Social Icons

Pages

Friday, October 30, 2015

MAALIM SEIF: ILICHOFANYA ZEC NI MAPINDUZI

Mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, amesema sababu kubwa ya kufutwa matokeo ya uchaguzi Zanzibar ni baada ya juhudi za kutaka kumtangaza mgombea urais wa CCM, Dk. Ali Mohammed Shein kuwa mshindi wakati hakushinda kukwama.
Maalim Seif alisema hayo wakati akizungumza na Nipashe mjini hapa jana, huku akisisitiza msimamo wake bado upo palepale wa kuitaka Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec) iendelee kuhakiki matokeo yalioyobakia na kisha kumtangaza mshindi wa uchaguzi huo.
“Sababu kubwa ya uchaguzi kufutwa baada ya juhudi za kulazimisha mgombea wa CCM Dk. Shein kuwa mshindi wakati hakushinda kukwama na sie hatutakubali maamuzi ya kidemokrasia ya wananchi kupigwa teke na watu wachache,” alisema.
Maalim Seif alisema uamuzi alioufanya Mwenyekiti wa Zec, Jecha Salim Jecha, ni sawa na kufanya mapinduzi ya kuondoa utawala madarakani jambo ambalo ni kinyume na misingi ya demokrasia na utawala wa sheria.
“Kilichofanyika ni sawa na kufanya mapinduzi kama wananchi wamefanya maamuzi ya kuchagua kiongozi wanaemtaka haiwezekani watu wachache wapinge maamuzi ya wananchi na kuingiza nchi katika mgogoro wa kikatiba?” alihoji.
Maalim Seif ambaye anawania wadhifa huo kwa mara ya tano, alisema Cuf inaendelea kuchukuwa hatua za kidemokrasia kuhakikisha uchaguzi huo unaendelea ikiwamo kuhakiki majimbo yaliyobakia na kuyatangaza na kama juhudi za kidiplomasia zitashindwa chama hicho kimepanga hatua za kuchukua ili haki ya wananchi ipatikane.
Mgombea huyo alisema uamuzi wa Mwenyekiti wa Nec kufuta matokeo yote unavunja Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 pamoja na sheria mbalimbali za uchaguzi ikiwamo kifungu cha 119 (1) kinachoanzisha tume ya uchaguzi na tume hiyo haitakiwi kufanya maamuzi bila ya suala husika kujadiliwa na kukubaliwa na akidi ya wajumbe inayotakiwa kabla ya wajumbe kuamua. 
Alisema hatua ya makamishna wawili wa Zec kutofautiana na uamuzi wa mwenyekiti wao, Cuf ina amini uamuzi wa kufuta uchaguzi ulikuwa ni uamuzi binafsi wa mwenyekiti huyo, kitendo ambacho ni kinyume cha kifungu cha 119(10) ambacho kinaitaka tume izingatie kila uamuzi ujadiliwe na uungwe mkono na wajumbe walio wengi.“Kwa sababu tume haikukaa pamoja ikiwa na mwenyekiti au makamu mwenyekiti na angalau wajumbe wanne na kwasababu na uamuzi uliotolewa ulikuwa ni wa peke yake, kikatiba ni batili na hauna nguvu zozote,” alisema Maalim Seif akiwa ameongozana na Mwenyekiti wa kampeni wa Cuf, Nassor Ahmed Mazrui na msaidizi wake Mansor Yussuf Himid.
“Majimbo 31 ya uchaguzi yameshahakikiwa na tume na matokeo yake kutangazwa baada ya kusainiwa na mwenyekiti na kubakia 23 yakiwamo 18 ya Pemba na hakukuwa na kasoro zilizojitokeza, tunamtaka arudi kazini kumalizia kiporo kilichobakia,” alisema.
Maalim Seif alisema uamuzi wa Mwenyekiti wa Zec wa kufuta matokeo yote ya uchaguzi umeiingiza Zanzibar katika mgogoro mkubwa wa kikatiba na kwamba kuanzia Novemba 2, mwaka huu  visiwa hivyo vitakuwa havina Rais kwa vile aliyepo sasa atakuwa amemaliza muda wake wa miaka mitano kwa mujibu wa katiba ya mwaka 1984.
Aidha, alisema kifungu cha 92 (1) cha Katiba ya Zanzibar kinaelezea uhai wa Baraza la Wawakilishi ni miaka mitano tokea lilipoitishwa na kwamba baraza jipya linatakiwa kuitishwa ndani ya siku 90 kama kinavyosisitiza kifungu cha 90 (1) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.
“Ni Rais yupi ataitisha baraza la wawakilishi, yote haya yanaleta mgogoro wa kikatiba ambao umesababishwa na mtu mmoja anaeitwa Jecha Salum Jecha kwa sababu tu ya kufuata maelekezo ya chama chake cha CCM,” alisema. Maalim Seif alitoa wito kwa Rais wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete na Rais wa Zanzibar,.
Dk. Ali Mohamed Shein, kubeba dhamana ya uongozi kwa siku chache zilizobakia za uongozi wao kwa kusimamia katiba na sheria za nchi ikiwamo kuheshimu maamuzi ya Wazanzibari yaliofanywa Oktoba 25, mwaka huu kupitia uchaguazi mkuu na kuzuia matumizi ya nguvu yanayofanywa na vyombo vya ulinzi dhidi ya raia.
 
WAGOMBEA WENGINE WAGOMA
Wakati huohuo, wagombea sita wa nafasi ya urais wa Zanzibar wametoa msimamo wa pamoja kuwa hawako tayari kushiriki uchaguzi wa marejeo iwapo tume ya uchaguzi itashindwa kuendelea kuhakiki matokeo ya uchaguzi na kumtangaza mshindi.
Wakizungumza na waandishi wa habari mjini Zanzibar JANA, wagombea wa vyama vya Demokrasia Makini, Sau, Chaumma, NRA, Jahazi Asili na DP, walisema sababu alizotoa mwenyekiti wa Zec kufuta matokeo ya uchaguzi huo hazina mashiko ya kikatiba na kisheria kwani kasoro ndogondogo zilizojitokeza tume ilikuwa na uwezo wa kufanya marekebisho bila kuathiri uchaguzi wote.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: