Social Icons

Pages

Monday, May 04, 2015

ADC: BAJETI 2015/16 WALALAHOI KUUMIA ZAIDI

Chama cha Alliance for  Democratic Change (ADC), kimesema bajeti ya 2015/ 16 inayotarajiwa kusomwa bungeni katika mkutano ujao, itawaumiza wananchi wa hali ya chini.
Kauli hiyo ilitolewa na Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Hassan Doyo, wakati akihutubia wakazi wa kijiji cha Songe Mnadani, Wilaya ya Kilindi, Tanga. Doyo alisema moja ya vitu vinavyoonyesha kwamba bajeti hiyo itamuumiza mwananchi wa hali ya chini ni bei ya mafuta ya ndege ambayo ushuru wake utashushwa.
Alisema ni jambo la kusikitisha kuona huduma zinazotumiwa na watu wa hali ya juu zinashushwa huku zile zinazotumiwa na watu wa hali ya chini zikiendelea kupanda. “Asilimia kubwa ya watu wanaotumia huduma ya usafiri ya ndege ni wenye kipato kikubwa siyo masikini, wengi wanaotumia usafiri wa basi ni walala hoi wasio na kipato kizuri, lakini eti leo hii mafuta ya ndege yanaondolewa ushuru,” alidai Doyo.
Pia alisema kuwa mafuta ya taa yatapanda kwa asilimia 75 na kwamba kama bajeti itapitishwa kama ilivyopangwa, gharama ya maisha kwa watu wa chini itapanda. Aliongeza kuwa hali hiyo itapandisha matumizi katika serikali ijayo itakayoundwa mwishoni mwa mwaka huu.
Aliwaomba Wabunge kuhudhuria kwa wingi katika Bunge hilo ili kuibana serikali isipitishe bajeti hiyo kama ilivyopangwa kwa kuwa kufanya hivyo ni kuwakandamiza wananchi wanyonge. “Najua Wabunge hivi sasa wana mambo mengi, wamejichimbia kwenye majimbo yao kwa ajili ya kujiandaa katika uchaguzi mkuu, ninaomba katika Bunge hilo la bajeti linalotarajia kuanza Mei 12, mwaka huu waache shughuli zao waende kuwapigania wananchi kwa sababu bila kufanya hivyo maisha yatakuwa magumu sana,” alisema Doyo.
Mwenyekiti wa ADC, Said Miraaj, alisema  gharama za maisha ya Watanzania  zimeendelea kupanda huku watu wenye kipato cha chini wakiendelea kunyonywa na walionacho wakizidi kuongezewa. Aliwataka Watanzania kutofanya makosa katika uchaguzi mkuu mwaka huu kwa kuhakikisha wanachagua viongozi wenye nia ya kuwakomboa.

CHANZO: NIPASHE

No comments: