivyo, wakati wa kutangaza matokeo, Nec ilieleza kuwa waliokuwa na sifa ya kupiga kura ni watu 23,161,440, ikiwa ni tofauti ya watu 410,148.

CHANZO: NIPASHE

No comments: