Social Icons

Pages

Wednesday, September 02, 2015

VYOMBO VYA ULINZI NA USALAMA VYAMUAGA RAIS KIKWETE

Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akikagua gwaride rasmi liliandaliwa na vikosi mbalimbali wakati wa sherehe ya kuagwa rasmi na vyombo vya ulinzi na usalama.
Vyombo vya ulinzi na usalama vimemuaga rasmi Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Rais Jakaya Kikwete, ambaye anaelekea kumaliza muda wake wa utawala wa miaka 10.
Sherehe za kumuaga Rais Kikwete zilifanyika jana katika Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam, huku zikiambatana na maonyesho mbalimbali ya kijeshi. Rais Kikwete alipigiwa mizinga ya heshima pamoja na kukagua vikosi mbalimbali vya majeshi ya ulinzi na usalama. 
Aidha, sherehe hizo zilipambwa na shamrashamra za ndege za kivita zilikuwa zikipita angani huku wanajeshi wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wakiwamo makomandoo wakionyesha mbinu mbalimbali za kukabiliana na maadui pamoja na kuwadhibiti.
Pia Jeshi la Magereza lilionyesha namna ya kudhibiti wafungwa mbele ya Rais Kikwete.
Sambamba na hilo pia Rais alishuhudia namna makomandoo wa jeshi walivyo wakakamavu katika kukabiliana na jambo lolote.
Baadhi ya vikundi vya majeshi yaliyokuwa yakifanya maonyesho mbele ya Rais Kikwete ni pamoja na JWTZ, Jeshi la Magereza na Jeshi la Polisi.
Sherehe hizo pia zilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali akiwamo Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal, Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein na Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi, Davis Mwamunyange na Mke wa Rais, Mama Salma Kikwete. 
 
ATUNUKU NISHANI
RAIS amewatunuku nishani mbalimbali maofisa 30 wa majeshi zikiwamo nishani ya utumishi uliotukukuka , nishani ya utumishi wa muda mrefu na nishani ya tabia njema.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: