Social Icons

Pages

Monday, May 04, 2015

UCHAGUZI CCM 2015: AGUSTINO RAMADHANI JAJI MKUU MSTAAFU

Jaji Augustino Ramadhani, akipiga kinanda  wakati wa Ibada katika kanisa kuu la Mtakatifu Albano  jijini Dar es Salaam
Historia yake
Jaji Augustino Ramadhani alizaliwa Desemba 28, 1945 mjini Unguja, Zanzibar akiwa mtoto wa pili kati ya wanane waliozaliwa kwa wazazi wake. Baba yake ni Mathew Douglas Ramadhani, raia wa Zanzibar aliyefariki dunia mwaka 1962.
Watu wengi hushangaa “mkongwe” huyu kuwa na majina mawili ya dini tofauti. Augustino (jina la Kikristo) na Ramadhani (jina la Kiislamu). Lakini ukweli wa mambo ni kuwa yeye ni Mkristo wa dhehebu la Anglikana na ni mchungaji wa kanisa hilo.
Elimu ya msingi aliianzia wilayani Mpwapwa Mkoa wa Dodoma katika Shule ya Msingi Mpwapwa mwaka 1952 -1953 darasa la kwanza na la pili. Baadaye alihamia mkoani Tabora na kusoma darasa la tatu na la nne katika Shule ya Mingi “Town School” mwaka 1954 – 1956. Mwaka 1957 – 1958 alisoma darasa la la sita na la saba katika Shule ya Msingi Kazel Hill (sasa inaitwa Shule ya Msingi Itetemia), kabla ya kurudi Mpwapwa ambako alikamilisha darasa la nane mwaka 1959.
Aijiunga na Shule ya Sekondari ya Wavulana Tabora mwaka 1960-1965 kwa ajili ya elimu ya kidato cha kwanza na nne pamoja na elimu ya kidato cha tano na sita. Baada ya kumaliza elimu ya sekondari alipata fursa ya kujiunga katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akianza kusomea Sheria. Shahada hii nyeti aliisoma kuanzia mwaka 1966 hadi alipohitimu Machi 1970.
Baada ya kuhitimu masomo ya chuo kikuu alijiunga na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mujibu wa sheria na aliajiriwa katika Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), kufanya kazi za uanasheria.
Kwa mtu mwenye shahada ya chuo kikuu enzi za miaka ya 1970, kupanda vyeo kilikuwa kitu cha lazima. Jeshi halikuwa na wasomi wengi kama ilivyokuwa katika sekta nyingine na kila aliyekuwa na elimu kubwa alikuwa mtu muhimu. Ndiyo maana haikushangaza kwamba mwaka 1971 tayari alikuwa Luteni (nyota mbili) akiwa kambi ya Mgulani na miaka sita baadaye akahamishiwa Brigedi ya Faru mkoani Tabora wakati huo akiwa tayari ni Meja.
Kwa kuwa nchi ilikuwa na upungufu mkubwa wa wasomi wa sheria, Rais wa Zanzibar wakati huo, Aboud Jumbe Mwinyi, alimwomba na kumwondoa jeshini Jaji Ramadhani na kumteua kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), mwaka 1978.
Oktoba 1978 aliteuliwa kuwa Jaji Mkuu wa Zanzibar. Mabadiliko mengine yakatokea tena Machi 1979 alirudishwa jeshini, ambako hakukaa muda mrefu; akahamishiwa vitani Uganda kuendesha mahakama za kijeshi (akiwa tayari na cheo cha Luteni Kanali).
Baada ya vita alirejea Zanzibar na kurudishwa kwenye utumishi wa kiraia ambako Januari 1980 aliapishwa kuwa Jaji Mkuu wa Zanzibar. Miaka tisa baadaye aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa ya Tanzania.
Alidumu katika ujaji wa Mahakama ya Rufaa kwa miaka minne hadi alipoteuliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) mwaka 1993. Alikaa NEC hadi Oktoba 2002 alipohamishiwa Zanzibar kufanya kazi kama Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) hadi Oktoba 2007.
Kati ya Novemba 2001 hadi Novemba 2007 aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Afrika Mashariki. Mwaka 2007 alifikia wadhifa wa juu kabisa kwa wanasheria wa Tanzania, alipoteuliwa kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania hadi alipostaafu mwaka 2010. Septemba 2014  aliteuliwa na Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu yenye makao yake jijini Arusha kuwa rais wa mahakama hiyo kwa kipindi cha miaka miwili.
Nguli huyu wa taaluma ya sheria amemuoa mwanajeshi wa ngazi ya juu, Luteni Kanali Saada Mbarouk na wamepata watoto wanne (wawili wanafanya kazi kama wafamasia nchini Uingereza, mmoja ni mwanasheria huko huko Uingereza na mmoja ni mwandishi wa habari hapa Tanzania).

Mbio za urais
Jaji Ramadhani hajatangaza kuwa atagombea urais lakini anatajwa sana ndani ya majukwaa ya kisiasa nchini. Na ile kauli ya Rais Jakaya Kikwete kuwa wagombea wazuri hawajajitangaza inamfanya ahisiwe kuwa mmoja wa “wagombea hao wazuri”.
Vyama vikongwe duniani vinapozidiwa na “mazonge” ya kiutawala na vikahitaji kurekebisha mifumo yao, huwatumia watu wenye sifa thabiti ilimradi hawatokei katika vyama hasimu. Jaji Ramadhani aliyetumikia nchi hii tangu enzi za Tanu na CCM bila shaka alikuwa mwana Tanu mzuri enzi hizo japokuwa kazi yake ya ujaji ilimweka kando kidogo na kushabikia chama anachokipenda.
Lakini pia, kutumikia Serikali na Jeshi kumemfanya awe karibu mno na CCM na mfumo wa nchi na hata nyadhifa nyingi alizopitia katika fani ya sheria hadi kuwa Jaji Mkuu zinataka uteuliwe na Amiri Jeshi Mkuu ambaye hadi leo ni Mwenyekiti wa CCM Taifa.

Nguvu yake
Kati ya watu wote wanaopigiwa chapuo na kutajwa kuwania urais kupitia CCM, ni Jaji Ramadhani pekee unayeweza kusema hana shutuma za kukosa uadilifu na uaminifu kazini. Amefanya kazi ya ujaji kwa mafanikio na hatukuwahi kusikia amehongwa au ametuhumiwa kuhongwa. Sifa hii inaweza kuleta aina ya rais mstaarabu, imara, anayejiamini na anayeweza kuchukua hatua bila kuhofia kuwa machafu yake yatamsuta.
Moja ya matatizo makuu ya Watanzania ni “ukosefu wa haki” katika nyanja zote za maisha yao na bila shaka Jaji Ramadhani amekuwa mtu anayesimamia utoaji na utendaji wa haki kwa kipindi kirefu. Huyu anaweza kuwa aina ya watu wanaoyafahamu matatizo ya Watanzania kwa kina na akiwa mara nyingi sana amekerwa nayo lakini akiwa hayuko katika nafasi za kuyachukulia hatua sahihi kwa sababu, labda yalipaswa kushughulikiwa na mihimili mingine ya dola. Kwa hiyo, anaweza kusimama na kusema kwa uwazi kuwa akipewa uongozi wa nchi anajua wapi pa kuanzia.
Jambo la tatu ni kuheshimika kwa watu wa kada ya kati. Jaji Ramadhani ni mtu anayeheshimika sana kutokana na kazi zake, kada ya wasomi na wanazuoni inafahamu mengi kumhusu na inaweza kutumika kupasha habari zake nzuri kwa wananchi wa chini bila kuulizwa maswali yasiyo na majibu.
Huyu ni mtu anayeaminiwa na wafanyakazi na makundi ya kidini. Wafanyakazi wanamwamini kwa sababu amekuwa mfanyakazi mwenzao mahakamani na jeshini, lakini ni mfanyakazi ambaye hakuwa na madoa mengi na hakuonesha mifano mibaya. Pia, yeye ni mchungaji wa kanisa la Anglikana; madhehebu ya dini yanaweza kuona nchi inahitaji kiongozi mnyenyekevu na mwenye hofu ya “Mungu” kwa dhati na hiyo inaweza kumwongezea uungwaji mkono.

Udhaifu wake
Jambo moja linalomharibia ni kutokaa ndani ya mfumo wa CCM. Nilieleza hapo juu kwamba Jaji Ramadhani amekuwa zaidi serikalini kuliko ndani ya chama na nikasema inawezekana hali hiyo pia ilimsaidia, kwa kiasi fulani, kuwa karibu na viongozi wa CCM. Lakini ukaribu huo haukuwahi kumfanya awe mtendaji ndani ya CCM, hili ni eneo la kwanza linalompa udhaifu wa utambulisho ndani ya chama.
Pili, yeye hafahamiki sana kwa wananchi wa kawaida. Pamoja na kwamba amekuwa Jaji Mkuu wa Tanzania, kwa miaka minne, na Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu, kwa miaka mingi, watu wanaweza kukosa kumbukumbu ya maamuzi mazito aliyowahi kufanya. Kwamba “umewahi kuwa Jaji Mkuu lakini watu wakisaka kwenye rekodi ni nini kikubwa hasa ulikisimamia na kulinda mhimili huo” hawakioni. Huu ni udhaifu kwa mtu ambaye anatarajia kuwa kiongozi wa nchi.
Tatu, katika utumishi wake wa miaka minne kama Mkuu wa Mahakama Tanzania hakuonekana kama mpambanaji mkubwa wa rushwa. Mwalimu Nyerere alikuwa “hachukui rushwa na alipambana na rushwa kufa na kupona”, Jaji Ramadhani naye “hakuwahi kuchukua rushwa lakini hakupambana na rushwa kufa na kupona”. Unaweza kujionea tofauti hiyo.
Tumeshuhudia mahakama zetu zikiendelea kuwa “sehemu ya kutoa na kupokea rushwa”, wananchi wanalalamika na kumwandikia Jaji Mkuu kila kukicha juu ya mienendo ya majaji na mahakimu lakini wakati wake hakuna uchunguzi mkubwa uliowahi kufanywa juu ya mienendo hiyo na hatua thabiti kuchukuliwa. Rushwa haiondolewi kwa kuchukiwa kwa maneno matupu bali kwa vitendo; katika uongozi wake hatukupata kuona yeye na majaji wenzake wenye dhamana wakipambana na rushwa kwa vitendo.
Eneo jingine la udhaifu wake mkubwa linaweza kuangaliwa wakati akihudumu kama Makamu Mwenyekiti wa NEC kati ya mwaka 1993 – 2002. Chini ya uongozi wake na wenzake kulifanyika chaguzi mbili, ule wa mwaka 1995 na ule wa mwaka 2000 zote akishinda Rais Benjamin William Mkapa.
Baadhi ya waangalizi wa ndani na nje ya nchi walitoa tathmini zao zikionyesha kuwa chaguzi zile hazikuwa huru na za haki na kwamba vyombo vya dola vilitumika waziwazi kuisaidia CCM na viliizidi nguvu NEC. Hii ina maana kuwa Jaji Ramadhani amewahi kushuhudia demokrasia ikikandamizwa wakati ana dhamana kubwa ya kusimamia uchaguzi na hakuchukua hatua zozote wala kuonyesha msimamo wa kutenda haki.
Kwa upande mwingine, yeye mwenyewe, kwa mikono yake, amewahi kushiriki katika ukandamizaji wa demokrasia (si kutazama tu, alishiriki!). Hukumu ya Mahakama ya Rufani dhidi ya mgombea binafsi (hoja na kesi ya Mchungaji Christopher Mtikila) ililaumiwa sana na wapigania haki wengi, mashirika binafsi na hata majukwaa ya kidini na baadhi ya wanasheria waliishangaa Mahakama ya Rufaa ya Tanzania ikitoa hukumu ambayo inaifanya mahakama kukwepa wajibu wake wa kusimamia haki hadi ionekane inatendeka.
Katika hukumu hiyo, Jaji Ramadhani na wenzake walijaribu kuzunguka mbuyu wakikwepa kuiudhi Serikali. Sehemu ya hitimisho la hukumu hiyo (tafsiri ni yangu) ilisema: “….Kwa upande wetu, tunasema kwamba suala la mgombea binafsi linapaswa kushughulikiwa na Bunge ambalo lina mamlaka ya kubadilisha Katiba (na uwezo huo) siyo wa mahakama ambazo, kama tulivyoeleza, hazina mamlaka hayo. Uamuzi wa kuanzisha au kutoanzisha mgombea binafsi unategemea mahitaji ya kijamii ya kila taifa kutokana na hali halisi ya historia yake. Kwa hiyo, suala la mgombea binafsi ni la kisiasa na si la kisheria……..”
Hadi sasa baadhi ya wanasheria nguli, nilioongea nao, wanasisitiza kuwa, walau Jaji Ramadhani na wenzake hata kama wangekuwa wanajikosha kwa serikali, wangeweza kuuma na kupuliza na kuhitimisha kuwa “suala la mgombea binafsi ni haki ya kikatiba na kwamba wanaiamuru Serikali isimamie utekelezaji wake”, na kisha Serikali ndiyo ingetumia taratibu zake kuliarifu Bunge lifanye kazi yake.
Katika dunia ya sasa ambapo mihimili ya dola inafanya kazi yake, mahakama yoyote ina wajibu wa kuhakikisha sheria zote zinazowanyima haki wananchi zinabatilishwa. Haiwezekani nchi inakuwa na sheria inayokiuka haki za raia halafu mahakama inatoa hukumu ya kusema Bunge liamue litakavyo “hata kwa jambo linalovunja haki za raia”. Hii ni rekodi nyingine inayoonesha kuwa taswira ya Jaji Ramadhani imewahi pia kutumika vibaya kwa kufanya maamuzi ambayo yanakinzana na uzito wa dhamana aliyowahi kupewa.

Nini kinaweza kumfanya apitishwe?
Jaji Ramadhani anaweza kupitishwa kwa sababu ya taswira yake ya uadilifu, usafi na kuchukia rushwa. CCM ya sasa, iliyochofuka sana, inahitaji mgombea msafi asiye na madoa mengi ili awe na uwezo wa kuwashughulikia bila haya wale wote wanaotumia ofisi za umma kujinufaisha, ikiwa atapigiwa kura na kuwa Rais. Ikumbukwe kuwa huyu ni mwanataaluma nguli na askari mstaafu wa cheo cha juu jeshini na anao uwezo wa kusimamia mambo, labda aamue kushindwa kimakusudi.
Lakini, pia, mtu wa namna hii atajenga taswira safi na kupitia upya malengo na mustakabali wa chama hicho kuona kama anaweza kukirudisha katika malengo yake ya miaka ya 1970, ya kuwatetea wakulima na wafanyakazi ambayo kwa sasa yamekufa.
Kwa sababu hana makundi ndani ya CCM, hili linaweza kumbeba.  Kwamba CCM inatafuta mtu ambaye atayafanya makundi makubwa yanayogombana ndani ya chama hicho yamheshimu; ikikosea kumpata mtu huyo itaparaganyika na kama mtu huyo atakuwa ni Jaji Augustino Ramadhani maana yake makundi hayo yatatishwa na heshima/uadilifu wake na kuanza kumuunga mkono mara moja.

Nini kinaweza kumwangusha?
Kitisho kikubwa kwa wahafidhina ndani ya CCM ni “ugeni” wa Jaji Ramadhani katika chama chao. Pamoja na kuwa kwake karibu na Serikali, jeshi na hata kufahamiana na viongozi wengi wa CCM, hakuwahi kuwa mmoja wa wahafidhina na wale wanaojidai “CCM ni mali yao”. Ikiwa hawa wenye chama watamwekea ngumu, ataanguka.
Jambo jingine ni kwamba ikiwa uongozi wa juu wa CCM utaona yeye ni chaguo la chama hicho, yeye na uongozi wanaweza kukumbana na kisiki kikubwa cha makundi yenye pesa kutumia kila mbinu ili aenguliwe. Watu wa namna yake wanaweza kuonekana kama “watakaotia mchanga kwenye kitumbua cha mabosi, kilichoandaliwa muda mrefu” na dawa yake ni kumpiga fitina kwa nguvu za pesa na kila ushawishi hadi andolewe. 

Asipopitishwa (Mpango B)
Jaji Ramadhani amekwishastaafu mbio za utendaji wa umma, lakini yeye ni mmoja wa wachungaji muhimu wa kanisa la Anglikana. Nilipoongea na ofisa mmoja wa juu wa kanisa hilo alinijulisha kuwa huenda miaka michache ijayo mkongwe huyu akatawazwa pia kuwa askofu kwenye moja ya dayosisi za kanisa hilo. Kwa hivyo, kama hatateuliwa kuwania urais naona ana kazi ya kudumu ya “kuchunga kondoo wa Bwana wasipotee”!

Hitimisho
Aina ya watu kama Jaji Ramadhani ni kitisho kikubwa kwa makundi yaliyojitangaza muda mrefu na kujisuka vilivyo kunasa tiketi ya urais kupitia CCM. Mtu mwadilifu, mwenye rekodi nzuri kiutendaji, aliyepitia jeshini, aliyekuwa jaji wa mahakama kuu hadi jaji mkuu na ambaye sasa anatajwa kugombea urais, lazima tu atatisha. Atatisha kwa sababu ya rekodi zake za kuvutia na kukosa mawaa na kashfa wakati anafanya kazi kwenye sekta ambayo kama angependa angekula rushwa kila siku, lakini alikataa.
Hakika, mzee huyu asidharauliwe hata kidogo. Huenda watu wa namna yake ndiyo kimbilio la CCM kwa sasa, katika wakati ambao chama hicho kinapaswa kufanya maamuzi magumu ili walau kiokoe sehemu iliyobaki katika nyumba inayoungua.

CHANZO: MWANANCHI

No comments: