Social Icons

Pages

Friday, June 05, 2015

'SERIKALI ISIKUBALI KUUZA NYUMBA ZA NHC UPANGA'


Chama Cha Wapangaji Tanzania, kimeiomba Wizara ya Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kutokubali kuuza nyumba za Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), zilizopo katikati ya miji hasa Upanga jijini Dar es Salaam, kwa kuwa wanaotaka kuzinunua ni matajiri wachache wenye kiu ya kunufaika na rasilimali za nchi.
Aidha, chama hicho kimeishauri serikali kusitisha upangaji wa muda mrefu kwa nyumba za NHC, ili Watanzania wengi hasa wanaoanza kazi waweze kunufaika na nyumba hizo. Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa chama hicho, Ndumey Mukama, alisema utafiti wao umebaini kuwa kuna wapangaji wa kudumu NHC ambao sasa wanataka kuuziwa nyumba hizo kwa bei ya kutupa wakati tayari wameshajenga nyumba maeneo mengine.
Alisema wapangaji wa muda mrefu wa NHC hasa maeneo ya mjini kama Dar es Salaam ni watu wenye uwezo ambao wengine wamejenga nyumba nzuri na wanazipangisha kwa dola za Marekani, huku wakiendelea kulipa kodi ndogo NHC. Alisema wapo wanasiasa wachache na baadhi ya wapangaji wa muda mrefu wanaong'ang'ania kuuziwa nyumba hizo kinyume cha utaratibu.
Aliishauri Serikali iweke sheria ya ukomo wa upangaji wa nyumba za serikali angalau miaka mitano ili kutoa nafasi kwa Watanzania wengi hasa wanaoanza maisha kuweza kupanga nyumba hizo.
Mukama alisema: "Utaratibu wa sasa wa wapangaji kukaa kwa muda mrefu katika nyumba hizo umewajengea kiburi wapangaji hawa na wamefikia hatua ya kutaka kuuziwa nyumba hizi kwa bei chee wakati ni rasilimali ya Watanzania wote. Hawa wanaouwezo wa kununua nyumba zinazojengwa sasa katika maeneo mengine na NHC wakanunue huko."
Alisema jambo lingine linalowapa kiburi wapangaji wa NHC ni kusikilizwa 'sana' na serikali hata pale ambapo wanakiuka masharti ya upangaji. Chama hicho pia kimeishauri serikali itengeneze sera ya nyumba ambayo itawabana pia wenye nyumba binafsi na kuweka usawa kwenye sekta hiyo.

CHANZO: NIPASHE

No comments: