Taasisi ya kueneza amani nchini ya Global Peace
Foundation (GPFTZ) kwa kushirikiana na Baraza la Wadhamini la Taasisi ya
Viongozi wa Dini Tanzania (IRCPT) imezindua kampeni ya kuhamasisha
amani katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 25,
mwaka huu.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo jijini Dar es Salaam jana,
Mkurugenzi wa IRCPT, Lanon Godela, alisema lengo la kampeni hiyo ni
kuhamasisha wananchi kushiriki uchaguzi huo kwa amani na utulivu.
Alisema katika mkakati wao wa uhamasishaji wamelenga zaidi makundi
ya vijana kwa kuwa ndiyo wengi zaidi ikilinganishwa na makundi mengine
na pia ndilo ambalo limekuwa likishawishika kuingia katika viashiria
vya kuingia katika machafuko.
Kundi jingine alisema ni la wanawake ambao wamekuwa waathirika
wakubwa katika nchi mbalimbali duniani pale yanapotokea machafuko.
Godela alisema kazi kubwa ya kampeni hiyo ni kuwaelimisha wananchi
faida za kushiriki katika uchaguzi kwa amani pasipo kuangalia vyama vya
siasa wanavyotoka bali kuliweka mbele taifa na maslahi yake.
“Kampeni hii imeandaliwa maalum kwa ajili ya kuhamasisha wanawake
na vijana kuwa mabalozi wazuri wa kulinda na kuitetea amani ya nchi hasa
katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu, tunaamini wakipata
elimu watajiepusha na vitendo mbalimbali vya uchochezi na uharibifu wa
amani ya nchi,” alisema.
Godela alisema katika kufanikisha hilo, pia wamepanga kuyafikia makundi hayo kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment